Wednesday, November 8, 2017

TEMBO WAHARIBU MAZAO KIWANGWA/MKANGE.



Diwani wa kata ya Kiwangwa Malota Kwaga,akitoa taarifa ya kata kwenye kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Chalinze .(picha na Mwamvua Mwinyi)
...........................................

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze.

WIMBI la tembo limeibuka na kuharibu mazao ya wakulima wa baadhi ya vijiji vya kata ya Kiwangwa ,Mkange na Kibindu vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Saadan na vilivyo karibu na Mto Wami .

Aidha watu watatu wanadaiwa kuuawa kutokana na wanyamapori wakiwemo tembo na fisi.

Kati ya watu hao wawili wamefariki baada ya kujeruhiwa na fisi katika kijiji cha Kiwangwa na mtu mwingine alikufa kutokana na kujeruhiwa na tembo huko kwa Kwamduma.

Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha madiwani cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ngazi ya kata kipindi cha robo mwaka ,diwani wa kata ya Kiwangwa Malota Kwaga ,alisema tembo wamekuwa tatizo na kutishia maisha ya watu .

Alieleza mazao yaliyoliwa zaidi ni matikitimaji ,mapapayi,mahindi,migomba na nyanya.

Kwaga alisema ,zipo hatua alizozichukua ambazo ni kupeleka taarifa halmashauri na wilaya idara ya ardhi maliasili na utalii.
“Idara husika ilisema ipo sheria ya kulipa kifuta jasho walioathiriwa ama kuuawa na wanyamapori “
“Kwa upande wangu kauli hii hainifurahishi na haina mashiko kwani wakulima wameshapata hasara lakini badala ya kulipwa fidia wanaambiwa wanalipwa kifuta jasho” alieleza Kwaga.

Kwaga alisema pia hifadhi ya Taifa -TANAPA na baadhi ya viongozi wa halmashauri walikwenda kuzungumza na wananchi juu ya tatizo hilo na kutoa elimu .

Alisema kwasasa wakulima walioliwa mazao yao wameshaorodheshwa majina yao na watakwenda kufanyiwa uhakiki kwa ajili ya kulipwa fedha hizo .

Nae mkuu wa idara ya ardhi na maliasili katika halmashauri ya Chalinze ,Zaina Kijazi alikiri kuwepo kwa tatizo la wanyamapori tembo na kiboko kula mazao ya wakulima.

Alisema tembo wameharibu mazao hekari zaidi ya 200 ,kifo cha mtu mmoja kilichosababishwa na tembo na  vifo viwili vilivyotoka na fisi.

Zaina alisema tembo wanangia kwenye maeneo ya wakulima ni kutokana na kukariri njia ya mapito yao kutoka Saadan wakielekea Wamimbiki na Mikumi .
Tembo ni wanyama wanaopenda kula maboga,miwa na matikitimaji hivyo ni changamoto kwani ndio mazao yanayolimwa zaidi na wakulima hao.

Kwa upande wake mkulima wa kijiji cha Matipwili Deus Mabirika alieleza ,mazao yake yameharibiwa katika hekari moja ambapo miche ya mipapayi 294 aliyoinunua kila mche 5,000 imeharibiwa yenye gharama ya mil.1.470.

Alisema kati ya hasara aliyoipata ameambiwa atapatiwa kifuta jasho 50,000 kiasi ambacho ni kidogo .

Mabirika aliiomba wizara ya maliasili kuangalia suala hilo kwani fedha hizo ni ndogo hazikidhi mahitaji.


Baadhi ya madiwani,watendaji na wakuu Wa Idara katika Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani ,wakisikiliza taarifa kutoka kwa diwani wa kata ya Kiwangwa Malota Kwaga, wa pili kulia ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Halmashauri ya  Chalinze, Zaina Kijazi. (picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments:

Post a Comment