Friday, March 20, 2020

WAHAMIAJI HARAMU 49 WAKAMATWA BAGAMOYO.

Wahamiaji haramu 49 wamekamatwa  Wilayani Bagamoyo usiku wa kuamkia tarehe 19/03/2020 Wahamiaji hao haramu wamekamatwa na raia wema wakishirikiana na Jeshi la Polisi Wilayani Bagamoyo katika Kijiji cha Kidomole Kata ya Fukayosi.

Raia hao 49 wa Ethiopia wamekiri kuingia nchini kinyume cha sheria kwa kupitia pwani ya Bagamoyo wakitumia majahazi ikiwa lengo lao ni kuelekea Afrika kusini.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Zainab Kawawa amesema kuwa walipokea taarifa toka kwa raia wema juu wa uwepo wa kundi la watu wasiofahamika katika Kijiji cha Kidomole kilichopo Kata ya Fukayosi, na baada ya taarifa hiyo hatua za haraka zilichukuliwa na Jeshi la Polisi Wilayani humo kufika eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata wahamiaji hao haramu 49.

Mhe. Zainab ameongeza kwa kusema kuwa, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona ulioingia Nchini, tumeona ni vyema kuwafanyia vipimo vya awali vya kiafya wahamiaji hawa ili kujiridhisha kuwa wako salama kabla hawajaendelea na taratibu zingine za kimahakama.

"Hivyo tumewaleta hapa katika Kituo cha Afya Matimbwa ili kuwaangalia Afya zao kwanza hasa joto la mwili kuwaangalia kama wana homa kali, kama wana dalili zozote za kikohozi, au mafua makali, kisha wataendelea na taratibu zingine za kisheria, Alisema Kawawa.

 “Niwapongeze Wananchi wema waliosaidia kukamatwa kwa wahamiaji hawa haramu, lakini pia nitoe rai kwa Wananchi wote wa Bagamoyo kuwa wazalendo na kuacha kabisa vitendo vya kuwasaidia wahamiaji haramu na kufanya Bagamoyo kuwa uchochoro wa kupita kuelekea Nchi jirani, kuwasaidia wahamiaji haramu kupita Bagamoyo na kokote Nchini kunahatarisha usalama wa Nchi yetu hasa kipindi hiki ambacho Nchi nzima inapambana na mlipuko wa ugonjwa huu wa Corona” Alisema Mhe. Zainab Kawaw.

Jeshi la Polisi Wilayani Bagamoyo limekuwa likiwakamata wahamiaji haramu hasa wanaotoka Nchini Ethiopia na kuingia Nchini kwa kutumia pwani ya Bahari ya Hindi, wakiwa njiani kuelekea Nchi jirani na kuwafikisha katika vyombo vya Sheria ikiwa ni katika kupambana na uingiaji wa makundi haya ya wahamiaji haramu.

No comments:

Post a Comment