Friday, May 31, 2024

DED BAGAMOYO AFUNGUA MAFUNZO KUHUSU MABORESHO YA MITAALA YA ELIMU YA AWALI, MSINGI, SEKONDARI NA UALIMU KATIKA SHULE YA SEKONDARI BAGAMOYO MKOANI PWANI.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Bw Shauri Selenda tarehe 30 Mei 2024 amefungua mafunzo kuhusu maboresho ya mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo Mkoani Pwani.


Mafunzo hayo, yamelenga kuwapitisha washiriki katika muundo wa Elimu, Maboresho Elimu Msingi na Sekondari pamoja na Ualimu.


" Ndugu zangu nyinyi mliopo hapa ni asilimia ndogo sana ya washiriki wanaohitajika kupata mafunzo haya, hivyo nawaomba muwe makini kutumia muda Ili muweze kupata Yale yaliyotarajiwa kutoka kwa wawezeshaji wetu ". Alisema Bw Selenda.


Mafunzo haya ya siku mbili yanajumuisha Walimu Wakuu 78 toka Shule za Msingi za Serikali na binafsi Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Ofisi ya Raisi- TAMISEMI






Thursday, May 30, 2024

WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO 2024

SOMA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO NA VYUO VYA KATI KWA MWAKA 2024.

UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO NA VYUO VYA KATI, 2024



CHAGUA MKOA ULIKOSOMA


MKOA WA KAGERA KUANZISHA MASHAMBA YA KAHAWA ZAIDI YA HEKTA 4,000

 

Na Alodia Dominick,

Bukoba.

Mkoa wa Kagera unatarajia kuanzisha mashamba ya pamoja ya kahawa zaidi ya hekta 4,000 lengo likiwa ni kuondoa umaskini kwa wananchi wa mkoa huo.


Hayo yamebainika katika mkutano wa wadau wa kahawa uliofanyika Mei 29, mwaka huu katika ukumbi wa mkuu wa mkoa huo.


Akifungua mkutano huo mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa, amesema kuwa, kuanzishwa kwa mashamba ya pamoja ya  kahawa ni agizo la Wizara ya kilimo ililolitoa hivi karibuni kwa bodi ya kahawa Tanzania (TCB) kuhakikisha inatoa matrekta na Wizara itatoa miche ya mibuni zaidi ya milioni 5.


"Dhamira ya serikali ni kupanua kilimo cha kahawa, sote tunayo kumbukumbu kahawa ilivyokosa bei wakulima wengi walikata miche ya kahawa hivyo mashamba mengi yana miche michache ya kahawa na tunao uwezo wa kuzalisha mara mbili ya kahawa  tuliyo nayo katika mkoa wetu wa Kagera"


"Tukifanya hivyo hata ile ya kutajwa tajwa eti sisi ni wa pili kutoka mwisho kwa umaskini itaisha tutakuwa tunashikilia namba 10 bora za uchumi Tanzania, sisi kama mkoa tukishirikiana na wizara ya kilimo tumeamua kufungua mashamba ya pamoja ya kahawa kwa mwaka huu tunaenda kuanzisha hekta 4,000 wilaya za Karagwe na Muleba ili kufikia mwaka 2030 mkoa wa Kagera umaskini usiwepo tena" amesema Mwassa.


Aidha amesema kuwa, baada ya kuanzishwa kwa mashamba hayo watakuwa wanakata hekali mbili wanagawia wakulima na wale watakaohitaji hekali zaidi watapatiwa.


Katibu Tawala mkoa wa Kagera (RAS) Steven Ndaki amesema kuwa, mkoa wa Kagera ndiyo mkoa wa kwanza Tanzania kwa uzalishaji wa zao la kahawa kwa mwaka huzalisha tani 60,000 hadi tani 80,000 ingawa uzalishaji huo unakumbwa na changamoto mbalimbali.


Changamoto hizo ni pamoja na utoroshaji wa kahawa ambapo baadhi ya wananchi wanalazimika kuivuna kahawa kabla ya wakati na kusababisha ubora wa kahawa kushuka.


Ametaja  lengo la kikao hicho kuwa ni kujadili fursa, mafanikio na changamoto na mwisho watoke na mkakati utakaowezesha kudhibiti ubora, kuongeza tija na kuimarisha mfumo wa masoko wa zao hilo.


Baada ya wadau wa kahawa kujadili kwa undani wametoka na maazimio ambayo ni kila halmashauri kuweka mikakati ya kuzuia biashara ya magendo ya kahawa bila kutumia nguvu ili kulinda mapato ya wakulima pamoja na serikali, halmashauri za Karagwe na Muleba zitenge maeneo kwa ajili ya kilimo cha kahawa.


