Monday, March 9, 2020

WANAWAKE MTWARA WAWAFANYIA UKATILI WAUME ZAO.

HADIJA HASSAN, MTWARA.

WAKATI Dunia ikiadhimisha siku ya wanawake kwa kupinga ukatili dhidi ya kina mama, hali imekuwa tofauti kwa wanawake wa wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara kwa kugeuka vinara wa kuwafanyia ukatili waume zao.

Hayo yameelezwa na afisa tawala wa wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara fransisi Mkuti kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Sebastian Waryoba wakati wa sherehe ya wanawake iliyoadhimishwa kiwilaya katika kijiji cha Chingungwe Wilayani humo.

Mkuti alisema kuwa licha ya mashirika na asasi mbali mbali za kiraia kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake lakini bado kina mama wa wilaya hiyo wamekuwa vinara wa kuwafanyia ukatili waume wao.

“kuna kinamama wanawafanyia ukatili waume zao, kuna kina mama wababe wanawapiga waume zao, wanawapiga biti, wakikaribia kupanda kitandani wanawaambia piga magoti hapo leo hupati mpaka useme ulikuwa wapi? Mnatutaabisha sio vizuri” alifafanua Mkuti.

Hata hivyo Mkuti alieleza kuwa pamoja na mateso na ukatili huo wanaofanyiwa wanaume lakini bado wameonyesha kuwa wavumilivu na kubakia kukaa kimiya kwa kuona aibu kueleza yanayowakuta.

Kwa upande wake Afisa mradi wa kuboresha huduma za kisheria (LIWOPAC) Bi Fatuma Nyama alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 77% ya mashauri mbali mbali yanayopokelewa kwa wasaidizi wa kisheria yanahusiana na wanawake huku asilimia 23% zikiwa ni za wanaume.

Alisema kuwa kati ya mashauri 558 yaliyopokelewa na shirika hilo kwa mwaka 2019 mashauri 430 yaliripotiwa na wanawake na mashauri 128 yaliripotiwa na wanaume.

No comments:

Post a Comment