Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsindikiza mgeni
wake Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi wakati akielekea kupanda ndege mara
baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili hapa nchini
..............................
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri amesifu ushirikiano kati ya taasisi
za Tanzania na Misri zinazoshughulikia mapambano dhidi ya rushwa na kumpongeza
Rais John Pombe Magufuli kwa kuonesha mfano wa uongozi bora unaopambana na
maovu katika nchi yake.
“Nampongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kupambana na rushwa na
ufisadi na huo ni mfano wa sifa za uongozi bora” alieleza Rais Al Sisi wakati
akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam.
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Taasisi ya
Udhibiti wa Utawala ya Misri (Administration Control Authority of Egypt)
zimekuwa na ushirikiano wa karibu kwa kubalidilishana utaalamu, uzoefu na mbinu
katika kutekeleza majukumu yao.
Katika mkutano, huo ambao uliofanyika mara baada ya kumalizika mazungumzo
rasmi kati ya nchi hizo, Rais Al Sisi alieleza dhamira ya nchi yake ni
kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuunga mkono jitihada za kuleta amani
barani Afrika na kuendelea kuwa na msimamo mmoja katika masuala ya kimataifa.
“Tunampongeza Rais Magufuli na Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika
kutafuta amani barani Afrika hasa katika eneo la Maziwa Makuu” Rais Al Sisi
alisema na kumpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa kwa jitihada
zake za usuluhishi katika mgogoro wa Burundi.
Rais huyo ambaye alikuwa nchini kwa ziara rasmi ya siku mbili, ameeleza
kutambua mzigo mkubwa inaoubeba Tanzania katika kushughulikia migogoro ikiwa ni
pamoja na kuhudumia maelfu ya wakimbizi kutoka katika nchi mbalimbali.
Katika mkutano ambao ulihutubiwa pia na mwenyeji wake Rais Magufuli, Rais
huyo wa Misri alieleza utayari wa nchi yake kuendeleza na kuimarisha uhusiano
wake na Tanzania kwa kuhimiza kubuni na kutekeleza miradi ya pamoja, kuongeza
biashara na uwekezaji pamoja na kubadilishana wataalamu.
”Misri na Tanzania hatma yao ni moja, tutaendelea kushirikiana kwa
hali na mali na kwa kuwa tuna dhamira, matumaini yetu makubwa ni kufanikiwa”
Rais Sisi alisisitiza.
Kabla ya mkutano huo na wanahabari, Rais wa Misri alikuwa na mazungumzo
ya faragha na mwenyeji wake Rais Magufuli na baadae kuhudhuria mazungumzo rasmi
ya mashauriano kati ya Tanzania na Misri.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama
pamoja na mgeni wake Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi wakati wa nyimbo za
mataifa mawili zikipigwa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere(JNIA). Rais huyo wa Misri ameondoka mara baada ya kumaliza ziara yake
ya siku mbili hapa nchini
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Rais wa
Misri Abdel Fattah Al Sisi mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili
nchini.
No comments:
Post a Comment