Maazimio mengine ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya uvunaji wa kahawa mbichi na utoroshaji wa kahawa, msimu wa ununuzi wa kahawa ufunguliwe mapema mwezi Aprili ili kuwezesha ununuzi wa kahawa aina ya arabica na kuzuia magendo, kuongeza tija na ubora wa kahawa.


Amcos ziwezeshwe kuweka mikakati ya kuwakopesha wakulima mapema kabla ya kuvuna ili kudhibiti biashara ya kahawa changa ikiwa bado shambani (obutura), mikutano ya wadau wa kahawa ngazi ya mkoa ihuishwe na wajumbe wote kutoka maeneo ya uzalishaji washirikishwe.


Serikali iwekeze kikamilifu kwenye mialo,  beria na mikapani kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti utoroshaji wa kahawa.


MWENGE WA UHURU WAZINDUA KLABU YA WAPINGA RUSHWA NA DAWA ZA KULEVYA  GREAT MINDS SCHOOL 

 

NA HADIJA OMARY, LINDI

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 Godfrey mnzava amezindua klabu ya Wapinga Rushwa na Dawa za kulevya ya shule ya Great minds primary school iliyopo Halmashauri ya manispaa ya Lindi Mkoani Lindi .


Uzinduzi huo ulioenda sambamba kwa Shule hiyo kukabidhiwa  cheti cha ufunguzi,  uzinduzi rasm wa klabu hiyo ulifanyika jana   katika viwanja vya shule ya msingi Mnazi Mmoja Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambako mkesha wa mwenge huo wa uhuru ulifanyika.


Akizungumza na wanafunzi, walimu , viongozi alioambapatana nao pamoja na wananchi waliojitokeza katika viwanja hivyo Mnzava  aliwataka wanafunzi na wana klabu hiyo kuendelea kujifunza vizuri maswala hayo ya Rushwa na mapambano dhidi ya Dawa za kulevya ili wawe mabalozi wazuri kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.


Awali akisoma risala kwa kiongozi huyo, Anjela Lukanga mwanafunzi wa shule ya Great minds, amesema klabu hiyo ina jumla ya wananchama 33 ambapo kati yao wasichana 12 na wavulana 21na inalengo la kuwajenga kimaadili pamoja na kushirikishwa kwenye mapambano dhidi ya Rushwa na Dawa za kulevya.


" Tunashukuru kwa kutuwezesha kutambua nafasi na wajibu wetu kwa kushiriki kuzuia na kupambana  na Dawa za kulevya  hapa Nchini sambamba na kutujengea uwelewa juu ya madhara na kuchukia Rushwa na dawa za kulevya katika maisha yetu hali tungali bado mashuleni.


Kwa upande wake salome mbonile kutoka ofisi ya mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya amesema ili kuhakikisha Elimu ya kuendeleza mapambano dhidi ya Dawa za kulevya inawafikia watu wengi  mamlaka hiyo imeanza kushirikiana na taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU kwa kuziongezea majukumu klabu za kupinga Rushwa zijifunze na kuzungumzia maswala hayo ya Dawa za kulevya.


" katika Mkoa wa Lindi tayari kama mamlaka tumesha ziongezea majukumu hayo shule  zipatazo 22 za Sekondari , 86 za msingi na vyuo klabu mbili " alisema Bi.Salome.


Ujumbe wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 kuhusu Dawa za kulevya ni " Epuka matumizi ya Dawa za kulevya zingatia utu. Boresha huduma za kinga na tiba









Wednesday, May 29, 2024

TAWI LA UDSM KUJENGWA KAGERA.

 

Na Alodia Babara,

Bukoba

Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa ametaja manufaa manne yatakayopatikana baada ya kukamilika ujenzi wa tawi la chuo kikuu cha Dar es Salaam ikiwemo kupanua mji, kukuza uchumi, kuongeza fursa kwa vijana wa Kagera na kuongeza urafiki.


Tawi hilo la chuo kikuu litajengwa katika kijiji cha Itahwa kata ya Kalabagaine halmashauri ya Bukoba na eneo la chuo hicho ni hekali 315 ambazo zilitolewa na wananchi wa vijiji viwili vya Kangabusharo na Itahwa na hafla  ya kukabidhi eneo la ujenzi kwa mkandarasi imefanyika Mei 29,mwaka huu.


Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika katika eneo litakapojengwa tawi la chuo kikuu cha Dar es Salaam amewashukuru  wananchi kwa kutoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na kutoa manufaa manne yatakayopatikana baada ya kukamilika kwake.


"Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutukumbuka wanakagera kutuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu, wanakagera walitamani kuwa na chuo kikuu miaka mingi iliyopita kwani wanahistoria ya kupenda kusoma" amesema Mwassa


Ameongeza kuwa, wanatambua chuo hicho ni kwa ajili ya watanzania wote na raia wa nchi nyingine lakini watatumia fursa hiyo vizuri.


Amesema kuwa, uwepo wa mradi huo utaleta fursa mbalimbali kwa wakazi wa mkoa wa Kagera ikiwemo fursa ya elimu kwa wakazi wa Kagera kwani kitakuwepo kituo cha mafunzo ya ujasiriamali hata kama mtu hajamaliza kidato cha sita, kupanua mji, kukuza uchumi, na kuongeza urafiki.


Aidha ametoa rai kwa wanafunzi wanaosoma shule za sekondari zinazozunguka eneo la chuo kikuu kuongeza bidii katika masomo ili watakapohitimu kidato cha sita waweze kuendelea na masomo ya juu katika chuo hicho.


Pia amemtaka mkandarasi wa ujenzi katika chuo hicho kumaliza kwa wakati ujenzi huo.

Kwa upande wake Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia taaluma Prof. Beneventura Rutinwa amesema mpango wa ujenzi wa tawi la chuo hicho ulianza mwaka 2019 na kwa kipindi cha kwanza cha ujenzi zitatumika shilingi bilioni 20.

Amesema ujenzi ulianza Mei 17,2024 utakamilika Octoba mwaka kesho utachukua muda wa miezi 18.

Aidha mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima amesema, wilaya ipo tayari kutoa ushirikiano kipindi chote cha utekelezaji wa ujenzi huo.


KLABU ZA WAPINGA RUSHWA MASHULENI ZINASAIDIA KUENDELEZA  MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

 

Na Hadija Omary, Lindi.


Imeelezwa kuwa Kuanzishwa kwa klabu za wapinga rushwa mashuleni ni chachu ya kuimarisha na kuhamasisha wanafunzi kupenda kushiriki kwenye vitendo vya kuzuia, kupinga na kupambana na rushwa katika jamii.


Hayo yameelezwa na  Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024,  Godfrey  Mnzava alipotembelea Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Sekondari Hawa Mchopa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mkoani Lindi. Kwa lengo la kuimarisha klabu hiyo.


Mnzava  amesema kuwa kwa kuzingatia kauli mbiu ya KUZUIA RUSHWA NIJUKUMU LAKO NA LANGU, TUTIMIZE WAJIBU WETU,  jamii inapaswa kuendelea kutoa msisitizo na kuwekeza zaidi katika kuelimisha wanafunzi ambao ndio viongozi wa kesho ili waweze kujua madhara ya Rushwa kwa jamii.


"Tuweke nguvu zaidi katika kuunda klabu za wapinga rushwa mashuleni na vyuoni ili kuwaandaa hawa viongozi wetu wa kesho kujua madhara ya rushwa na kuichukua rushwa ili tuweze kujenga taifa la watu wanaoichukia rushwa na kutoa haki vile inavyopaswa" ameeleza.


Awali akitoa taarifa ya Klabu ya Kuzuia na Kupinga Rushwa, Katibu wa Klabu hiyo Noshard Christopher ameeleza kuwa kupitia Klabu hiyo wanafunzi wamepata fursa ya kutambua madhara na viashiria vya rushwa pamoja na kuelimisha wanajamii kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia nyimbo, ngonjera, uchoraji wa katuni na uandishi wa insha.


"Tuna imani kwamba uwepo wa vilabu vya kupinga Rushwa mashuleni na vyuoni vinasaidia jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Rushwa na hivyo kujenga Tanzania imara isiyokuwa na Rushwa.


Vilevile, tunawahamasisha wananchi kufichua na kukemea vitendo vya Rushwa katika maeneo yao kwa kutoa taarifa ofisi ya TAKUKURU kwa njia ya simu namba ya  bure 113" ameongeza Noshard.


Amesema klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Hawa Mchopa ilianzishwa miaka 7 na hadi sasa jumla ya wanachama hai 122, kati yao wavulana ni 71 na wasichana 51.




SERIKALI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI.

 

Wizara ya Ujenzi imeanza utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi kwa utaratibu wa ubia (PPP)katika kutekeleza miradi ya miundombinu.


Haya yamebainishwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati wa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25, Bungeni jijini Dodoma leo, Mei 29, 2024


Amesema ni katika kuipunguzia Serikali gharama kubwa za utekelezaji wa miradi ya miundombinu hasa barabara na madaraja ambayo Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha.


