Monday, March 9, 2020

MBOLEA ZA VIWANDANI ZINAHARIBU MASHAMBA.

Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika Maandalizi ya eneo la kutengenezea mbolea ya asili inayotokana na kuoza kwa mimea (MBOJI).
.............................................


NA HADIJA HASSAN LINDI.

Matumizi makubwa ya kemikali na mbolea za viwandani ni moja ya sababu inayowafanya wakulima katika maeneo mengi hapa nchini kufanya kilimo cha kuhama hama kutokana na mashamba yao ya awali kupoteza rutuba ya udongo.

Hayo yameelezwa na Ofisa Mradi wa Shirika la kilimo endelevu Tanzania (SAT) Stanslaus Kisatu, katika mafunzo ya maofisa ugani jamii 37 wa vijiji vinne vya Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi yaliyofanyika katika ofisi ya kijiji cha Kinyope.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyotolewa na Shirika la kilimo endelevu Tanzania (SAT) kwa kushirikiana na SWISS AID TANZANIA yana lengo la kuwafundisha wakulima mbinu mbali mbali za kilimo hai ikiwa pamoja na urutubishaji Aridhi, matengenezo na matumizi ya mbolea ya asili inayotokana na kuoza kwa mchanganyiko wa mimea (MBOJI) ambayo itatumika katika upandaji wa mazao katika mashamba yao.

Kisatu alisema kuwa kilimo cha kuhama hama ni moja ya madhara yanayotokana na wakulima kutofuata kanuni za kilimo hai na badala yake kutumia kemikali na viuwatilifu vingine hali inayopelekea Aridhi kuchoka na kushindwa kutengeneza virutubisho kwa mimea inayopandwa.

“Aridhi ikichoka inamfanya mkulima kushawishika kufanya kilimo katika eneo lingine kutokana na kupata mazao machache kwa sababu anapopata mazao kidogo hulazimika kutafuta Aridhi mpya , hivyo kitendo hicho kinachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa misitu ya hifadhi” alisema kisatu.

“sasa hivi wakulima wamekuwa wakilalamika sana kuwa mashamba yao yanaingiliwa na nyani lakini kumbe wao wamejikuta wameanzisha mashamba katika makazi ya wanyama poli hivyo moja kwa moja wanawapelekea chakula wanyama poli bila wao kujua, lakini wakifuata mbinu za kilimo hai kulikuwa hakuna sababu ya kutoka eneo moja kwenda sehemu nyingine kwa kuwa Aridhi ambayo wanaitumia itakuwa inaboreshwa siku hadi siku” alifafanua kisatu.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema kuwa kwa kutumia kanuni hiyo ya kilimo hai licha ya kuwa ni rafiki wa mazingira lakini pia ni gharama yake ni nafuu ukilinganisha na matumizi ya kemikali na viuwatilifu vya viwandani Kwa upande wake mariamu Bwanaly Mgani jamii kutoka kijiji cha Ruhoma alisema kuwa matumizi ya mbolea ya asili inayotokana na kuoza kwa mchanganyiko wa mimea (MBOJI) ni nafuu na inaweza kutumika kwa wakulima hata wa hali ya chini kwa kuwa inatumia malighafi yanayowazunguka katika mazingira yao.

Nae Mgani jamii kutoka katika kijiji cha Kinyope alisema kuwa kutokana na mafunzo hayo amejifunza kuwa endapo wakulima wote hapa nchini wataamua kutumia mbolea ya asili (MBOJI) kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza uwezekano wa magonjwa mengi yanayotokana na matumizi ya kemikali.

Mchanganyiko wa nyasi mbichi, nyasi kavu, samadi pamoja na maji vikiwa pamoja tayari kwa kutengeneza mbolea ya asili inayotokana na kuoza kwa mimea (MBOJI) iliyotengenezwa na washiriki hao wa mafunzo



No comments:

Post a Comment