Picha
ya pamoja baina ya wawakilishi wa makampuni ya uwekezaji kutoka nchini China na
viongozi wa mkoa wa Pwani akiwemo mkuu Wa Mkoa huo mhandisi Evarist Ndikilo wa
katikatika kati ya walioketi, Na wa kwanza kulia aliekalia kiti ni katibu
tawala mkoani hapo Zuberi Samataba na wa kwanza kulia ni mmoja wa wawekezaji
hao aitwae Liv Ming .
..........................
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha.
WAWAKILISHI wa makampuni ya uwekezaji toka nchini China ,waliofika mkoani
Pwani kuangalia fursa za uwekezaji ,wamefurahishwa na kuvutiwa na fursa nyingi
walizoziona na kuonyesha nia ya kuwekeza.
Aidha wameeleza watatuma wataalamu wao watakaojua wawekeze kwenye sekta
gani kati ya maeneo na sekta waliyoonyeshwa ili kujiletea manufaa.
Wakizungumza baada ya kumtembelea mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist
Ndikilo walieleza, baada ya kuonyeshwa maeneo hayo ya uwekezaji kwa njia ya
video ,wameguswa na kufurahishwa kuwekeza mkoani hapo.
Mmoja wa wawakilishi wa wawekezaji hao, Liv Ming aliipongeza nchi ya Tanzania
kwa ushirikiano na mahusiano yake na nchi yao ,tangu enzi za marais Julius
Nyerere na Mao Tse Sung.
“Tumejionea fursa nyingi za kiuwekezaji na tutatuma wataalamu wetu kuja
kuangalia na kutupa ushauri tuwekeze kwenye eneo gani kwani tumeona uwekezaji
kwenye sekta ya umeme, vipuri vya magari na uhifadhi wa mazao-kilimo,” alisema
Ming.
Ming alieleza kuwa,wameona maeneo mbalimbali kwa njia ya video ambayo
wanaweza kuwekeza na wataendelea kufanya mawasiliano na mkoa kwa ajili ya
masuala ya uwekezaji wa viwanda kwenye sekta mbalimbali.
“Tumevutiwa na mambo mengi pia kuna baadhi ya makampuni ya wenzetu kutoka
China wamewekeza viwanda zaidi ya miaka 20 hivyo tutaendelea kuhamasisha
wenzetu nao waje kuwekeza,” alisema Ming.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo alisema ,ujio wa
wageni hao ni faraja kwa mkoa huo na Taifa kijumla kwani itasaidia azma ya
serikali ya kuwa nchi ya viwanda.
Alielezea ,mkoa utaendelea kuhamasisha wawekezaji wa nje na ndani ya nchi
ili wawekeze kwenye sekta mbalimbali zilizopo.
Mhandisi Ndikilo,alisema wamejipanga kuwa ukanda wa viwanda kufikia
malengo ya serikali ya awamu ya tano ya nchi ya viwanda na uchumi wa kati.
Ujio wa wawekezaji hao ni kufuatia ziara ya wiki mbili iliyofanywa na
timu ya baadhi ya viongozi mkoa wa Pwani wakiwemo viongozi na wataalamu
waliokwenda kujifunza uhamasishaji na masuala ya uwekezaji nchini China mwezi
Oktoba mwaka huu .
Katika safari hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa ambapo waliweza
kuzungumza na makampuni 106 huku 30 kukubali kuja mkoani Pwani kwa ajili ya
kuangalia maeneo ya uwekezaji na hatimae kuwekeza.
No comments:
Post a Comment