Wednesday, November 22, 2017

UMEME WA UHAKIKA WAJA - WAZIRI WA NISHATI AKIWA BAGAMOYO.


Serikali imesema inaboresha upatikanaji wa umeme ili kukabiliana na mkakati wa kuwa Tanzania ya viwanda ambayo inahitaji umeme wa uhakika.

Kauli hiyo imetolewa jana tarehe 21 Novemba 2017 mjini Bagamoyo na waziri wa Nishati Merdard Kalemani alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme kilichopo kijiji cha Kidomole kata ya Fukayosi.

Alisema tayari limetengezwa toleo la kuongeza mega watts  kutoka Kinyelezi namba 2 ambazo zitaanza kuchukuliwa kuanzia Tarehe 7 Desemba mwaka huu 2017 na kwamba kila mwezi zitachukuliwa mega watts 30 kuziingiza kwenye Grid ya taifa na lengo ni kuchukua mega watts 240 ifikapo mwezi Agosti 2018 na hivyo kuondoa tatizo la umeme hapa nchini.

Alisema nchi ya viwanda inahitaji umeme wa uhakika ili kuweza kuzalisha bidhaa mbalimbali kutoka viwandani hivyo serikali imejipanga kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika ili kuwafanya wawekezaji wawe na uhakika wa kuzalisha bidhaa zao za viwandani.

Akizungumzia kiwanda hicho cha nguzo za umeme zinazotengenezwa kwa kutumia zege, Waziri kalemani alisema uwepo wa kiwanda hicho ni hatua nzuri katika kukuza uchumi wa viwanda hpa nchini.

Alisema mwezi juni mwaka huu serikali imepiga marufuku uingizwaji wa nguzo za umeme kutoka nje ya nchi ili zitumike zile zinazozalishwa hapa nchini.

Aliongeza kwa kusema kuwa, nguzo hizo zinazotengenezwa kwa zege ni bora ukilinganisha na zile za miti ambazo hazidumu muda mrefu.

Alifafanua kuwa nguzo za miti zinadumu kati ya miaka mitatu hadi mitano wakati zile zinazotengenezwa na zege zinadumu kwa muda wa miaka 70.

Aidha, waziri Kalemani alisema kuanzia tarehe 01 Desemba serikali kupitia shirika la umeme nchini litanunua nguzo kutoka katika kiwanda hicho ili kuzitumia katika miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Umeme wa Stiegler's.

Alisema mradi wa Umeme wa Stiegler's ni mradi mkubwa utakaowezesha kupatikana kwa umeme wa uhakika na kusema kuwa mradi huo na mingine itasaidia kufikia malengo ya kuwa na umeme wa uhakika wa mega watts 5000 kwenye grid ya taifa  mwaka 2020 ambao ni umeme mkubwa ukilinganisha na umeme uliopo sasa wa mega watts 1451 tu. 

Waziri Kalemani alimponeza Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Hemed Mwanga kwa kufanikisha wilaya yake kuwa na viwanda vingi ili kwenda sambamba na malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Magufuli katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.

Alisema kwa viwanda vilivyopo wilaya ya Bagamoyo na mkoa wa Pwani kwa ujumla iko haja ya kufanya juhudi ili kuhakikisha Mkoa wa Pwani unakuwa na umeme wa kutosha kwaajili ya uendeshaji wa viwanda hivyo. 

Awali akitoa taarifa ya uzalishaji Mwenyekiti wa Bodi ya kiwanda hicho cha East Africa Infrastructure Engineering Limited, Otieno Igogo alisema kwa sasa Kiwanda hicho imesimamisha uzalishaji wake kutokana na changamoto ya kukosa soko la kuuzia nguzo hizo hali inayosababisha hasara katika uendeshaji wa kiwanda hicho.

Alisema nguzo hizo za zege zinazojulikana kama Pre Stressed Concrete Poles ni teknolojia ya kisasa ambayo inawezesha nguzo hizo kudumu kwa miaka 70 ambayo itasaidia kuokoa fedha za kunua nguzo za miti kila wakati.

Kiwanda cha East Africa Infrastructure Engineering Limited, kinajishughulisha na uteengenezaji wa nguzo za umeme ambazo zinatengenezwa kwa zege.

 Uwekezaji wa Kiwanda hicho umgharimu shilingi za kitanzania Biloni 13 kipo kijiji cha Kidomole kata ya Fukayosi, Halmashauri ya Bagamoyo wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani. 
 Waziri wa Nishati Merdard Kalemani kushoto akipena mikono na Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda hicho, Otieno Igogo mara baada ya mwenyekiti huyo wa bodi kumaliza kusoma taarifa yake mbele ya waziri jana tarehe 21 Novemna 2017.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Hemed mwanga akimkaribisha Waziri wa Nishati Merdard Kalemani katika kiwanda cha East Africa Infrastructure Engineering Limited.

Mkuu huyo wa wilaya alitumia nafasi hiyo kumshukuru Waziri wa Nishati kwa kukubali wito wake na kufika katika kiwanda hicho ili kujionea uwekezaji uliofanywa na Mtanzania katika kuitikia wito wa Rais Dkt. john Magufuli wa Tanzania ya viwanda inawekana.
Sehemu ya nguzo za zege (Pre Stressed Concrete Poles) zinazotumika kusambazia umeme ambazo zinazalishwa na Kiwanda cha East Africa Infrastructure Engineering Limited, kilichopo kijiji cha Kiromo Kata ya Fukayosi Wilayani Bagamoyo.
 Waziri wa Nishati Merdard Kalemani (kulia) akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya kiwanda hicho, Otieno Igogo mara baada ya kumaliza kutembelea kiwanda hicho.
 Waziri wa Nishati Merdard Kalemani (kulia) akiagana na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga, mara baada ya kumaliza kutembelea kiwanda hicho.

No comments:

Post a Comment