Ndugu wananchi,
Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yalianza rasmi mwaka 2003
baada ya Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya
Afrika kuridhia kuwepo kwa sherehe hizo. Maadhimisho haya hufanyika
katika nchi 46 za kanda ya Afrika ambazo ni wanachama wa Shirika la Afya Duniani
tarehe 31/08 ya kila mwaka.
Ndugu wananchi,
Tanzania, inaadhimisha maadhimisho haya kwa malengo makuu manne.
Kwanza
Tanzania ina nia ya kufufua ari na kujenga heshima ya huduma za tiba asili
ambazo historia inatuambia kuwa zimekuwa zikikandamizwa na kudharaulika. Kwa
kiwango kikubwa ukoloni pamoja na ukoloni mambo leo umekuwa ukikandamiza tiba
zetu za asili na kufanya Waafrika wenyewe kuzinyanyapaa tiba hizo.
Hali hiyo
imetufanya tuyumbe, tukose dira na mwelekeo katika suala zima la
kuboresha Tiba Asili katika nchi yetu.
Pili kwa kupitia maadhimisho haya Serikali inawahamasisha Waganga wa Tiba
Asili kujiepusha na migongano katika jamii kwa kutohusisha ushirikina na uchawi
kama chanzo cha ugonjwa. Kuna taarifa na migongano mingi ya kutisha juu
ya hili. Itakuwa jambo la busara kwa waganga wa tiba asili kupitia kwenye
vyama vyao kupanga mikakati ya kudhibiti na kuondoa kabisa vitendo vibaya
vinavyochafua taaluma yao.
Tatu, maadhimisho haya yanahimiza masuala ya uboreshaji na usajili wa
dawa za asili. Lengo ni kuweza kutengeneza dawa kwa kuzingatia taratibu na
miongozo ya utengenezaji dawa bora. Aidha utafiti endelevu wa dawa za
asili kwa magonjwa mbalimbali unahimizwa kwa madhumuni ya kupata dawa ambazo
zinaweza kupatikana kiurahisi ili mwenye kuhitaji aweze kuzipata.
Nne, kwa kupitia maadhimisho haya Waganga wa Tiba Asili wanahimizwa
kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma na huduma za afya.
Ndugu wananchi,
Kama mnavyofahamu katika kuadhimisha Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika
kila mwaka tunakuwa na ujumbe maalum au kauli mbiu. Ujumbe maalum wa mwaka huu
ni “Ujumuishaji wa Tiba Asili katika Mifumo ya Afya: Tulipofika sasa”
(“Integration of Traditional Medicine in Health Systems: The journey so far”).
Kauli mbiu hii inawalenga na kutoa majukumu kwa Viongozi na Wataalam wa
Tiba ya Kisasa kuweza kushirikiana na Waganga wa Tiba Asili katika utoaji wa
huduma za afya. Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inafanikiwa kuijumuisha huduma
za tiba asili katika utoaji wa huduma za afya; Serikali imerasimisha huduma za
tiba asili kwa kujumuisha katika Sera ya Afya; kuwepo kwa Sheria, Kanuni,
Miongozo na taratibu za utoaji wa huduma za tiba asili nchini.
Aidha, Waganga wa Tiba Asili wanahimizwa kusajiliwa, kusajili vituo na
dawa zao zinazotumika hususan dawa zinazouzwa katika maduka ya dawa za asili.
Hadi tarehe 30 Juni, 2017; waganga 16,200; vituo 212 na dawa za asili tatu
zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Huo ni mwanzo mzuri
ijapokuwa juhudi zaidi zinahitajika kuwezesha “Ujumuishaji wa Tiba Asili katika
Mifumo ya Afya: Tulipofika sasa”. Vilevile; nitoe wito kwa Waganga wa Tiba
Asili kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zinazowasimamia katika kutoa huduma
za tiba asili kwa wateja wao.
Nawataka wajiepushe na matangazo
yanayokizana na sheria, kanuni na taratibu ikiwa pamoja na kuondoa mabango
yaliyozagaa mitaani yanayoonyesha kuwa wanaweza kutibu na kuponya magonjwa
mbalimbali kwa mfano UKIMWI.
Ndugu wananchi,
Napenda kuwakumbusha wananchi kwamba kwa sasa huduma za tiba asili
zinatambuliwa rasmi kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Afya na Sheria namba 23 ya
mwaka 2002. Madhumuni ya sheria hii ni kusimamia, kudhibiti na kuendeleza tiba
asili ya Tanzania. Vilevile, udhibiti wa maadili ya uganga na ukunga wa tiba
asili nchini umepewa kipaumbele.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Baraza la Tiba za Asili na Tiba Mbadala
limeundwa kama chombo kikuu cha Serikali kitachosimamia na kuratibu shughuli
hizo.
Sheria hiyo pia inalinda afya na haki za watumiaji wa tiba ya asili
na tiba mbadala, kuboresha na kuendeleza tiba na dawa za asili, kuongeza
ufanisi katika utoaji wa huduma na kuondoa utoaji holela wa Tiba Asili.
Ni
muhimu kwa kila mganga wa tiba asili kuzingatia Sera, Sheria, kanuni na
taratibu zilizowekwa, kuachana na matangazo yasiyofaa, kuacha kuweka mabango
hovyohovyo barabarani, matangazo katika vyombo vya habari ni lazima yapate
kibali cha Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Ndugu wananchi,
Tanzania tunayo mitidawa mingi na mingi inayotumika kutibu magonjwa
mbalimbali.
Wataalam mbalimbali ikiwa pamoja na waganga wa tiba asili
sajilini dawa zenu ili ziweze kuwanufaisha wananchi wengi. Pia, ni ukweli
usiopingika kuwa dawa nyingi za kisasa hutengenezwa kutokana na mitidawa,
na elimu ya mwanzo kabisa juu matumizi ya miti hiyo kutumika kama dawa inatokana
na waganga wa tiba asili.
Tanzania ina rasilimali kubwa ya mitidawa na wapo
waganga wenye ujuzi katika hilo. Hivyo basi, ni vyema waganga wa tiba
asili kwa kushirikiana na Serikali kuendeleza ujuzi na utalaamu wao kwa
madhumuni ya maendeleo yao na jamii nzima kwa ujumla.
Ndugu wananchi,
Mwaka huu 2017 maadhimisho ya Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika
yanafanyika kwa kutoa elimu kwa wananchi kazi ambayo imeanza rasmi tarehe
28/08/2017 na itaendelea kutolewa hadi kilele tarehe 31/08/2017. Katika muda huo
wote mada mbalimbali zitakuwa zinatolewa ili kuwaelimisha wananchi na hususan
watoa huduma wa tiba asili na tiba mbadala kuhusu Sera, Sheria, Kanuni na
Miongozo.
Wananchi na wadau wa tiba asili nchini ni vema mkasikiliza taarifa hizo.
Ahsanteni
No comments:
Post a Comment