Saturday, December 21, 2019

WAZAZI PANGENI JINA LA MTOTO MAPEMA- DC KAWAWA


Na Omary Mngindo, Chalinze

WAZAZI wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wametakiwa kuandaa majina ya watoto watakaozaliwa mapema, hatua itakayowarahisishia kupata matangazo yenye majina.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo Zaynabu Kawawa, akizungumza na wananchi wa Chalinze kabla ya uzinduzi ulioenda sanjali na ugawaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa Halmashauri hiyo, ambapo watoto 11,816 kati ya 37778 wamepatiwa vyeti vyao vya kuzaliwa.

Alisema kuwa hatua ya wazazi kukubaliana jina la mtoto kabla ya kuzaliwa, itaondoa usumbufu wa upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa unaotokea hivi sasa, kwani mtoto atakapozaliwa tu kwenye cheti chake kitaandikwa jina lake.

"Niwashauri wazazi wenzangu tubadilike, tuandae majina ya watoto watakaozaliwa mapema, ili kuondokana na adha inayopatikana katika upatikanaji wa vyeti vyao, kwani mtoto akiwa na jina mapema katika cheti chake litaandikwa, hivyo kuondoa usumbufu usio wa lazima," alisema Kawawa.

Awali Mganga Mkuu wa halmashauri ya Chalinze Dr. Ernest Kyungu akisoma taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji Amina Kiwanuka, imeeleza kwamba mpango wa usajili wa watoto chini ya miaka mitano unalenga kumwezesha kila mtoto kupata cheti cha kuzaliwa.

"Vilevile mtoto atakayezaliwa kuanzia siku ya utekelezaji wa mpango huu anasajiliwa ndani ya muda mfupi baada ya tukio la kizazi kutokea, serikali kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini  (RITA) na kutekelezwa kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo," ilieleza taarifa hiyo.

Dr. Kyungu aliongeza kwamba chimbuko la mpango huo ni kutokana na ukweli kwamba, idadi kubwa ya wananchi hawajasajiliwa hivyo hawana vyeti vya kuzaliwa, hatua ambayo serikali imeamua kulipatia ufumbuzi.

"Kwa mujibu wa sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012, ni asilimia 13.4 tu ya wa-Tanzania Bara waliosajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa, baada ya kubainika kwa changamoto hii, serikali na wadau wa masuala ya usajili walifanya tathmini ya kina juu ya suala hilo," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment