Tuesday, August 29, 2017

DADA POWA, KAKA POWA, MARUFUKU BAGAMOYO.



Mkuu wa Wiaya ya Bagamoyo, Alhajj, Majid Mwanga amemuagiza Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, kuwakamata wale wote wanaojishughulisha na biashara ya ngono wanawake na mashoga,  maarufu kama dada powa, na kaka powa, ili kukomesha vitendo hivyo katika Wilaya ya Bagamoyo.

Mh. Majid, aliyasema hayo wakati wa kuzindua Mpango Mkakati juu ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI wa Wiaya ya Bagamoyo uliozinduliwa jana Tarehe 28 Agosti 2017. katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Bagamoyo.

Alisema katika mitaa ya Bagamoyo wapo kina dada powa na kaka powa, ambao ni kichocheo cha maambukizi ya VVU na UKIMWI na kwamba sasa ni marufuku kuona dada powa na kaka powa katika wilaya ya Bagamoyo.

Aliongeza kwa kumtaka Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, kufanya doria katika mitaa ya Bagamoyo ambayo inafahamika kwa biashara ya ngono na kuwakamata wale wote wanaohusika lengo likiwa ni kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI lakini pia ni kurudisha utamaduni wa Bagamoyo ambao ni kuwa na maadili mema na sio kujiuza.

Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Wilaya ya Bagamoyo, alimtaka Mkuu wa Polisi pia kuwakamata wale wanaouza pombe hovyo, wauzaji wa dawa za kulevya na Bangi kwakuwa hivyo vyote ni visababishi vya maambukizi ya VVU na UKIMWI. katika wilaya ya Bagamoyo.

Aidha, Mkuu wa Wilaya pia alimuagiza mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo kuwakamata  wacheza ngoma wakiwa nusu uchi katika mitaa ya Bagamoyo kwani ni vitendo vinavyokiuka maadili ya Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla.

''Wapo wanaocheza ngoma wakiwa uchi na wengine wakipita kwenye magari na kutoa viuno nje na wengine kwa miguu, hawa OCD. washughulikie'' Alisema Mkuu wa wilaya Majid.

 Awali akiwasilisha mada mbele ya Mgeni Rasmi, Mratibu wa Huduma za Ushauri na Upimaji wa VVU Wilaya ya Bagamoyo, Mmanyi Philipo, alisema Tanzania katika kupunguza maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI Kitaifa kutoka asilimia 7% Mwaka 2003-2004 hadi Asilimia 5.1% Mwaka 2011 – 2012:

Aidha, Wilaya  ya Bagamoyo, Kiwango cha Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI ni Asilimia 5.9% ambacho ni kikubwa zaidi kuliko kiwango cha Maambukizi ya VVU Kitaifa ambacho ni Asilimia (5.1%).
 Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP. Adam maro.


No comments:

Post a Comment