Mkurugenzi
wa Idara ya Nyumba Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Michael
Mwalukasa akizungumza na Waandishi wa Habari Leo Jijini Dar es salaam kuhusu
mfuko wa kuwawezesha watumishi wa Serikali kumiliki Nyumba ambapo zaidi ya watumishi
2000 wameshanufaika na mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 3 ili kuwawezesha
kumiliki nyumba bora. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Mikopo ya Nyumba Bi Lucy
Kabyemera na Kushoto.
Mkurugenzi
Msaidizi Mikopo ya Nyumba,Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Lucy
Kabyemera akifafanua kwa waandishi wa habari kuhusu faida wanazopata watumishi
wa Umma kutokana na mikopo inayotolewa na Serikali ili kuwawezesha kumiliki
makazi bora. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Nyumba Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Michael Mwalukasa.
................................
Serikali imewawezesha watumishi zaidi ya 2000 kumiliki nyumba bora kwa
kuwapatia mikopo yenye riba nafuu na kuchangia kuongeza tija katika utumishi wa
umma.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Nyumba Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Bw. Michael Mwalukasa wakati akizungumza na waandishi wa
habari leo Jijini Dar es salaam.
Mwalukasa alisema kuwa kupitia Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa
Serikali watumishi wengi walioomba mikopo hiyo wameweza kupewa kwa lengo la
kuwawezesha watumishi wa Serikali wa ngazi zote mijini na vijijini kujenga,
kukarabati au kununua nyumba.
“Mfuko huu umewawezesha watumishi wa Serikali kujenga nyumba kwenye
maeneo yenye hadhi na yanayokubalika kisheria hivyo kuchochea kasi ya
maendelezo ya nyumba kwenye Miji na Wilaya zote hapa nchini” alisisitiza
Mwalukasa.
Akifafanua Mwalukasa amesema kuwa watumishi wanaokopa kwenye mfuko huo
hurejesha mikopo hiyo kwa riba nafuu ya asilimia tatu tofauti na taasisi
nyingine ambazo hutoza riba kubwa.
“Tofauti na taasisi nyingine ambazo hukopesha nyumba iliyokamilika na
kutoza riba kubwa, mfuko huo unatoa mikopo kwa ajili ya kujenga,kununua na
kuboresha nyumba na kuwapa fursa watumishi kukopa kadiri ya uwezo na matakwa
yao ya ujenzi”. Alisema Mwalukasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Mikopo ya Nyumba Bibi Lucy
Kabyemera aliongeza kuwa baadhi ya wakopaji pia hunufaika na ushauri wa kutumia
teknolojia ya gharama nafuu za ujenzi kutokana na tafiti zinazofanywa na
Taasisi ya Utafiti wa Vifaa vya Ujenzi wa Nyumba Bora (NHBRA).
Pia Kabyemera aliwataka watumishi wa Serikali kutumia fursa hiyo ili
waweze kumiliki nyumba bora kwa gharama nafuu katika maeneo yaliyopimwa.
Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Serikali ulianzishwa na
Serikali mwaka 1963 kupitia waraka namba 8 na baadae kuendeshwa kupitia waraka
wa watumishi wa Serikali namba 4 wa mwaka 1965.
Baadhi
ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Leo Jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment