Chama cha Wamiliki wa Mabasi
Yaendayo Mikoani (TABOA) na Umoja wa Wasafirishaji Abiria Jijini Dar es Salaam
(UWADAR) wamekanusha taarifa inayosambazwa kwenye mitandao kuwa Novemba 14
mwaka huu watakuwa na mgomo wa kusitisha huduma za usafirishaji.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa UWADAR, Kismat
Dhalla wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwa ajili ya kukanusha suala
hilo.
Dhalla amesema kuwa taarifa hiyo iliandaliwa na vyama hivyo lakini
ilishatolewa katika vyombo vya habari siku nyingi zilizopita hivyo kuna baadhi
ya watu wameamua kuisambaza upya bila ridhaa ya wahusika.
“Ni kweli ile taarifa ni ya kwetu lakini tulishaitoa siku nyingi na mgomo
huo haukufanyika kwa kuwa tuliahidiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini
na Nchi Kavu (SUMATRA) kuwa itayafanyia kazi madai yetu”, alisema Dhalla.
Dhalla ameongeza kuwa tayari SUMATRA imeandaa mkutano na wadau ambao
utafanyika mnamo Novemba 15 mwaka huu kwa ajili ya kujadili kuhusiana na baadhi
ya Kanuni zilizotungwa katika Sheria hiyo ya SUMATRA.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa SUMATRA, Tumaini Silaa
amesema kuwa lengo la SUMATRA ni kuhakikisha kuwa usafiri unapatikana muda wote
na unamfaidisha msafiri na msafirishaji ndio maana mamlaka hiyo inajitahidi kuyamaliza
malalamiko ya TABOA na UWADAR pindi yanapojitokeza.
“Sisi kama SUMATRA tunaona kuwa hakuna mgogoro kati yetu na wadau wa
usafiri isipokuwa ni kutoelewa Kanuni ambazo zimepitishwa na Mhe. Waziri mwenye
dhamana hivyo tutakapokutana katika mkutano huo tutaeleweshana kwani tunaamini
kuwa kanuni zilizoandaliwa ziko vizuri”, alisema Bw.Silaa.
Amefafanua kuwa baadhi ya watu bado wanachanganya Kanuni za mwaka 2007
ambazo zimefutwa na kanuni hizi mpya lakini wanatakiwa kufahamu kuwa kanuni
mpya zimeweka usawa kwa upande wa msafirishaji, abiria, dereva na kondakta.
Pia, kanuni hizo mpya bado hazijaanza kutumika mpaka pale SUMATRA
itakapotoa elimu ili kila mmoja awe na uelewa na Sheria na Kanuni zake.
No comments:
Post a Comment