Na Eliafile Solla
Baadhi ya wananchi wanaoishi
katika Kata na Vijiji vya mpakani mwa Tanzania na nchi ya Burundi,
wamelalamikia sehemu ya ardhi yao kutumiwa kwa shughuli mbalimbali za
kibinadamu na raia jirani wa Burundi. Hayo yalijitokeza katika ziara ya
Makatibu Wakuu iliyofanyika katika Mikoa ya Kagera na Kigoma kwa lengo la
kukagua maeneo yote ya mpaka wa Kimataifa.
Makatibu Wakuu kutoka Ofisi ya
Rais- IKULU, TAMISEMI, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali walifanya ziara Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera,
kukagau zoezi la uimarishari wa mpaka uliofanyika mwaka 2014.
Ziara hiyo iliyojumuisha wataalam
mbalimbali wanaoshughulikia mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na nchi
zinazoizunguka, ilikuwa ya siku nne ambapo wajumbe walitembelea baadhi ya
maeneo yaliyopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka lililofanyika mwaka 2014.
Katika ziara hiyo pia, wataalam walitembelea maeneo ya mpaka katika Mkoa wa
Kagera ambapo walibaini, baadhi ya raia wa Burundi wanafanya shughuli nyingi za
kibinadamu katika maeneo ya mpaka kitu ambacho kiusalama siyo sawa.
Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Florens Turuka ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa
wajumbe hao alisema, lengo la kutembelea na kukagua maeneo ya mpaka wa kimataifa
uliopitiwa na zoezi la uwekaji wa alama za hifadhi ya mpaka (vigingi) mwaka
2014 ni kukusanya taarifa kutoka kwa wananchi.
Alisisitiza kwamba, taarifa itakayotolewa na wananchi katika maeneo
yaliyopitiwa na uimarishaji wa mpaka, itaisaidia Serikali kujua ni mikakati
gani iwekwe katika maeneo yanayozunguka mpaka ili kuwalinda wananchi pamoja na
mali zao.
Nae mkuu wa Wilaya ya Ngara
Luteni Kanali Michael Mtenjele, alisema katika taarifa ya Wilaya kwamba, mpaka
kati ya Tanzania na Burundi uko salama na Wilaya imeendelea kuwa na mahusiano
na mawasiliano ya karibu na nchi hiyo. Aliongeza kwamba, mara nyingi
zinapotokea changamoto mawasiliano ya simu hufanyika na nchi ya Burundi na
kuyatatua kitu ambacho kisingewezekana kama mahusiano yangekuwa siyo mazuri.
Taarifa ya Wilaya pia ilibainisha
kwamba, zoezi la uimarishaji mpaka lililofanyika mwaka 2014 liliwaathiri baadhi
ya wananchi wa Tanzania waliokuwa wanaishi mpakani. Kanali Michael alisema,
pamoja na athari ambazo tayari Wilaya ilishabainisha, wajumbe wanaweza kupata
taarifa zaidi kuhusu hali ya mpaka kutoka kwa wananchi wanaoishi mpakani
watakapokuwa wanatembelea na kukagua maeneo hayo.
Pamoja na wajumbe kutembelea na
kukagua baadhi ya maeneo yaliyopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka
2014, pia walifanya mikutano ya hadhara na wananchi wa vitongoji na vijiji
husika ili kupata taarifa ya hali ya mpaka. Katika mikutano hiyo ya hadhara,
baadhi ya wananchi walisema, zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka 2014
liliwaathiri wao na mali.
Bibi Jesca Lameck mwenye umri
kati ya miaka 75-80 ni mmoja kati ya wananchi waliosema zoezi la uimarishaji wa
mpaka la mwaka 2014 lilimuathiri. Bibi Jesca alisema, katika zoezi hilo
lililohusisha uwekaji wa alama (vigingi) katika hifadhi ya mpaka, alijikuta
sehemu ya shamba lake la miti, kahawa, matunda na makaburi vikiangukia upande
wa nchi ya Burundi.
Baada ya kutembelea na kufanya
mikutano na wananchi waliopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka 2014,
mwenyekiti Dkt Florens Turuka, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi alipokea taarifa
kuhusu athari zilizotokana na zoezi hilo, pamoja na changamoto nyingine
zinazohusu mpaka tofauti na za uwekaji alama za hifadhi ya mpaka. Aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Ngara kwa
jinsi unavyosimamia mahusiano na nchi ya Burundi na kuahidi kuifikisha mbele
zaidi taarifa aliyoipata kuhusu changamoto za mpaka wa Tanzania na Burundi.
No comments:
Post a Comment