Mkurugenzi wa Amana
Bank Dkt. Muhsin Masoud akizungumza na waandishi wa Habari.
Amana Bank imefanikiwa kupata wateja wapya elfu
ishirini katika kipindi cha mwaka 2017 ikiwa ni asilimia 25 ya wateja wote toka
kuanzishwa kwake mwaka 2011.
Akizungumza na waandishi wa Habari katika
kuadhimisha miaka sita toka Benki hiyo ilipoanza kutoa huduma, Mkurugenzi wa Amana
Bank Dkt.
Muhsin Masoud alisema Benki hiyo kwa sasa imeongeza wateja wake na
kuongeza huduma mbalimbali katika matawi yake.
Maadhimisho hayo ya miaka sita yamekwenda
sambamba na wiki ya huduma kwa wateja iliyoanza leo Tarehe 20 mwezi wa 11 mpaka
25 kwa mwaka huu 2017.
Dkt. Muhsin alisema uboreshaji wa huduma pamoja
na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo zimewavutia wateja na kuahidi kuboresha
zaidi utoaji wa huduma katika matawi yake yote.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi
hiki cha miaka sita ni pamoja na kuwa na bidhaa mbalimbali ambazo zinakidhi
mahitaji wa wateja, ikiwemo kuanzisha mikopo kwa wafanyabiashara wadogowadogo
ambayo inaanzia milioni moja hadi milioni kumi.
Alisema katika kuhakikisha Benki hiyo inakuza
mitaji kwa wateja wake kupitia mikopo isiyokuwa na riba kwa wafanyabiashara
wadogo wadogo, tayari mpaka sasa Benki hiyo imeshatoa shilingi za kitanzania
Bilioni moja na nusu.
Alisema miongoni mwa mafanikio ni kuanzishwa kwa
kadi za Master Card ambayo itamuwezesha mteja kupata huduma kwenye ATM yoyote
inayotumia mfumo wa Master Card na kupata huduma za kibenki hata akiwa nje ya
nchi.
Alisema kwa sasa Benki hiyo ina matawi saba nchi
nzima na kwamba hivi karibuni inatarajia kufungua tawi lingine mkoa wa Tanga huku mawili mengine yakitarajiwa
kujengwa katika mikoa ambayo bado haijawekwa wazi ikiwa lengo ni kufikisha
matawi kumi kwa mwaka 2018.
Aliongeza kwa kusema kuwa katika kuhakikisha
wananchi wanapata huduma za Benki hiyo hata katika maeneo ambayo Amana Bank
haina matawi, imesajili mawakala zaidi ya 300 ambao wanatoa huduma za kibenki
kupitia huduma ya Amana Bank Mtaani.
Aidha, alisema licha ya kuwepo matawi saba kwa
sasa, huduma ya Amana Bank Mtaani pia wateja wanaweza kupata huduma za kibenki
kupitia mtandao ikiwemo huduma kwa njia ya simu (Mobile Internet) pamoja na
Internet Banking.
Dkt. Muhsin alisema licha ya kuwa Benki hiyo
inafanya shughuli zake kwa kufuata misingi ya sheria za kiislamu haina maana
wanaohudumiwa ni waislamu pekee.
Alisema toka kuanzishwa kwake watu wa dini zote
wanahudumiwa kama kawaida na kwamba wengi wasiokuwa waislamu wamenufaika na
mfumo huo wa kiislamu ambao hauna riba ndani yake.
Aliongeza kuwa, katika uislamu imeharamishwa riba
na imeruhusiwa biashara, hivyo Benki hiyo ya Amana inafanya biashara na wateja
wake na ndio msingi wa kuendesha Benki hiyo.
Akifafanua zaidi alisema Benki hiyo haikopesha
pesa taslimu na kwamba mteja atapewa kitu au huduma ambayo alipaswa kuipata kwa
pesa taslimu na kupewa muda wa kulipa kitu hicho au huduma hiyo kwa bei ambayo
watakuwa wamekubaliana kama ilivyo biashara yoyote ile.
Alisema mfumo huo umewanufaisha wengi kwani mtu
anapata kitu alichotaka na kuepuka kutumia pesa nje ya malengo hali
iliyowavutia hata wasiokuwa waislamu kufungua Akaunti katika Benki hiyo.
Dkt. Muhsin Alisema nchi za ulaya zinaendesha
mfumo huo wa Benki za kiislamu na kwamba wamenufaika kwa kuinua hata uchumi wa
nchi.
Akizungumzia taarifa zilizosambazwa kwenye
mitandao zikisema Benki ya Amana imefungwa, Dkt. Muhsin alisema taarifa sio za
kweli na kwamba tayari juhudi za kuwatafuta walihusika na kusambaza taarifa
hizo zinafanywa na mamlaka zinazohusika ili kuwachukulia hatua za kisheria.
Alisema Benki hiyo haijafungwa na inaendelea na
shughuli zake kama kawaida katika matawi yake yote hapa nchini.
Kufuatia uzushi huo wa kufungwa kwa Benki ya
Amana, Benki kuu ya Tanzania (BoT) Novemba 17 mwaka huu imewataka wananchi
kupuuza taarifa hizo na kuziita ni za uzushi na zimetolewa kinyume cha sheria.
Mtaalamu wa Mfumo Benki za Kiislamu wa Amana
Bank, Jamali Issa amewataka wananchi kutumia fursa hiyo ya wiki ya huduma kwa
wateja ili kujua na kupata huduma zinazotolewa na Benki hiyo pekee inayofuata
misingi ya sheria ya kiislamu hapa nchini.
Alisema wananchi wanaweza kufika tawi lolote la
Amana Bank na kupata huduma mbalimbali ikiwemo jinsi ya kufungua Akaunti, kujua
taratibu za mikopo na Aina mbalimbali za Akaunti zinazoweza kufunguliwa ndani
ya benki ya Amana.
Jamali alisema wiki ya huduma kwa wateja imeanza
leo Tarehe 20 Novemba na kufikia kilele chake Tarehe 25 mwezi huu wa Novemba
2017.
Mkurugenzi wa Amana
Bank Dkt. Muhsin Masoud akiwa na mteja wa kwanza katika Benki hiyo Dawson
Ishengomawakikata utepe kuashiria uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja na maadhimisho ya miaka sita toka kuanza kutoa huduma kwa Banki hiyo.
Mkurugenzi wa Amana
Bank Dkt. Muhsin Masoud akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani).
Mtaalamu wa Mfumo Benki za Kiislamu wa Amana
Bank, Jamali Issa akizungumza na waandishi wa Habari.
Mkurugenzi wa Amana
Bank Dkt. Muhsin Masoud akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Benki hiyo.
No comments:
Post a Comment