Kaimu
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Semu
Mwakyanjala akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu ulaghai kupitia simu za
mkononi unaofanywa na matapeli katika kipindi hiki. Kulia ni Afisa Uhusiano wa
TCRA Bi. Mabel Masasi.
.....................................
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tahadhari
kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini kuwa makini na utapeli unaofanywa
kupitia simu za mkononi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Meneja Mawasiliano
kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Semu Mwakyanjala wakati
akizungumza na waandishi wa habari.
Semu alisema kuwa kuna ongezeko la matapeli wanaoghushi utaratibu wa
mawasiliano na kuwalaghai watu kutuma pesa kwa simu za mkononi hivyo Mamlaka na
vyombo vya usalama vinashughulikia suala hilo.
“Usitekeleze maagizo yoyote yanayohusu fedha kwa mawasiliano ya simu hata
kama yanatoka kwa mtu unayemfahamu, mpigie aliyekutumia ujumbe kwa namba
nyingine ili kuthibitisha’’ alifafanua Semu.
Alitahadharisha kuwa mtu akipokea taarifa kwa njia ya simu au ujumbe
mfupi wa maandishi kuwa ametumiwa fedha kimakosa na kutakiwa kuzirudisha
asifanye hivyo mpaka atakapojiridhisha na uhalali wa taarifa hiyo.
Akizungumzia matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya mitandao, Semu
alibainisha kuwa kwa miezi miwili ya Novemba na Desemba 2016 jumla ya fedha
iliyopita kwenye mitandao ya simu za mkononi ni shilingi trilioni 13.07 hali
inayothibitisha ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya
mitandao hapa nchini.
Alitaja makampuni yaliyohusika na takwimu za miamala hiyo kuwa ni Zantel
(EASY PESA), Tigo (TigoPesa), Vodacom (M PESA), Airtel (Airtel Money) na
Halotel (HALOPESA).
Aidha aliwataka wananchi kutoa taarifa polisi kuhusu matapeli na
kuwasilisha malalamiko yao ya huduma za mawasiliano kwa TCRA kupitia sanduku la
posta 474 Dar es salaam au wafike kwenye ofisi za TCRA zilizo karibu au wapige
simu namba 0784 558270, 0784 558271 na barua pepe (malalamiko@tcra.go.tz)
No comments:
Post a Comment