Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, kushoto akiangalia jengo la wodi ya wazazi linalojengwa na Taasisi ya Kiislamu ya DHI NUREYN ya Iringa, kulia ni Mhandisi wa majengo wa DHI NUREYN, Ally Upete.
......................
Taasisi ya kiislamu ya Dhi Nureyn yenye makao
yake makuu mjini Iringa inajenga majengo mawaili katika Hospitali ya Bagamoyo,
yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia 494.
Majengo hayo ni wodi ya wazazi itakayokuwa na
uwezo wa kuwekwa vitanda 30 pamoja na jengo la wagonjwa wa dharula hali
kupunguza msongamano katika katika wodi ya wazazi.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo
ametembelea katika Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo ili kujionea majengo hayo na
kusema kuwa Taasisi hiyo imefanya kitu chenye thamani kubwa kwa serikali na
kwamba Serikali inathamini Mchango huo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema anatoa shukrani za
dhati kwa Taasisi ya Dhi nureyn kwa msaada huo ambao utasaidia kuondoa
msongamano kwa wazazi wanaofika kujifungua hospitalini hapo.
Aliwataka watumishi katika Hospitali ya wilaya ya
Bagamoyo pindi majengo hayo yatakapokamilika kutoa huduma bora zitakazolingana
na ubora wa majengo hayo ili kuondoa malalamiko kwa wananchi wa Bagamoyo.
Aidha, aliwataka watumishi wote katika Hospitali
hiyo kuyatumia vizuri majengo hayo na kuyatunza ili iwe kielelezo kwa vizazi na
iwe hamasa kwa wafadhili waliojenga waweze kuvutiwa kutoa msaada mwingine
zaidi.
Alitumia fursa hiyo pia kumpongeza Mkuu wa Wilaya
ya Bagamoyo, Alhajj, Majid Mwanga, kwa kuwatafuta wafadhili hao na kufanikisha
ujenzi mkubwa ndani ya wilaya yake na kwamba itabaki kuwa alama ya milele
atakayoiacha katika wilaya hiyo.
Akisoma Taarifa fupi mbele ya mkuu wa Mkoa,
Mganga mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Dkt. Silvia Mamkwe, alisema ujenzi huo ni
msaada mkubwa kwa Hospitali ya wilaya Bagamoyo, ambapo kukamilika kwake
kutaondoa adha ya msongamano kwenye wodi ya wazazi.
Alisema ujenzi huo unaoendelea hivi sasa ni jengo
la wodi ya wazazi litakalogharimu shilingi milioni mia tatu kumi na sita laki
nane kumi na tisa mia saba na kumi, 316,819,710. Na Jengo la wagonjwa wa
dharula litagharimu milioni mia moja sabini na nane laki nne themanini na tisa mia tisa sabini na saba 178,489,977
.
Aidha, alisema uongozi wa hospitali na ya Wilaya
pamoja na watumishi wote wanaendelea kuwapa ushirikiano wafadhili hao (DHI
NUREYN) ili waweze kufanikisha ujenzi huo kama walivyopanga.
Dkt. Mamkwe alisema kukamilika kwa ujenzi huo
kutaisaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa matibabu haswa kwa wagonjwa wa
dharula na wodi wazazi.
Alisema kuwa jengo la wodi ya wazazi
litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kulaza kina mama 30, ambapo kila mama
atalala kwenye chumba chake, pamoja na chumba cha kujifungulia kina mama
kitakachokuwa na vitanda vya kujifungulia vinane wakati kwa kwa sasa kuna
vitanda vitatu tu vya kujifungulia.
Aliongeza kwa kusema kuwa, jengo la dharula lina
umuhimu mkubwa kwa sasa katika mji wa Bagamoyo, hasa ikizingatiwa kuwa, kuna
ongezeko la watu kutokana na ujenzi wa viwanda, na kukamilika kwa barabara ya
Bagamoyo Msata hali inayopelekea kuwa na majeruhi wengi wanaotokana na ajali za
Barabarani.
Alisema Jengo hilo la huduma za dharula litakuwa
na vitanda sita na ofisi za watoa huduma ili kukabiliana na majanga ya ajali mbalimbali
yanayotokea mara kwa mara.
Aidh, alisema Taasisi ya Dhi Nureyn imeahidi
kuweka vifaa tiba katika yake hayo inayojenga na kukabidhi tayari kwaajili ya
matumizi tu.
Akielezea historia ya Hospitali hiyo ya wilaya ya
Bagamoyo, alisema Hospitali hiyo ilianzishwa na Mfanyabiashara Sewahaji mwaka
1895 ambapo mwaka 1961 ilimilikwa rasmi na Serikali na kwamba mpaka sasa
Hospitali hiyo ina uwezo wa kulaza wagonjwa
100 kwa siku katika wodi sita zilizopo.
Mganga huyo wa Wilaya ya Bagamoyo, alisema pamoja
na ujenzi huo unaodhaminiwa na Taasisi ya Dhi nureyn, bado Hospitali hiyo inakabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa majengo, mifumo mibovu ya maji
taka na safi pamoja na miundombinu ya umeme.
Taasisi ya Dhi Nuryn imefanikisha uchimbaji
kisima katika Hospitali ya Bagamoyo ili kuondoa tatizo la maji katika Hospitali
lakini pia imeweza kuchimba visima katika makazi ya watu kwenye mitaa iliyokuwa
na tatizo la maji na hivyo kufanya jumla ya idadi ya visima vilivyochimbwa na
Taasisi ya Dhi Nureyn mjini Bagamoyo kufika kumi mpaka sasa.
Mganga mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Dkt. Silvia Mamkwe,kulia akisoma Taarifa fupi kuhusu majengo ya wodi ya wazazi na jengo la wagonjwa wa dharula, mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani, mbeleya yake kutoka kushoto ni mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, wa pili ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid mwanga, watatu ni mkuu wa mkoa wa pwani, Mhandishi Evaristi Ndikilo, wa nne ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Almasi Masukuzi na watano ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Omari Latu.
No comments:
Post a Comment