WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wa Vyama vya Ushirika waliokula fedha za
wakulima wa korosho wilayani Masasi wazirudishe na wakishindwa mali zao
zikiwemo nyumba zitauzwa ili kufidia.
Pia
Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa ahakikishe
anawasaka viongozi wa chama Ushirika cha Msingi cha Nanyindwa wilayani Masasi
ambao wamekula fedha za wakulima na kisha kutoroka.
Amesema
viongozi wa vyama vya Ushirika katika wilaya hiyo si waaminifu, ambapo mwaka wa
fedha 2016/2017 jumla ya sh. bilioni 2.3 za wakulima ziliibiwa na viongozi hao,
ambapo mwaka 2017/2018 sh. bilioni 1.7 zimeibiwa.
Waziri
Mkuu alitoa maagizo hayo jana (Jumatatu, Februari 2018) alipozungumza kwa
nyakati tofauti na wananchi pamoja na watumishi wa wilaya akiwa kwenye ziara
yake ya kikazi mkoani Mtwara.
Alisema
viongozi wa Ushirika wa Nanyindwa ambao wametoroka ni Michael Mkali, Yusuph
Mataula, ambapo alimuagiza Bw. Byakanwa kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo
vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Pia
Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini
kuvichunguza vyama vya Msingi katika maeneo na wakikuta kuna kiongozi amekula
fedha za wakulima wamkamate na kumchukulia hatua za kisheria.
Alisema
wakati wa watu kuomba kuchaguliwa kuongoza vyama vya Ushirika kwa lengo la
kujitajirisha umepita na Serikali imedhamilia inawasimamia wakulima wa mazao
mbalimbali nchini wakiwemo wa korosho ili kuhakikisha nao wananufaika.
Waziri
Mkuu alisema vyama vya Ushirika wilaya hiyo vinaongoza kwa ubadhilifu wa fedha
za wakulima ambapo wiki iliyopita Bw. Byakanwa aliwakamata viongozi 36 wa Vyama
vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) wilayani Masasi.
Viongozi
hao ambao ni wenyeviti na makatibu wanakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa
fedha za wakulima wa korosho ambazo ni zaidi ya sh bilioni 2.3, ambazo ni
malipo ya zao hilo kwa msimu wa ununuzi 2016/2017 na 2017/18.
Alisema
mbali na wafanyabiasharahao, pia Meneja wa benki ya NMB tawi la Masasi, Aidan
Msuya anaye alikamatwa kwa tuhuma za kufanya muamala wa fedha za malipo ya
wakulima sh milioni 45 kwa zaidi ya mara 11 kwa siku moja.
Waziri
Mkuu alimpongeza Bw. Byakanwa kwa hatua alizozichukua dhidi ya viongozi
hao na kumuagiza ahakikishe viongozi wote waliosababisha ubadhirifu huo
wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.