Sunday, March 15, 2020

AJALI YA MOTO MOROGORO YAWAJERUHI WAANDISHI WA HABARI

Na Rashid Mtagaluka, Morogoro .

Waandishi wa Habari watatu kutoka vyombo habari tofauti mkoani Morogoro wamejeruhiwa na Moto wakati walipokuwa wakikusanya taarifa za ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 8:30 mchana wa leo Machi 14,2020 mjini Morogoro. 


Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Morogoro Kamishina Msaidizi Mwandamizi Gudluck Zerote amesema, chanzo cha tukio hilo hakijafahamika, ingawa Kamanda Zerote alikiri huwenda mrundikano wa mitungi ya gas iliyowekwa kiholela kwenye mojawapo ya chumba kwenye nyumba hiyo ukachangia. 


Kwa mujibu wa Kamanda Zerote, waliojeruhiwa kwenye tukio hilo lililotokea mtaa wa Mzambarauni ulioko kata ya Mafisa ni Hassan Ninga wa Imaan Media, Omar Hussein wa Sahara Media na Salum Yusuf wa Abood Media ambao wamekimbizwa hospital ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro. 


"Tumepokea taarifa ya Moto majira ya saa 8:39 mchna wa leo na ilipofika saa 8;45 tulishafika hapa na wakati tukizima moto upande huu kumbe kulikuwa na chumba kimoja kilikuwa kimehifadhiwa mitungi mitano mikubwa ya gas" ,alisema Zerote na kuongeza. 


"Lakini muda mfupi ndipo mitungi hiyo iliyokuwa imehifadhiwa bila kibali na mfanyabiashara ambaye hatujapata jina lake, ikaanza kulipuka mmoja baada ya mwingine, tukaamua kusubiri pembeni maana gas ikishawaka kiasi hicho huwezi kuzima kwa kutumia maji, hivyo tukasubiri ipowe". 


Aidha Kamanda Zerote ametoa wito kwa wananchi kutohifadhi gas zaidi ya ile ya matumizi yao ya kawaida Kama ilivyotokea kwenye nyumba hiyo iliyoharibika vibaya kutokana na watu kuvunja madirisha ili kujinusuru. 


Naye mwenyekiti wa mtaa huo wa Mzambarauni Mohammed Salum amesema tukio hilo licha ya kuwajeruhi waandishi wa Habari watatu, pia limeleta taharuki mtaani hapo kwa baadhi ya wakaazi kukimbia ovyo bila kuchukua tahadhari nankusababisha baadhi yao kuumia. 


Pia kiongozi huyo ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mtaani humo ameishauri Mamlaka husika kupiga marufuku biashara ya gas kufanyika kiholela bla kuzongatia sheria, kanuni na taratibu ili kuepusha madhara kwa jamii. 


Kwa upande wake diwani wa kata ya Mafisa kulikotokea tukionhilo Bwana Alli Rashid Kalungwana amesema pamoja na tukio hilo kusababisha maafa kwa tasnia ya habari, lakini hakukuwa na madhara zaidi kwa wananchi wa kata yake. 


Nao baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema iko haja kwa serikali na vyombo vyake vya dola kuongeza juhudi ya kutoa elimu ya matumizi sahihi ya nishati hii mbadala kwa lengo la kuwasaidia wananchi kufahamu jinsi ha kujikinga na ajali za Moto. 


Rajab Farijala Rajab ambaye ni miongoni mwa wananchi wa kata ya Mafisa Manispaa ya Morogoro ameiomba serikali kuangalia upya sheria inatoruhusu wafanyabiashara wa gas kuhifadhi mitungi mingi na mikubwa kwenye nyumba moja inayoishi watu, ili kuokoa nguvu kazi kubwa ya Taifa

No comments:

Post a Comment