Saturday, November 18, 2017

MGOGORO WA RAZABA CCM BAGAMOYO YAINGILIA KATI.



Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Abduli Rashidi Sharifu amesema Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Bagamoyo kinatambua uwepo wa kjiji cha Winde na kwamba hakijawahi kuvunjwa wala kuondolewa kwenye ramani ya Bagamoyo.

akizungumza katika Mkutano ulioitishwa katika kijiji cha Winde kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo, Sharifu amesema Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) ina mipaka yake na wananchi wa winde wana mipaka yao hivyo kila mmoja anapaswa kuheshimu mipaka yake.

Mwenyekiti huyo mpya wa CCM wilayani Bagamoyo, alisema CCM Bagamoyo itasimia haki katika kuhakikisha kila upande unapata haki stahiki na si vinginevyo.

Aidha, ametoa wito kwa wenyeji wote wa kijiji cha Winde kuhakikisha wanayaendeleza maeneo yao kwa kuyalima na kujenga nyumba kwaajili ya makazi badala ya kuacha mapori hali inayopelekea kuonekana kama hakuna wenyewe.

Alisema kazi ya CCM ni kusimamia ilani yake na hivyo isingependa kuona wananchi wanaoishi ndani ya serikali ya chama cha mapinduzi wananyanyasika kwa jambo ambalo linaweza kuzungumzika.

Aliongeza kwa kusema kuwa kwa nafasi yake yeye Mwenyekiti wa chama atafuatilia ngazi ya serikali ili kuona namna ya kuwasiliana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuangalia uwezekano aidha kuwalipa fidia wananchi wa kijiji cha winde kwa thamani ya sasa au kuwaachia maneo yao ya asili wandelee na shughuli zao kama kawaida.

Alisema katika kuhakikisha Mchakato huo unapewa nguvu jina la kitongoji hicho lirudishwe ambalo ni Winde badala ya Razaba na kwamba Tawi la CCM lianzishwe na kurudisha kitongoji chake cha asili cha Winde.

Awali wakisoma risala mbele ya Mwenyekiti wa CCM wilaya wananchi wa kitongoji hicho RAZABA Kata ya Makurunge Halmashauri ya Bagamoyo wilaya ya Bagamoyo, wamesema mgogoro kati yao na Ranchi ya ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) umechukua zaidi ya miaka 40 sasa bila ya mafanikioa.

Walisema wanachi wa Winde wanatambua uwepo wa RAZABA lakini tatizo ni pale RAZABA ilipotanua mipaka yake na kuingiza kijiji chote cha Winde kwenye miliki yao kitu ambacho sio sahihi kwakuwa wanachi hao hawakushirikishwa.

Aidha, kupitia vikao mbalimbali wananchi hao wameiomba serikali ya awamu ya tano kuingilia kati mgogoro huo na hatimae wananchi hao wabaki kwenye maeneo yao na kuendeleza shughuli zao.



Mgogoro huu wa watu wa kijiji cha winde na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo RAZABA umedumu kwa zaidi ya miaka 40 sasa huku RAZABA ikidai kuchukua eneo hilo kwa kuwalipa fidia wananchi hao toka mwaka 1976 na wananchi wa kijiji cha winde wakidai hawajawahi kulipwa fidia.

Kwa mujibu wa mtendaji wa RAZABA ambae hakutaka kutajwa jina lake wala kurekodiwa kwa madai kuwa sio msemaji wa RAZABA,  amesema Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo imeanzishwa mwaka 1976 mwezzi wa kumi na kwa makubaliano kati ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo jumla heka 77,663 zilikabidhiwa kwa serikali ya mapinduzi Zanzibar chini ya wizara ya kilimo na maliasili kwa lengo la ufugaji wa Ng'ombe na kwamba wananchi wote walilipwa fidia toka wakati huo.  
 

  Wananchi wa kitongoji cha RAZABA Kata ya Makurunge Halmashauri ya Bagamoyo wilaya ya Bagamoyo,wakionyesha mabango yao kudai Ardhi yao ambayo kwa sasa inamilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) kwenye mkutano uliofanyika leo Tarehe 18 Novemba 2017, kitongoji cha RAZABA.


Wananchi wa kitongoji cha RAZABA Kata ya Makurunge Halmashauri ya Bagamoyo wilaya ya Bagamoyo,wakiwa kwenye mkutano wao kudai Ardhi yao ambayo kwa sasa inamilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) kwenye mkutano uliofanyika leo Tarehe 18 Novemba 2017, kitongoji cha RAZABA.


Bango linaloonyesha kwamba eneo hilo linamilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) chini ya wizara ya kilimo na maliasili ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.


No comments:

Post a Comment