“Lengo la kutumia utaratibu huu ni kujenga miundombinu na kuitekeleza kwa wakati.”


Aliitaja iradi inayotekelezwa kwa utaratibu huo kuwa ujenzi wa barabara ya Kibaha-Chalinze-Morogoro-Dodoma (Expressway) yenye urefu wa kilometa 423.8 kwa mfumo wa kulipia.


Tuesday, May 28, 2024

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA 2024 AWAPA HEKO MTAMA KWA KUANZISHA KITUO CHA REDIO

 

Na HADIJA OMARY, LINDI


kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 Godfrey Mnzava ameipongeza halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi kwa uibuaji wa mradi wa  kituo cha kurusha matangazo cha Redio Mtama.


Mradi huo wa ujenzi wa studio za redio jamii Mtama FM(106.3) uliibuliwa mwaka 2023 chini ya ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliopo chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.



Akizungumza na wananchi mara baada ya mwenge wa uhuru kutembelea katika Redio hiyo iliyopo katika Mtaa wa majengo katika halmashauri hiyo  kiongozi huyo amesema mradi huo ni mzuri na kwamba utawezesha halmashauri kufikisha Taarifa kwa wananchi kwa uharaka.



Hata hivyo Mnzava ameitaka  jamii kutumia kituo hicho ili kiweze kuleta tija kwao na kutoa wito kwa uongozi wa halmashauri kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kwa hatua zilizobaki ili kiweze kuanza kutumika kwa wakati.


Aidha Mnzava ametumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa vyombo vya habari na kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 ambayo inasisitiza juu ya Umuhimu wa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Utunzaji wa Mazingira.


Akitoa taarifa kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge Mhandisi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF ) Mhandisi Baraka Elieza amesema mradi huo  unatekelezwa na makandarasi ElsewedyElectric East Africa Ltd P.O BOX 9213 DSM ukiwa na gharama kiasi cha Tsh. Milioni 972 huku gharama zote zikilipwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote yaani UCSAF.



Mhandisi Elieza ametaja wanufaika wa mradi huo kuwa ni wananchi wote kutokana na redio hiyo kusikika kwenye kata zote 20 za Halmashauri ya Mtama, kutumia redio katika kuelimisha jamii kupitia vipindi mbalimbali, kutumia redio kama chanzo cha mapato ya halmashauri kutokana na kurusha matangazo ya wateja mbalimbali.





UPOTOSHAJI WA VIVUKO KIGAMBONI UNA MASLAHI BINAFSI: WAZIRI BASHUNGWA

 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewatoa hofu Wananchi wa mkoa wa Dar es salaam wanaotumia usafiri wa vivuko eneo la Kigamboni -Magogoni juu ya taharuki kuhusu huduma inayotolewa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) nakueleza kuwa imetengenezwa na watu wenye maslahi binafsi.


Ameyasema hayo leo Mei 28, 2024 wakati alipokuwa akifanya mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha huduma ya usafiri wa vivuko nchini.


"Niwatoe wasiwasi Wananchi wa Dar es salaam pamoja na kigamboni, taharuki ambayo imetengenezwa hakukuwa na sababu ya kutengenezwa. Lakini sisi tunaofahamu yapo maslahi binafsi nyuma ya utengenezaji wa hii taharuki" Amekaririwa Bashungwa


Ameeleza kuwa sasa vivuko vingi vinaendelea na matengenezo, lakini pia Mkandarasi Songoro Marine anaendelea na ujenzi wa vivuko vipya katika karakana yake mkoani Mwanza kwa ajili yakupelekwa kwenye maeneo mbalimbali kutoa huduma kwa wananchi.


Aidha, Bashungwa amesema kuwa tayari ameikutanisha TEMESA na Kampuni ya AZAM Marine na kujadili namna bora yakushirikiana kwa pamoja kuboresha utoaji huduma ya usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni - Kigamboni.


"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaboresha vivuko na tutaweka machaguo kwa abiria ambapo watakuwa na chaguo. Ukitaka kutumia kivuko cha TEMESA sawa au ukitaka cha AZAM muda mchache kuvuka kwasababu zile ni ndogo siyo kama kivuko kikubwa ambacho unasubiri kupakia magari na abiria ili muweze kuondoka pamoja" Amesisitiza.


Bashungwa amesema Wizara inatambua changamoto ya wananchi ni huduma bora ya vivuko nakusema kuwa kuanzia mwezi Agosti mwaka huu wataanza kutekeleza mpango huo utakaotoa wigo kwa wananchi kuchagua huduma wanayotaka kutumia.


