Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Fatuma O. Latu, amefungua
rasmi mafunzo kwa wataalamu watakaoendesha zoezi maalumu la uandikishaji na
usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili wapatiwe vyeti vya
kuzaliwa bure.
Mafunzo
kwa Wataalamu wasajili hao yamelenga kuwajengea uwezo ili kutekeleza mpango wa
usajili wa watoto kwa kasi inayotakiwa na kwa ufanisi mkubwa.
“Ni
wajibu wenu kuhakikisha zoezi hili mnalitekeleza kwa weledi mkubwa, ili
muisaidie Serikali kupata takwimu sahihi zitakazoisaidia kupanga shughuli za
maendeleo katika Halmashauri yetu ya Bagamoyo, hivyo umakini mkubwa unatakiwa
wakati wa mafunzo ili kupata uelewa sahihi wa kutekeleza zoezi” Amesema Bi.
Fatuma Latu
Anaongeza
“Kila mtoto ana haki ya kusajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa kwani cheti
hiki kina umuhimu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kumtambulisha mtoto wakati wa
kupata huduma muhimu za kijamii, mfano; wakati wa kuandikishwa shule, kuingia
chuo kikuu, wakati wa kujiandikisha ili kupata kitambulisho cha Taifa, kuomba
pasipoti ya kusafiria na matumizi mengine mengi muhimu, hivyo ni wajibu wa kila
mzazi kuhakikisha anatumia fursa hii kuhakikisha mtoto wake anasajiliwa na
kupatiwa cheti cha kuzaliwa”
Jumla
ya watoto 14,565 wanatarajiwa kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kupitia
mpango huu maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, ambapo zoezi la
usajili wa watoto ili kupatiwa vyeti vya kuzaliwa linatarajiwa kuanza siku ya
tarehe 06/12/2019 na litaendelea hadi tarehe 19/12/2019.
Usajili
huu wa watoto utafanyika katika Ofisi za Kata zote 11 za Halmashauri ya Wilaya
ya Bagamoyo, pia katika Vituo vya kutolea huduma za Afya, ambavyo ni Zahanati
zote, Vituo vya Afya na katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, ambapo Mzazi
anatakiwa kufika katika Vituo hivyo vya usajili akiwa na nakala (copy) ya kadi
ya kliniki au tangazo la mtoto kuzaliwa ili kufanya usajili huo.
Mpango
wa usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka
mitano katika Mkoa wa Pwani, unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa
kushirikiana na Serikali ya watu wa Canada, Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia watoto (UNICEF) pamoja na Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (RITA).
No comments:
Post a Comment