Monday, March 9, 2020

JELA MIAKA 5 KWA KOSA LA WIZI KAZINI.

KIBAHA MARCH 09.2020

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Mkoa wa Pwani, leo imemuhukumu aliyekuwa meneja wa kituo cha kuuza mafuta cha UKODI INTERNATIONAL COM LIMITED Malima Charles mwenye umri wa miaka 40 mkazi wa Maili moja Kibaha, kwenda jela miaka mitano (5) baada ya kumkuta na hatia katika makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili mahakamani hapo ambayo ni KUVUNJA OFISI NA WIZI.

Akisoma hukumu hiyo iliyodumu kwa muda wa saa moja ambayo ilivuta hisia za wakazi wa Kibaha Mkoa wa Pwani, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Joyce Mushi, ameeleza kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamuhuri na ili kuwa fundisho kwa watumishi wengine wanopewa dhamana ya kusimamia vituo vya mafuta, mahakama imemkuta na hatia na kumhukumu kwenda Jela miaka 5 kwa makosa yote mawili

Mtuhumiwa huyo amekutwa na hatia kufuatia mahakama hiyo kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamuhuri kufutia makosa yote mawili yaliyokuwa yakimkabili na hivyo kumtia hatiani na kutakiwa kutumikia kifungo hicho cha miaka mitano kwa makosa yote.

Mwendesha mashtaka katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali Auleilia Mushi alieleza mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa akiwa meneja wa kituo cha kuuza mafuta cha UKODI INTERNATIONAL COM LIMITED, alikula njama za kuvunja ofisi na kuiba kiasi cha fedha za Kitanzania zipatazo milioni 45,266,133 za mwajiri wake na kutoweka kusikojulikana huku akijua fika kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Mwendesha mashitaka huyo wa Serikali aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo alivunja ofisi hizo tarehe 24.12.2018 na kuondoka na mauzo ya siku husika ambayo yalikuwa hayajapelekwa kuhifadhiwa Benki kutokana na siku hiyo kuwa ni siku ya mwisho wa juma na baada ya kutekeleza wizi wake akatoweka hadi pale jitihada zilipofanyika za Jeshi la Polisi kuweza kumsaka na kumtia nguvuni na kuweza kufikishwa mbele ya vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.

Akijitetea mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo mtuhumiwa huyo Malima Charles maarufu kwa jina la Mukama alikiri kufanya kosa hilo na kuiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na anafamilia inayomtegemea na yeye akiwa anamatatizo ya kiafya.

No comments:

Post a Comment