"Wapo wanaotaka kushinikiza ili utaratibu na mwelekeo uende kama wanavyotaka wao, sisi hatuendi hivyo"amesema Bashungwa huku akisema kuwataja watu hao ni kuwapa sifa.


ZAIDI YA WANANCHI 6,000 KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI MTAMA

 


Na Hadija Omary, Lindi

Zaidi ya  watu  6,000 wa vijiji vya Chiuta, Mikongi na maeneo ya jirani katika halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi wameanza kunufaika na upatikanaji wa huduma ya uhakika ya maji safi na salama.


Hiyo ni baada ya kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa kwa mwaka 2024 Godfrey Mzava kuweka jiwe la msingi katika mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya maji Chiuta -Mikongi, Mei 27,2024.


Mradi huo unaogharimu Kiasi  cha zaidi ya Milioni 452 umeboreshwa kwa lengo la kukidhi mahitaji halisi ya wananchi wa vijiji vya Chiuta na Mikongi ambapo  hapo awali  ulikuwa unatoa huduma ya maji chini ya asilimia 30 ya mahitaji halisi kwa jamii ya Kijiji cha Chiuta Pekee.


Akitoa taarifa ya mradi mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa, Mhandisi wa mradi huo Olaph John  amesema mradi huo unatekelezwa na Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Masasi kwa kushirikiana na Shirika la World Vision kwa usimamizi wa Serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) ambapo kwa uboreshaji huo unakwenda kutoa uhakika wa upatikanaji wa maji kwa wananchi Kwani utazalisha maji takribani lita 168,000 kwa siku badala ya Lita 7,490 zilizokuwa zinazalishwa hapo awali.


Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za mwenge Kitaifa kwa mwaka 2024 Mnzava amelishukuru Kanisa la Anglikan kwa namna linavyoiunga Mkono Serikali katika kuwahudumia wananchi akiwataka pia  kumaliza shughuli zilizosalia katika mradi huo huku wananchi wa Chiuta wakiahidi kutunza miundombinu yake.


Mradi  wa uboreshaji wa maji Chiuta -Mikongi utatumia mfumo wa malipo ya kabla (Pre -Paid Meters)kwenye vituo vyake vyote vya kuchotea maji.


BARABARA YA NYENGEDI-RONDO KUJENGEWA KWA KIWANGO CHA LAMI.

 

Na Hadija Omary, Lindi

Hatua ya Serikali kupitia wakala wa Barabara za vijijini na mijini (TARURA) kuanza kujenga Mradi wa barabara ya Nyengedi-Mnara -Rondo yenye urefu wa km 1.15 kwa gharama ya Shilingi milioni 939,107,800.00 kwa kiwango cha lami kumeleta faraja  kwa wananchi wa vijiji hivyo.


Ujenzi wa Barabara hiyo umewekwa jiwe la msingi na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mzava mei 27, 2024 ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwa halmashauri ya Mtama na hivyo kupunguza gharama za matengenezo ya kila mwaka.


Kabla ya kuweka jiwe la msingi kiongozi huyo wa Mwenge wa uhuru Kitaifa,  ameeleza matumaini yake juu ya mradi huo kuwa utakamilika kwa wakati uliopangwa mwezi Oktoba Kama mkataba unavyoelekeza huku akiwahimiza Wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) kusimamia vizuri ili wanachi wapate unafuu wa huduma ambazo zitategemea barabara hiyo.


Akitoa taarifa ya mradi huo Meneja wa  (TARURA)Wilaya ya Lindi Mhandisi Dawson Paschal amesema mradi  unatekelezwa na Mkandarasi M/s.M.E & Company Limited ukiwa kwa sasa umefikia asilimia 15 ya utekelezaji na  unakwenda kukamilisha urefu wa km 7.1 ambazo zinajengwa kwa sehemu tofauti zilizokuwa korofi zaidi.


Wakazi hao wamesema barabara hiyo itakapokamikika itawasaidia kuunganisha mawasiliano kati ya wananchi wa Nyengedi na Rondo na pia kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo hususan mazao.


“Kabla ya hapo adha ilikuwa kuwa hasa kwenye kusafirisha mazao yetu kutoka mashambani lakini wajawazito walikuwa walikuwa wanateseka kufika kituo cha afya kwa sababu barabara ilikuwa korofi sana na wa mama wengine walikuwa wanajigungulia njiani “Alisema Ramadhan Selemani Nchia    Mkazi wa Kijiji cha Mkangambili -Rondo.


Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024 ukiwa katika halmashauri ya Mtama umekimbizwa kwa umbali wa Km 204.2 ukipita katika miradi 8 ya maendeleo yenye thamani ya Bilion 2.526.





