Wednesday, November 30, 2016

MAADHIMISHO YA SIKU YA WALEMAVU KITAIFA YAFUTWA

index
Maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani, ambayo kitaifa yalitarajiwa kufanyika jijini Dar es salaam,Desemba 3, mwaka huu yameahirishwa na badala yake kila mkoa utaadhimisha kivyake.

Akitoa tamko la kuharishwa kwa maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Simbachawene amesema maadhimisho hayo yalilenga kila halmashauri isafirishe wanachama wa vyama vya watu wenye ulemavu ili washiriki maadhimisho hayo jijini humo.

Amesema kwa mujibu wa maelekezo aliyopewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa wakuu wa mikoa kuwa badala ya maadhimisho hayo ya kitaifa kukusanya walemavu wote kwenye mikoa kwenda Dar es salaam yafanyike kwenye mikoa yao.

Tuesday, November 29, 2016

HALMASHAURI ZAONGOZA KWA RUSHWA ZIKIFUATIWA NA POLISI.

mlowolapicha
 Halmashauri nyingi hapa nchini zinaongoza kwa kupokea rushwa kubwa kubwa huku jeshi la polisi likiongoza kwa kupokea rushwa ndogo ndogo suala ambalo limepelekea mapambano dhidi ya rushwa kuwa magumu.

Hayo yameelezwa jana na Mkurugenzi wa Takukuru Valentino Mlowola wakati wa mkutano wa mkuu mwaka wa siku 2 wa Shirikisho la mamlaka za kuzuia na kupambana na rushwa nchi za Afrika Mashariki(EAAACA) unaofanyika jijini Arusha ambapo unawashiriki kutoka mataifa 8 barani Afrika.

Mlowola alisema kuwa Hadi sasa katika kipindi cha mwaka mmoja wa wameweza kuokoa zaidi ya billion 45 za miradi mbalimbali zilizokuwa ziangukie mikononi mwa watu wachache ambapo aliitaka jamii kutoa ushirikiano dhidi ya mapambano ya kuzuia rushwa.

Alisema kuwa miradi mingi inayopitia katika halmashauri nyingi hapa nchini imekuwa ikigubikwa na rushwa na kuifanya miradi hiyo kujengwa chini ya viwango hali inayopelekea matumizi mabaya ya fedha za umma.

Aidha katika jeshi la Polisi alitanabaisha kuwa kumekuwa na ongezeko la kuomba na kupokea rushwa ndogo kutoka kwa jamii hali inayosababisha wananchi kukosa imani na kupelekea malalamiko kwa jeshi hilo.

“Waandishi wa habari iwapo mtaona mradi wowote hauendi kwa viwango vilivyokusudiwa mtoe taarifa kwani hivi sasa tuna maofisa wetu katika kila wilaya ambao wataweza kufanya uchunguzi na kubaini mianya ya rushwa”alisema Mlowola.

Kwa upande wake waziri wa nchi ofisi ya Raisi Utumishi na Utawala Bora  Angela Kairuki alisema kuwa serikali imeanzisha mahakama ya mafisadi ambapo kesi kadhaa zimeanza kusikilizwa hali itakayopelekeakupunguza kuomba na kupokea rushwa hapa nchini.

Alisema kuwa kesi nyingi zimepelekwa katika mahakama hiyo na siku si nyingi mafanikio ya vita dhidi ya ubadhirifu wa mali za umma utapungua kama sio kwisha kabisa

Waziri huyo alitoa wito kwa taasisi mbalimbali za serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha mapambano dhidi ya rushwa katika nchi za ukanda wa afrika mashariki zinakoma.

ASKARI POLISI AFARIKI DUNIA KIBAHA KWA KUJIPIGA RISASI BILA YA KUKUSUDIA.

Askari  Polisi  mwenye namba H.3348 PC  Armand  Evarist  Furaha mwenye umri wa miaka 33 amefariki dunia baada ya kujipiga risasi kwa bahati mbaya.

Taarifa iliyotolewa na  Kaimu kamanda wa  Polisi  Mkoa wa  Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP- Blasius Chatanda imesema tukio hilo  limetokea Tarehe 22 Novemba 2016 majira ya saa moja usiku katika eneo  la maili moja sokoni, kata ya maili moja Tarafa ya Kibaha Wilaya ya Kibaha  mkoani  Pwani.

