Sunday, December 22, 2019

VULU AMSHUKURU RAIS MAGUFULI.

 Na Omary Mngindo, Kibiti

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa namna anavyoitekeleza kwa vitendo ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Vulu ametoa kauli hiyo akiwa ziarani katika wilaya za Kibiti, Kisarawe na Kibaha Mji, akihudhuria Mabaraza ya Jumuia ya Wanawake (UWT- CCM) yaliyofanyika kwenye wilaya hizo.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, imedhamiria kuwakomboa wananchi kwa kujenga hospitali mpya kila wilaya, ujenzi wa vituo vya afya, zahanati ikiwemo ununuzi wa ndege na miundombinu ya umeme, barabara sanjali na usafiri wa reli na bahari.

Akiwa Kibiti kwenye siku yake ya kwanza ya ziara hiyo, Vulu akizungumza na wana-UWT hao alisema kuwa Rais Magufuli amezifanyia kazi sekta zote, huku akishukuru zaidi sekta ya afya inayolenga kuhakikisha wanaanchi wananufaika na huduma hiyo.

"Rais wetu amefanya mambo mengi makubwa na anaendelea na juhudi hizo, niwaombe wana-UWT wa Kibiti na wilaya zote tumuunge mkono katika harakati hizo za kimaendeleo anazozitekeleza, kwa fedha zetu za ndani" alisema Vulu.

Aidha amekabidhi kipimo cha sukari na presha kwenye Kituo cha afya Kibiti, huku akimshukuru Mbunge wa Jimbo hilo Ally Ungando, Madiwani, Mkuu wa wilaya na viongozi wote sanjali na wananchi katika kujiletea maendeleo.

Akiwa Kisarawe alizungumza na wana-UWT hao kisha kuwakabidhi boksi za karatasi (rimu) kwa ajili ya matumizi ya Jumuiya zote pamoja na chama ikiwa na lengo la kuboresha utendajikazi kwa wana-CCM hao, huku akimshukuru mbunge Alhaj Suleiman Jafo kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya.


Juzi alikuwa Kibaha Mji, ambapo Vulu aliwapongeza wana-Jumuiya kwa kufanikisha ushindi serikali za mitaa, huku akimpongeza mbunge wa Jimbo Silvestry Koka kwa kazi anayoifanya akishirikiana na Mkuu wa wilaya, Madiwani na ofisi ya Mkurugenzi kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mji Judith Mluge alimpongeza Vulu na wabunge wote wa Viti Maalumu kwa namna wanavyoshirikiana katika kuiendeleza Jumuiya hiyo.

Baadhi ya wenyeviti wa UWT kata zinazounda wilaya ya Kibaha mji
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, (mwenye kilemba cha kijani) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa jumuiya ya wanawake Kibaha mji muda mfupi baada ya kuzungumza na kukabidhi boksi za karatasi

PICHA ZOTE NA OMARY MNGINDO.  

No comments:

Post a Comment