Monday, May 27, 2024

LUGANGIRA KUANZISHA MABINT CUP KAGERA.

 

Mbunge viti maalum (CCM) mkoa wa Kagera Neema Lugangira akizumgumza na waandishi wa habari hawako pichani

.........................

Na Alodia Babara,  Bukoba

Mbunge viti maalum (CCM) mkoani Kagera Neema Lugangira ameanza maandalizi ya ligi ya mpira wa miguu  maarufu kama Mabintcup itakayowahusisha watoto wa kike na wanawake.


Maandalizi ya ligi hiyo tayari yameanza kwa kuunda kamati tendaji ambayo wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Katibu wa chama cha soka mkoa wa Kagera Alhaji Amir, mkurugenzi wa Bukoba tour Wiliam Ruta, mwenyekiti wa chama cha soka wanawake mkoa wa Kagera Dkt Leonia Kaijage, mtu wa habari za mitandaoni na yeye mbunge Lugangira akiwa ni mwenyekiti wa kamati hiyo ambayo itashirikiana na watu wengine.

                   

Neema Lugangira mbunge viti maalum mkoani Kagera jana akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba ambao wamejiunga pamoja kwa hiyari yao kuunga mkono agenda ya Mabinti Cup ametaja malengo ya kuanzisha ligi hiyo kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhamasisha usawa wa kijinsia.


Malengo mengine ni pamoja na kutumia michezo kama nyenzo ya kuchagiza maendeleo kwa kuimarisha demokrasia na maendeleo, fursa za kiuchumi, afya ya uzazi kwa wanawake, vijana wa kike na kiume.


Rugangira amesema Mabinti Cup anaianzisha kama yeye kwa kushirikiana na chama cha soka mkoa wa Kagera KRFA si kwa matakwa ya kisiasa bali kwa mapenzi aliyonayo katika soka.


“Baada ya kutafuta timu zitakazoshiriki kwenye ligi kadiri mechi zitakavyokuwa zinaendelea vitaibuliwa vipaji na kuvitambua ili vikuzwe, kwenye kuibua na kukuza vipaji hapo tutajitahidi kutafuta timu kubwa za wanawake ili mashindano yawe ni kama  kiwanda cha kuzalisha vipaji” amesema Lugangira.


Ameongeza kuwa, viwanja vitakavyotumika kwenye michezo vitafanywa kama kambi  ya elimu ili kupitia michezo yahamasishwe maendeleo.


“Kama mechi inaanza saa 10:00 masaa mawili kabla yatatumika kutoa elimu juu ya maswala mbalimbali ambayo ndiyo malengo yetu na kaulimbiu ya Mabinti Cup ni piga kete ukatili wa kijinsia” amesema Lugangira.


Ligi hiyo inatarajia kuanza Novemba mwaka huu wachezaji ni vijana kuanzia miaka 18 hadi 25 timu zitakazoshiriki ni 16 huku timu 14 zikiwa za manispaa ya Bukoba, timu moja kutoka wilaya ya Misenyi na nyingine moja kutoka Bukoba Vijijini ambazo zitacheza kwa njia ya mtoano.


Aidha Lugangira amesema kuanzia mwezi June hadi Julai watasajili timu na kupata viongozi, Agosti zitatolewa semina kwa wachezaji na viongozi na kuanzia Septemba hadi Oktoba ni mazoezi kwa timu zitakazokuwa zimepatikana.


Amesema ligi hiyo itakuwa ni mwendelezo kutoka ngazi ya wilaya, mkoa, kikanda hadi Taifa.


Faisal Hamed ni mwandishi wa habari kutoka kituo cha Eatv amemshauri mbunge huyo kuwa, watakapokuwa wanatafutwa wachezaji wa kushiriki katika ligi hiyo kamati ipite na kwenye vituo vya watoto yatima kwani huko wanaweza kupatikana wachezaji bora.


Ameeleza kuwa, kutokana na kwamba wakati ligi inaendelea wanahitaji kuibua vipaji vya mabinti basi kamati ipite kwenye vituo hivyo ili kuweza kuibua vipaji kwani michezo hiyo inaweza kuwa faraja kwa mabinti wanaolelewa katika vituo vya watoto yatima.


Diana Deus mwandishi wa habari gazeti la Habari Leo amemshukuru mbunge kwa wazo la kuanzisha ligi hiyo na kusema kuwa ligi hiyo itasaidia kuibua vipaji kwa vijana wa kike na ili kuweza kutimiza kauli mbiu ya ligi hiyo na waandishi wa habari kuandika kwa undani zaidi habari za unyanyasaji wa kijinsia akaomba mafunzo kwa waandishi hao.