Kaimu Kamanda Chatanda alisema Marehemu alikuwa amepangiwa lindo kwa mkuu wa wilaya ya Kibaha ambapo baada ya kushuka  kwenye Gari  Bunduki ilfyatuka  na  kumjeruhi na  kwamba alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya rufaa ya Tumbi.

SSP Chatanda alisema marehemu alikuwa mbele katika Gari namba PT 1732  lililokuwa likiendeshwa na Askari mwenye namba F. 3064 CPL Grayson na kutaja Bunduki aliyokuwa nayo marehemu aina ya SMG ambayo ilimpiga kifuani upande wa kushoto.  

Monday, November 28, 2016

MAHAFALI SEKONDARI YA YEMEN, WAHITIMU WATAKIWA KUWEKA MALENGO YA KUENDELEA NA MASOMO.

Wahitimu wa kidato cha 4 Shule ya Sekondari Yemen iliyopo Chang'ombe jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi Mkurugenzi wa Benki ya Amana, Dkt. Muhsin Masoud akizungumza katika mahafali hayo.
.............................
 
Vijana waliomaliza elimu ya sekondari  wametakiwa kuweka malengo ya kuendelea na elimu ya juu ili  kuongeza ufahamu  wa mambo mbalimbali katika maisha yao.

Wito huo umetolewa na mkurugenzi wa Benki ya Amana, Dkt. Muhsin  Masoud alipokuwa akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne katika shule Sekondari yemen iliyopo Chang'ombe jijini Dar es Salaam.

Dkt. Muhsin  ambae alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, amesema Kidato cha nne sio mwisho wa  elimu na kwamba kila muhitimu anatakiwa kujiwekea malengo ya kuendelea na elimu ya  juu.

Aliongeza kwa kusema kuwa, sio lazima ukimaliza kusoma ukaajiriwe bali elimu itakufanya uweze hata  kuendesha mambo yako kwa ufanisi.

Aidha, aliwataka   vijana  wahitimu  kuwa waadilifu  katika shughulizao mbalimbali katika jamii kwani tabia hiyo ya uadilifu  itawajengea heshima na  uaminifu.

Kwa  upande wake Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Astahili Akilimali, amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwasimamia wahitimu hao  ili wadumishe tabia ya  usomaji wa Qur ani kama walivyokuwa shuleni na kuongeza kuwa hali hiyo itaendelea kuwajengea hofu juu ya Muumba wao.

Aliongeza kwa kuwataka wazazi na  walezi ambao bado wana watoto wao  shuleni hapokutoa ushirikiano na walimu ili kufanikisha malezi ya  wa toto katika kuwapatia elimu.

Alisema haipendezi kwa mzazi  kukaa kimiya bila ya  kuuliza maendeleo ya mwanae kwa mwalimu na kusema kuwa hali hiyo itapelekea mtoto afanye anachotaka kwakuwa hakuna wa kumfuatilia mambo yake.

Nao wahitimu wa kidato cha nne katika shule hiyo ya Yemen  wamesema kuwa wamefurahi  kumaliza kidato cha nne katika shule hiyo na kwamba wamejifunza mambo mbalimbali yakiwemo yanayohusu dini yao.

Aidha, wahitimu hao wameahidi kuendeleza tabia njema walizopata shuleni hapo ili wawe  mfanowa  kuigwa katika jamii.
Meneja wa Shule za Yemen, Jamila Awadh, akizungumza katika mahafali hayo.

Wahitimu wasichana wa kidato  cha 4 Sekondari ya Yemen wakiwa katika mahafali.
Kutoka  kushoto ni  Meneja wa shule za  Yemen, Jamila Awadh, wa  pili kushoto ni mkuu wa shule ya Awali, Sheikha Saad na wa kwanza kulia ni  Afsa rasilimali watu, Anaf Saleh  Karama.
Kutoka kushoto ni  Mgeni rasmi, Dkt. Muhsin Masoud, wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya shule za Yemen Hassan Akrabi na wa mwisho kulia ni kiongozi  wa wazazi wa shule ya Sekondari Yemen, Abdulazizi Hassan.
Mgeni Rasmi, Dkt. Muhsin Masoud akifuatilia mahafali hayo.
Mwalimu mkuu wa shuleya Sekondari ya Yemen Astahili Akilimali akizungumza  katika Mahafali hayo.
 Mwenyekiti wa Bodi ya shule za Yemen Hassan Akrabi akizungumza katikaMahafali hayo.
Wazazi na walezi wakichukua picha za matukio kupitia simu zao za mkononi.