Friday, March 20, 2020

DC LINDI ATAKA WATOTO WASITEMBEE HOVYO KUEPUKA CORONA


NA HADIJA OMARY, LINDI.

MKUU wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga amewataka Wazazi na Walezi Wilayani humo, kuhakikisha Watoto hawatoki Majumbani mwao baada ya Shule kufungwa ili kuendelea kuchukuwa taadhari dhidi ya ugonjwa wa corona.

Ndemanga ameyasema hayo jana alipokuwa anazungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG baada ya kubaini uwepo wa mikusanyiko ya watoto katika Mitaa mbali mbali ya Manispaa ya Lindi wakiwa katika michezo yao.

Aidha, alisema kuwa lengo la Serikali kufunga Shule hizo ni moja ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa hatari wa corona kwa kupunguza misongamano ya watu katika maeneo mbali mbali.

“lengo la Serikali kufunga Shule lilikuwa kuwanusuru watoto hao pamoja na familia zao na ugonjwa huo kwa kupunguza misongamano na mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima sasa kama watoto hao wataendelea kufanya mikusanyiko mingine wakiwa nje ya shule basi haitakuwa na maana kwa shule kufungwa” alisema Ndemanga.

Ndemanga alisema kuwa ni wajibu wa mzazi au mlezi kuhakikisha kuwa mtoto haendi kwenye mikusanyiko ya michezo yoyote ikiwa ni pamoja na mchezo wa mpira, kuogelea bichi na kadhalika.

“Endapo mtoto ataachwa akienda mtaani na mzazi pasipokujua yupo wapi ikitokea kwa bahati mbaya tatizo amepata huko la ugonjwa wa corona sasa atakuwa analeta ugonjwa ndani jambo ambalo Serikali haikupenda litokee” alieleza Ndemanga.

Ndemanga alisema ili kuendelea kuwalinda watoto hao ni wajibu wa wazazi kwa kushirikiana na Serikali kuendelea kutoa elimu kwa watoto wao juu ya ugonjwa huu hatari wa Corona.

Nae Mganga Mkuu wa Manispaa ya Lindi Libamba Sobo alisema kuwa katika mikusanyiko ya michezo ya watoto sio tu hatari kwa watoto wale waliofunga Shule bali hata watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano nao ni hatari zaidi kwa kufikwa haraka na magonjwa kutokana na kinga zao.

Pamoja na mambo mengine alisema kuwa taadhari ya kunawa mikono kila baada ya muda inaweza kuwa msaada mkubwa wa kutopata maabukizi ya virusi hiyo vya corona hivyo ni wajibu wa wazazi na walezi kuwakumbusha watoto wao kunawa mikono mara kwa mara wanapotoka kucheza hata kama wakiwa maeneo ya nyumbani Kwa upande wake yusuph khatibu (8) mwanafunzi wa Darasa la pili katika shule ya Msingi Stadium iliyopo katika Manispaa hiyo ya Lindi aliwahasa watoto wenzao kuacha kukusanyika katika michezo mbali mbali mpaka pale ugonjwa huo utakapoisha au utakapopatikana tiba yake
 

No comments:

Post a Comment