Serikali imesema itahakikisha vijiji vyote visivyo na umeme vinapata
umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme vijijini awamu ya Tatu (REA-III)
unaotegemewa kukamilika mwaka 2020/21.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati
Mhe. Subira Mgalu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea Hassan Masala
juu ya mpango wa Serikali katika kusambaza umeme katika kata zilizobaki
wilayani Nachingwea kupitia REA III.
“Mradi wa REA III utajumuisha vipengele vitatu vya Densification, Grid Extension na Off grid renewable ambapo Mkoa wa Lindi chini ya miradi ya
uendelezaji wa grid (Grid extension) katika Mzunguko wa kwanza unatekelezwa kwa
muda wa miezi 24 na Kampuni ya Stategrig & Technical Works Ltd,” alifafanua
Naibu Waziri huyo.
Aliendelea kwa kusema, katika wilaya ya Nachingwea mpango wa Awamu ya
Tatu utavipatia umeme vijiji 30 ambapo kazi za utekelezaji wa mradi zilianza
Julai mwaka huu na zinatarajiwa kukamilika Juni 30, 2019.
Mgalu amesema, vijiji vilivyobakia vitapatiwa umeme katika mzunguko wa
pili wa REA III utakaoanza Aprili, 2019 hadi Desemba 2021.
Vile vile amesema, kazi ya kupeleka umeme mzunguko wa kwanza itahusisha
ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 380,
ufungaji wa transfoma 18, ujenzi wa njia za msongo wa kilovoti 0.4 zenye urefu
wa kilomita 360 na uunganishaji wa wateja 5,710 katika Mkoa mzima wa
Lindi.
Aidha amesema, kwa upande wa Wilaya ya Nachingwea jumla ya wateja 1,200
wataunganishwa, ambapo kwa sasa Mkandarasi anaendelea na upimaji wa njia za
umeme na tayari amefikia asilimia 30 na kazi za upimaji zitakamilika mwishoni
mwa Novemba 2017.
No comments:
Post a Comment