Baadhi ya wajumbe wa kamati maalum ya
kukagua mipaka ya kimataifa wakipokea taarifa ya kuhusu halisi ya mpaka wa Tanzania
na Burundi.
|
Na: Eliafile Solla
Tanzania ni nchi ambayo iko vizuri na
majirani zake kwa maana ya nchi zinazoizunguka na wananchi wake wanashirikiana
vyema na majirani zao katika masuala mbalimbali ya kijamii na kimaendeleo kama
vile biashara hasa ya kuuziana mazao.
Haya yalithibitishwa na Katibu Tawala wa
Wilaya ya Ngara mkoani Kagera Vedastus Tibaijuka wakati alipokuwa anatoa
historia ya mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Burundi kwa kamati maalum iliyojumuisha
ofisi saba za Serikali walipofika Wilayani humo kwa lengo la kutembelea na
kukagua mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi.
Katika kuimarisha mipaka ya kimataifa
kati ya Tanzania na nchi jirani zinazo izunguka, Serikali ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania imeunda kamati maalum kwa ajili ya kuhakikisha wananchi
wote wanaoishi kwenye vijiji vya mipakani wanakuwa salama pamoja na mali zao.
Kamati hiyo maalum inahusisha Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya
Rais, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Nae mkuu wa Wilaya ya Ngara Lt. Kan.
Michael Mtenjele aliieleza kamati hiyo maalum kwamba, Wilaya ya Ngara
imegawanyika katika tarafa 4 zenye jumla
ya kata 22, vijiji 75 na vitongoji 389.
Alisisitiza kwamba, Wilaya ya Ngara iko
mpakani kabisa mwa Tanzania na Burundi na hivyo siyo ajabu Watanzania kuwa na
ndugu, jamaa na marafiki upande wa Burundi au Waburundi kuwa na jamaa Tanzania.
Kwa sababu hiyo, wananchi hasa wa vijiji vya mpakani wanaishi vizuri na
majirani zao na kushirikiana katika masuala mbalimbali.
Katika taarifa yake kuhusu hali halisi
ya mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Burundi alisema, mpaka huo uko salama
na changamoto zinapojitokeza hukutana katika vikao vya ujirani mwema na
kuzitatua japo kuna baadhi ya wananchi kutoka Burundi huingia na kuishi upande
wa Tanzania bila kufuata sheria na taratibu za uhamiaji.
Mkuu huyo wa Wilaya aliieleza kamati
maalum kwamba, kwenye uimarishaji wa mpaka huo uliofanyika mwaka 2014, baadhi
ya wanachi wa vijiji vya mpakani walijikuta wakipoteza baadhi ya mali zao kama
vile nyumba na mashamba baada ya maeneo hayo kuonekana yako upande wa Burundi
na siyo Tanzania.
Hiyo imekuwa ni changamoto kwa sababu wananchi hao tayari
walishakuwa na familia zao katika maeneo hayo na wengine hadi makaburi ya jamaa
zao yapo upande wa Burundi na wao wanaishi upande wa Tanzania.
Nae kiongozi wa msafara wa kamati hiyo
maalum Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ndugu Ramadhan
Kailima, aliipokea taarifa hiyo kuhusu hali halisi ya mpaka wa Tanzania na
Burundi na kuahidi kwamba kwa pamoja kama kamati maalum watakaa na kuona ni
jinsi gani wanaweza kuwasaidia wananchi walioathirika na uimarishaji mpaka
uliofanyika mwaka 2014 kwa maana ya wale ambao baadhi ya maeneo yao yalibaki
upande wa nchi jirani ya Burundi.
No comments:
Post a Comment