Sunday, May 26, 2024

MILIONI 866 KUJENGA BARABARA KM 1.2 KWA KIWANGO CHA LAMI LIWALE

 

NA  HADIJA OMARY 

LINDI.

Wananchi wa Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi wanaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,  kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 866,659,200.40 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilometa 1.2  kwa kiwango cha lami katika Halmashauri hiyo.


Wametoa shukurani hizo mara baada ya mwenge wa uhuru kufika Wilayani humo na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi huo wa mradi wa barabara ambao unatajwa utarahisisha usafirishaji wa mazao.


Hamisi Rashidi, Dereva Boda boda amesema kipindi cha masika Barabara hiyo ilikuwa ikijaa maji mara kwa mara hali iliyopelekea kutopitika kwa urahisi kipindi hicho cha masika hivyo ujenzi wa barabara hiyo unaenda kumaliza kero hiyo.


Kwa mujibu wa Meneja wa wakala wa Barabara za mijini na vijijini TARURA Wilayani Liwale, Mhandisi. Living Stone Shija, amesema mradi huo wa barabara ya Murua-Mkurunguche- Ngojwike - Mandepe petrol station  unatekelezwa na mkandarasi M/S TECHINO COMBINE CONSTRUCTION  LIMITED.


Amesema mradi huo ulianza matengenezo yake tarehe 15/09/2023 na unatarajiwa kukamilika tarehe 15/07/2024 ambapo mpaka sasa tayari kazi mbalimbali zimeshafanyika.


Kwa upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Godlack Mlinga amesema Mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo ya Liwale katika kuyafikia maeneo tofauti, kupendezesha mandhari ya mji pamoja na kupunguza adha ya matengenezo ya mara kwa mara.


" niishukuru serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya Barabara hasa hizi za kati kati ya mji katika Wilaya yetu ambazo kwanza zinaenda kubadilisha muonekano wa mji wetu lakini pia kupitia bunge la bajeti serikali imeidhinisha fedha kwa ajiri ya ujenzi wa barabara ya Liwale-Nachingwea-Masasi na sasa tunasubiria kuanza utekelezaji wake"


Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Mradi huo kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mzava  amesisitiza kuendelea kutumia mfumo wa manunuzi wa kimtandao wa Serikali wa nest.


Baada ya kukagua barabara na kukagua nyaraka zinazoonyesha uhalali wa matumizi ya fedha pamoja na utaratibu ambao umetumika katika utekelezaji wa mradi huu mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 umeridhia kuweka jiwe la msingi katika mradi huu.








WAKAZI WA MASAKI KISARAWE  WALILIA BARABARA

Na Omary Mngindo, Kisarawe

WAKAZI wa Vijiji vinavyounda Kata ya Masaki Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, wameiomba Serikali kuandaa utaratibu wa Daladala nyingine zipitie barabara ya Kisanga kutokea Masaki.


Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi kijijini Masaki wakazi Fatuma Swaiba, Juma Idd na Ramadhani Seif walisema kuwa kwa sasa usafiri unaotokea Chanika bodaboda nauli ni shilingi elfu tano.


"Nauli yake kutoka Chanika mpaka kuanzia Kijiji cha Kisanga ni shilingi elfu 5,000 na kuendelea kutokana na umbali, lakini kuna umbali wa dakika 30 lakini upande wa barabara iko vizuri ukiachilia baadhi ya changamoto za maeneo machache," alisema Fatuma.


Aliongeza kuwa kwa kutumia mabasi yanayotokea stendi ya mabasi ya Pugu kuelekea Kisarawe mjini na vijiji mbalimbali wanatozwa shilingi elfu 4,000,  hivyo wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupatikana kwa usafiri.


"Kuna abiria wengine wanatokea maeneo ya Mkuranga na vitongoji vyake ambao kwanza wanafika pale Chanika, kisha wanapanda bodaboda kuelekea vijiji na vitongoji mpaka Masaki na kuendelea vijiji vingine," alisema mkazi huyo.


Seif alisema kuwa kwa kutumia pikipiki wanazozipanda kutokea Chanika kupitia Kisanga kutokea Masaki ni mwendo wa dakika 25 mpaka 27, huku wakilipa shilingi 5,000 kwa mtu mmoja wakiwa wawili wanatozwa shilingi 6,000.


"Hii barabara ni fupi sana, itakuwa ni vema wakapitisha daladala ili kuwahakikishia kuwa na usafiri wenye uhakika tofauti na bodaboda, kwa sasa tunawashukuru kwa kazi waliyotufanyia kwa miaka mingi, sasa tunaomba dalada," alisema Seif.


