Sunday, March 15, 2020

MACHOKODO, MAKAMO MWENYEKITI COREFA AZIKWA BAGAMOYO.

 Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Hasanoo, (kushoto mwenye kapelo) akipokea jeneza liliobeba Mwili wa aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho, Marehemu Shabani Omari Kangale (Machokodo) aliyefariki ghafla kwa ugonjwa wa Pumu.
............................................


Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Shabani Omari Kangale (Macho kodo) amefariki dunia akiwa nyumbani kwake huko Bagamoyo usiku wa tarehe 13 Machi 2020.


Taarifa zilizotolewa na familia ya marehemu zilisema marehemu alikuwa akisumbuliwa na pumu na kwamba sababu ya kifo chake ni pumu iliyombana kwa kasi.


Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Hassan Hasanoo alisema kifo cha Kangale ni pigo kubwa kwa COREFA na wana michezo wote mkoa wa Pwani.


Alisema Kangale alikuwa sio ni Makamo Mwenyekiti bali alikuwa ni zaidi ya Makamo Mwenyekiti kwa umahiri wake katika uongozi, busara na moyo wa kujitolea katika mambo mbalimbali yanayohusu chama cha mpira Pwani.


Watu mbalimbali waliohudhuria katika mazishi hayo wamemzungumzia marehemu Kangale kuwa ni mtu mwenye kupenda ushirikiano katika mambo mbalimbali ya kijamii jambo ambalo litafanya aendelee kukumbukwa.


Aidha, viongozi waliowakilisha makundi yao wamesema Marehemu Shabani Kangale (Machokodo) ni mtu wa kipekee katika utendaji wake wa kazi na namna anavyoweza kushughulikia matatizo.


Mashjabiki wa mpira wa miguu Bagamoyo na Mkoa wa Pwani kwa ujumla wamesema Chama cha Mpira wa miguu mkoa wa Pwani kimepata pigo kwa kuondokewa na kiongozi mchapa kazi, mpenda watu, na mwepesi wa kushughulikia matatizo.


Marehemu Shabani Omari Kangale (Machokodo) amezaliwa mwaka 1957 na kupata elimu yake ya usimamizi wa fedha, katika chuo cha IFM mwaka 1980 na kwamba katika uhai wake alifanya kazi sehemu mbalimbali ikiwemo TAMCO KIBAHA, KIWANDA CHA URAFIKI, TIPA, SCANIA, KAGERA SUKARI, KJ MOTORS, NASSACO, STEEL CAST NA MUWA.


Aidha, marehemu Kangale alihamia Bagamoyo mwaka 2003 na kuendelea na biashara zake binafsi.


Akiwa Bagamoyo aliwahi kuwa mweka hazina wa Chama cha mpira wa Miguu wilaya ya Bagamoyo (BFA) mwaka 2008 mpaka 2012.


Alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wilaya ya Bagamoyo (BFA) Mwaka 2012 mpaka 2016.
Kuanzia 2016 alikuwa Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa miguu mkoa wa Pwani (COREFA) mpaka umauti unamkuta.


Marehemu ameacha wake wawili, watoto sita na wajukuu watano
Mwenyezimungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Aamiyn.
Watu mbalimbali waliohudhuria mazishi ya aliykuwa Makamo Mwenyekiti wa Mpira wa miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Shabani Omari Kangale (Machokodo) wakiomba dua wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake Majengo Bagamoyo mjini hapo jana Machi 14, 2020.
 Swali ya jeneza iliyoswaliwa kwaajili ya marehemu Shabani Kangale (Machokodo) Nyumbani kwake Majengo mjini Bagamoyo Machi 14, 2020.
 
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Hasanoo, (kushoto mwenye kapelo) akiwa kwenye msiba wa aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Pwani, Shabani Kangale, katikati ni Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Kisarawe, Ally Mkomwa.
 
 Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Hasanoo, (kulia) akiwa eneo la makaburi Mwanakalenge Bagamoyo mahali ambapo amezikwa Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Shabani Omari Kangale (Machokodo).
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Bagamoyo na nje ya Bagamoyo, wakisindikiza mwili wa marehemu Shabani Omari Kangale (Machokodo) kuelekea makaburi ya Mwanakalenge Bagamoyo mjini, Machi 14, 2020.

No comments:

Post a Comment