Kumekuwa na taarifa za upotoshwaji kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula
hapa nchini ambapo hali hiyo inasababisha wananchi kukata tamaa ya kuendelea
kufanya kazi hasa ya kilimo na badala yake kubaki kuilalamikia Serikali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Dkt. Charles Tizeba wameihakikishia nchi kuwa Tanzania iko salama na chakula
kipo cha kutosha hivyo wananchi wasisikilize watu wengine ambao wana nia ya
kuupotosha Umma.
Akizungumza baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa
alisema nchi haijakumbwa na baa la njaa na aliwataka Watanzania kutosikiliza
kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kuhusu hali ya
chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la kupandisha bei
za vyakula.
Nae Waziri Tizeba alisema kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni
ya kuridhisha na kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazodai kuwa hali ya
chakula ni mbaya.
Tatizo kubwa lililopo ambalo linawachanganya Watanzania wengi ni
kuchanganya kati ya ukame na ukosefu wa chakula, wanaamini kuwa nchi ikiwa na
ukame lazima kutakuwa na njaa lakini si kweli kuwa vitu hivi vinaendana.
Nchi yaweza kuwa imekumbwa na janga la ukame lakini isiwe na janga la
njaa kwani kuna mazao ambayo yanastahimili ukame ambayo yanaweza yakalimwa na
kutoa mazao yatakayowawezesha wananchi kujipatia chakula pamoja na kuuza ziada
ya chakula hicho ili kupata fedha za kujikimu.
Mazao mengi ya jamii ya nafaka yana uwezo mkubwa wa kustahimili ukame,
mazao hayo ni pamoja na mihogo, viazi na mahindi, hivyo wananchi wanapaswa
kwenda na wakati kama hali ya nchi ni ya ukame basi walime mazao yanayoendana
na wakati huo na si vinginevyo.
Tusiwe wabishi kung’ang’ania kufanya kilimo ambacho tumekizoea kwani hali
ya hewa ama tabianchi kubadilika ni jambo lisiloepukika na linatokea muda
wowote, hakuna wa kulaumiwa kuhusu mabadiliko hayo zaidi ya wananchi wenyewe
kukubali mabadiliko hayo na kwenda sawa nayo.
Pia tunashauriwa kutumia mbegu zitakazokomaa mapema ili kupata mavuno kwa
haraka na kwa wingi pamoja na kutumia mazao wanayoyapata kwa uangalifu na
kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya.
Serikali pia inajitahidi kwa hali na mali kuwasaidia wananchi kuwa na
maisha bora ambapo pamoja na kuwepo kwa hali nzuri ya chakula.
Serikali kupitia
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kuweka akiba ya chakula
kwa kununua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi ili kuhakikisha nchi inaendelea
kuwa na chakula cha kutosha,
Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, FAO, TFNC
pamoja na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya hali ya chakula
na lishe nchini ambayo inatarajiwa kukamilika Januari 28 mwaka 2017 na
itazihusisha Halmashauri 55, tathmini hiyo itaiwezesha Serikali kupata taarifa
za uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe nchini.
Hivyo wananchi wanatakiwa wafanye kazi, wasifate maneno ya watu yenye
lengo la kupotosha jamii bali wawasikilize viongozi wao ambao waliwachagua
wakiamini kuwa watawaongoza na watawatatulia matatizo yao.
No comments:
Post a Comment