Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,
Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi akitoa maelekezo kwa uongozi wa Chama
cha Maafisa Habari Tanzania (TAGCO) wa kuendeleza mpango wa kutoa mafunzo ya
mara kwa mara kwa maafisa habari wa serikalini leo alipokuwa akifunga mafunzo
ya maafisa hao yaliyokuwa yakifanyika jijini Dodoma kwa siku tano.
..........................................
Na Shamimu Nyaki – WHUSM,Dodoma
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya
Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Ally Possi amewapongeza Maafisa Habari,Uhusiano
na Mawasiliano Serikalini kwa kutangaza vizuri shuguli za Serikali ikiwemo
miradi inayotekeleza ambayo itawaletea wananchi maendeleo.
Dkt.Possi ameyasema hayo leo Jijini
Dodoma wakati akifunga mafunzo ya kimkakati ya Uandishi wa Habari za Serikali
ya awamu ya pili kwa Maafisa Habari,Uhusiano na Mawasiliano Serikalini
ambapo amewataka kutumia elimu waliyopata kuendelea kuhabarisha umma kwa weledi
na kwa usahihi habari zinazohusu Serikali.
“Maafisa Habari mnafanya vizuri
katika kutangaza shughuli za Serikali kwa wananchi,naomba muendelee kufanya
hivyo kwa kuwa kada yenu ni muhimu katika kufikisha ujumbe wa Serikali kwa
wanachi na mtumie kalamu zenu vizuri ili kulinda na kudumisha amani ya nchi
yetu”alisema Dkt. Possi.
Aidha Dkt.Possi amewataka waandaaji
wa mafunzo hayo kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali pamoja na kutumia mifumo tofauti ya ndani na nje ya nchi
pamoja na kufanya tathmini ili kuona mabadiliko yaliyopatikana kutokana na
mafunzo hayo.
Hata hivyo Dkt. Possi aliwashauri
Maafisa Habari wote wa Serikali kujiunga na Chama cha Maafisa Mawasiliano wa
Serikali (TAGCO) ili kurahisisha mawasiliano miongoni mwao pamoja na
kushirikiana katika kazi wanazofanya ikiwemo kubadilishana uzoefu na kusaidiana
kijamii na kitaaluma.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Habari –MAELEZO Bw.Rodney Thadeusi amesema kuwa jukumu
la maafisa habari wa Serikali ni kutoa taarifa sahihi na kwa wakati
zinazohuzu Serikali kwa wananchi kutumia njia zote za mawasilano.
“Maafisa habari kazi yetu kubwa ni
kuisemea Serikali tusiposema sisi wengine watasema na wengine wanaweza kusema
ambayo sio sahihi na wakati mwingine kukosoa hata yale mazuri ambayo Serikali
inatekeleza kwa wananchi wake hivyo tuendelee kutumia taaluma yetu kuitangaza
vizuri Serikali”alisema Bw.Rodney.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama
hicho Bibi.Sara Msika amesema lengo la mafunzo hayo ni kuendelea
kuboresha taaluma ya maafisa hao katika kipindi hiki ambacho dunia imekuwa na
mabadiliko makubwa katika kada hii ya uandishi wa habari.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo
hayo Afisa Habari kutoka TBC Bibi.Catherine Nyoni ameshukuru waandaaji wa
mafunzo hayo kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa Maafisa Habari Serikalini
ambayo yamesaidia kuboresha taaluma yao pamoja na kubadilishana uzoefu.
Mafunzo hayo ya siku tano
yalioandaliwa na Idara ya Habari –MAELEZO pamoja na Chama cha Maafisa
Mawasiliano Serikalini (TAGCO) yamekuwa na mada mbalimbali ikwemo namna ya
kutumia mitandao ya kijamii kuhabarisha umma pamoja na uandishi mzuri wa habari
za Serikali.
No comments:
Post a Comment