Wednesday, March 25, 2020

SERIKALI YAPOKEA MSAADA WA VIFAA VYA KUKABILIANA NA CORONA (COVID-19)

WAMJW – Dar es Salaam.


Serikali imepokea msaada wa vifaa kinga kutoka China kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na mlipuko wa maambukizi ya homa kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi vya Corona (COVID-19) kutoka taasisi ya Jack Ma na Alibaba.


Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Muhammed Bakari Kambi amesema msaada huo ambao umetolewa na Taasisi ya Jack Ma na Alibaba ni pamoja na mavazi (PPE) 1,000 ya kujikinga wakati wa kuhudumia watu waliobainika kuwa na ugonjwa huo ni pamoja na vitendanishi (Rapid Tests) 20,000 na Barakoa (Masks) 100,000.


Prof. Muhammed amesema msaada huo utawasaidia wataalamu wa afya nchini wakati wa kuwahudumia waliobainika na watakaobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona.


“Tunashukuru kwa msaada huo kama serikali,tumekuja hapa kushuhudia sehemu ya shehena ya tani tatu ya vifaa-tiba vilivyotolewa na Taasisi ya Jack Ma na Alibaba ambavyo vimewasili usiku wa leo na ndege ya mizigo ya Jamhuri ya Shirikisho la Kidemokrasia Ethiopia,” amesema Prof. Muhammed.


Katika hatua nyingine, Prof. Muhammed amemshukuru Afisa Ubalozi wa Jamhuri ya Shirikisho la Kidemokrasia Ethiopia Ndg. Tewodros Girma ambaye amekabidhi msaada huo kwa niaba ya Balozi wa nchi hiyo, Mhe. Yonas Yosef.

No comments:

Post a Comment