Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe.Prof. Makame Mbarawa, akionesha kitu kwa mbele (hakionekani pichani)
kwa Mkurugenzi wa mradi huo, Mhandisi Mohammed Millanga, wakati alipofanya
ziara kukagua ujenzi wa jengo la tatu la abiria (TBIII). Kulia ni Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Salim Msangi.
Mhe.
Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, akitoa
tathmini ya ujenzi wa jengo la tatu la abiria (TBIII), mara baada ya
kulitembelea. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TAA (MAB), Prof.
Ninatubu Lema bna kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Salim Msangi.
.....................................
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa
amesema serikali italipia haraka vifaa vya ujenzi wa jengo la tatu la abiria la
Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) vilivyokwama
bandarini.
Mhe. Prof. Mbarawa alisema hayo hivi karibuni mara baada ya kufanya ziara
ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, ambapo alijibu moja ya
changamoto zilizosomwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege
Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi kuwa vifaa vya ujenzi vimekwama bandarini.
“Hivi vifaa vitalipiwa haraka ili mradi uendelee na kumalizika kwa wakati
kama ilivyosemwa utakamilika mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu 2017,”
alisema Mhe. Prof. Mbarawa.
Alisema anaamini kukamika kwa jengo hili litakuwa bora kwa nchi za Afrika
Mashariki na Kati, kwa kuwa litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni
sita kwa mwaka, na litapunguza msongamano uliokuwepo katika jengo la pili la
abiria (JNIA-TBII), ambalo lilijengwa kwa ajili ya kuhudumia abiria 1.5 milioni
kwa mwaka, lakini sasa linahudumia abiria 2.5 milioni kwa mwaka.
Awali, Mhe.Prof. Mbarawa alisema hii ni mara ya tatu kutembelea jengo
hili, na amefanya hivyo ili kumsimamia mkandarasi kwa karibu aweze kutoa mradi
mzuri usiokuwa na tatizo kwa siku za usoni.
Pia alisema serikali imejipanga kuboresha miundombinu ya viwanja vya
ndege ili ndege yake ya Shirika la ndege (ATCL), ambayo imezindua safari zake
katika baadhi ya mikoa iweze kutoa na kupaa bila tatizo.
“Huu mradi wa TBIII sio pekee, vipo viwanja 13 vitaboreshwa kwa kufanyiwa
ukarabati na upanuzi, na baadhi yake ni Mwanza, JNIA TBII, KIA, Songwe,
Sumbawanga, Tabora, Shinyanga na Kigoma,” alisema Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
Awali akisoma taarifa fupi ya mradi wa TBIII, Kaimu Mkurugenzi, Bw.
Msangi alisema mradi huo umekumbwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha kiasi
cha Euro 121,634,888.30, ambazo serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango
iliahidi kukamilisha taratibu upatikanaji wa fedha mapema ili kutoathiri
utekelezaji wa mradi.
Pia Bw. Msangi alisema changamoto nyingine ni uchelewaji wa malipo ya
kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwa vifaa vilivyopo bandarini hadi sasa
inadaiwa Tsh. Bil. 1,362,801,347.00, kati ya fedha hizo Tsh. Mil.
960,153,258.00 ni za kulipia vifaa maalumu vya usalama vya ukaguzi wa abiria
(X-ray machine), ambavyo vinatakiwa visiathiriwe na joto.
“Hali hii ya vifaa kuchelewa kutoka inasababisha kuongeza gharama za
mradi pamoja na kuchelewesha kazi zilizopangwa kufanyika, na pia hali hii
itasababisha uharibifu wa vifaa ambapo serikali itabidi kuvilipia pindi
itakapotokea uharibifu,” alisema Bw. Msangi.
Hatahivyo, Bw. Msangi alisema ujenzi wa jengo hilo utakaotumia gharama ya
Tsh. Bilioni 560, sasa umekamilika kwa asilimia 66.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAHUSIANO CHA TAA
Mkurugenzi
wa Mradi wa Jengo la Tatu la abiria (TBIII), Mhandisi Mohammed Millanga
akiendelea kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya ujenzi kwa Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (aliyeshika miwani),
wakati alipokagua ujenzi wa jengo hilo.
No comments:
Post a Comment