Idd alisema kuwa usafiri wa mabasi kutoka Pungu kupita Kisarawe na vitongoji vingine mpaka kufika Masaki nauli yake sh. 4,000, lakini kuna mzunguko mkubwa vyombo hivyo hutumia zaidi ya masaa mawili hali inayowachosha. 






Saturday, May 25, 2024

SERIKALI KUREJESHA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIKA NA MVUA-MAJALIWA

 

SERIKALI KUREJESHA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIKA NA MVUA-MAJALIWA

Asisitiza mpango wa Serikali wa kukuza sekta ya kilimo

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imejipanga kuendelea kurejesha miundombinu yote ya barabara zilizoathiriwa na mvua zilizonyesha nchini.

Amesema hayo leo (Jumamosi Mei 25, 2024) alipokagua daraja lililopo katika kijiji cha Nambilanje ambalo limeharibika kutokana na mafuriko. Daraja hilo linaunganisha Wilaya za Liwale na Ruangwa.

“Kwa wakati huu ambao barabara nyingi zimekatika na kuharibiwa na mvua, Sio mkoa wa Lindi pekee, eneo hili TANROADS wameshafika, wameangalia hii hali na Waziri wa Ujenzi ameshatoa taarifa kwamba wanaendelea na uhakiki”

Amesema kuwa Serikali inasubiri taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kuisha kwa mvua ili itoe fedha na kutangaza zabuni za ujenzi za ukarabati na matengenezo ya maeneo yote yaliyoathiriwa.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa pole kwa watanzania wote waliopata athari ya mvua hizo “Nawasihi muendelee kuwa watulivu na mjenge imani na Serikali yenu Mheshimiwa Rais katika mipango yake nina uhakika daraja litafanya kazi”.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amegawa pampu ishirini na mabomba yatakayotumika kumwagilia kwenye bustani za mbogamboga kwa wakazi wanaojishughulisha na kilimo hicho eneo la Nandagala wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi wachangamkie fursa ya  kilimo hicho kwani kilimo cha mbogamboga kinawezesha mkulima kupata kipato cha haraka “Tunataka eneo hili liwe kituo kikuu cha upatikanaji wa mazao ya mbogamboga”

Aidha amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati endelevu ya kukuza sekta ya kilimo ikiwemo mpango wa kutumia mabonde mbalimbali nchini ikiwemo yaliyo katika wilaya ya Ruangwa kukusanya maji ya mvua na kuyatumia katika kilimo na mifugo.





KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AKOSHWA NA MRADI WA KITEGA UCHUMI WILAYA YA LIWALE 

 

KIONGOZI wa Mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mzava  ameonyesha kuridhishwa na mradi wa  ujenzi wa vibanda 34 vya biashara katika eneo la stendi kuu ya mabasi Halmashauri ya wilaya ya Liwale  wenye Thamani ya shilingi milioni 137, 754, 450.00

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kuona utekelezaji wa mradi Mzava ameipongeza halmashauri hiyo kwa maono makubwa ya kuongeza chanzo kipya cha mapato  kitakachowasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo 

Hata hivyo Mzava ametoa siku tatu kwa halmashauri hiyo kuandaa mikataba mipya watakayoingia na wafanyabiashara wanaotumia vibanda hivyo

" pamoja na kuwapongeza kwa kubuni chanzo cha mapato lakimi niwaagize halmashauri kuandaa mikataba mipya mutakayowapa wafanyabiashara hawa ambao wapo kwenye vibanda hivi ndani ya siku tatu kuanzia leo mei 25 hadi 29 mwenge wa uhuru uwe umeshapata taarifa ya utekelezaji wake" alisisitiza Mzava

Kwa upande wake kaimu afisa Mipango wa halmashauri hiyo Hamisi Abdallah  amesema Ujenzi wa vibanda hivyo ulilenga kuongeza vyanzo vipya katika halmashauri hiyo  ambapo hadi sasa halmashauri imeshakusanya shilingi milioni 25, 296,500.00 zilizotokana na ukodishaji wa vibanda hivyo kati ya bajeti ya shilingi 44, 480, 000.00 zilizopangwa kukusanywa kwa mwaka 2023/2024

" kukamilika kwa mradi huu, umewezesha  mazingira mazuri ya wananchi kujiajiri wenyewe na pia kuongeza wigo wa ukusanyaji wa  mapato ya Halmashauri na kodi kwa TRA"

Kwa upande wake   Johari Hamisi mfanyabiashara katika vibanda hivyo amesema toka halmashauri kujenga vibanda hivyo ha wao kukodishwa wamekuwa wakinufaika kutokana na kuwa na  mazingira mazuri na ya kuvutia ya kufanyia biashara