Saturday, December 21, 2019

OCODE YATOA ELIMU JUMUISHI KWA WALIMU NA WANAFUNZI NA WAZAZI MANISPAA YA UBUNGO


Meneja wa  Uwezo Tanzania  Zaida Mgalla akizungumza na washiriki hawapo pichani wa  mdahalo wa uwajibikaji wa pamoja katika kuleta elimu bora na jumuishi  katika manispaa ya Ubungo uliowashirikisha wazazi, walimu, wanafunzi, viongozi wa dini pamoja na viongozi mbali mbali wa serikali za mitaa pamoja na wadau wa maendeleo katika sekta ya elimu.
 ............................................

VICTOR MASANGU, DAR ES SALAAM.

KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini hususan kwa wanafunzi wa shule za msingi hasa kwa wale wenye mahitaji maalumu  Shirika la Organization for Community Development (OCODE) limeamua kuja na mpango wa kutoa mafunzo kwa walimu, wanafunzi na wazazi kuhusiana na umuhimu wa elimu bora na elimu  jumuishi pamoja na kujadili changamoto zilizopo ili kuzitafutia ufumbuzi.


Hayo yamebainishwa na  Afisa miradi kutoka shirika  hilo la OCODE Tunu Sanga wakati wa mdahalo wa uwajibikaji wa pamoja katika kuleta elimu bora na jumuishi lengo ikiwa ni kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi wanapata haki  yao ya upatikanaji wa elimu iliyo bora kwa ajili ya kuleta mabadilik chanya ya kimaendeleo katika siku zijazo.


Aidha alisema kwamba lengo kubwa la Shirika lao ni kushirkiana na wadau mbali mbali wa sekta ya elimu kukaa pamoja na kujadili mambo mbali mbali ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika mfumo mzima wa kuwa na elimu jumuishi na elimu iliyobora hasa katika makundi ya watu wenye ulemavu na wale wenye mahitaji maalumu.


“Tupo katika mdahalo huu ambao tumeamua kuuandaa  kwa kushirikiana na watu mbali mbali wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa serikali za mitaa, walimu, wazazi, pamoja na wanafunzi ili tuone ni namna gani tunaweza kufika mbali katika suala zima la kuwa na elimu jumuishi hivyo kwa sasa tupo katika manispaa ya ubungo na kwamba tutaendelea katika maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam,”alisema Sanga.


Kwa upande wake  Afisa elimu vifaa  na Takwimu katika Manispaa ya Ubungo  Brayson Maleko amebainisha kwamba kwa sasa kumekuwepo na matukio mbali mbali ya vitendo vya kikatili na unyanyasaji kwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi kulawitiwa  kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo wazazi na walezi kuwa na malezi mabaya kwa watoto wao.


Pia katika kupambana na hali hiyo kwa sasa Manispaa ya ubongo imeanzisha kampeni maalumu kwa ajili ya kupita katika kata zote 14 lengo ikiwani ni kutoa elimu pamoja na kukataa na kupinga kabisa vitendo vya mtoto wa kiume kulawitiwa kwani ni kinyume kabisa na sheria na taratibu za nchi zilizowekwa na kuwaasa wazazi kuhakikisha wanalisimaamia kwa pamoja suala hilo lisiweze kujitokeza tena.


“Ndugu mwandishi kwa sasa wanafunzi  wa kiume wapatao 12 katika shule moja ya  msingi  iliyopo katika  Manispaa ya Ubungo Jijini Dar e es Salaam  wamebainika kufanyiwa vitendo  vya ukatili ikiwemo  kulawitiwa na wazazi wao na wengine kulawitiana wenyewe kwa wenyewe kutokana na sababu  mbali mbali ya ukosefu wa elimu pamoja na malezi mabaya kutoka kwa wazazi wao na walezi,”alisema Maleko.


Kwa upande wake Meneja wa  Uwezo Tanzania  Zaida Mgalla  aliwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanawalinda na kuwatunza watoto wao ili waweze kujitambua na kuepukana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwataka walimu kuwa na nidhamu, huku  mmoja wa walimu walioshiriki katika Mdahalo  huo  Ambrose Mbwala  amesema kuwepo kwa  baadhi ya wanafunzi kufanyiwa  ulawiti vinatokana na tabia ya kushiriki mambo mabaya ya mitani ikiwemo, ngoma, utandawazi, pamoja na vigodoro vya usiku.


MDAHALO huo umewajumjisha wadau mbali mbali wa sekta ya elimu, viongozi wa dini, viongozi wa serikali za mitaa, wazazi, wanafunzi, pamoja na walimu kwa lengo la kuweza kuhakikisha elimu bora na elimu jumuishi katika ngazi za shule za msingi ili kuweza kuboresha sekta ya elimu  kwa kushirikiana na serikali ya awamu  ya tano.

Afisa elimu vifaa  na Takwimu katika Manispaa ya Ubungo  Brayson Maleko akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusina na mikakati ambayo wamejiwekea katika kusaidia na kuinua sekta ya elimu ikiwemo kuanzisha kampeni ya kuondoa vitendo vya ukatili kwa watoto wa mashuleni. 
Baadhi ya wakufunzi wa mdahalo huo wakiwa wanafuatili mdahalo ulioandaliwa na shirika la OCODE  kuhusiana na suala zima  la elimu jumuishi na elimu bora katika maeneo mbali mbali hususan kwa wanafunzi wa shule za msingi katika manispaa ya Ubungo. 
Mmoja wa walimu kutoka shule ya msingi Goba  iliyopo katika Manispaa ua Ubungo Ambrose Mbwala ambaye alishiriki katika mdahalo huo akitoa ufafanuzi juu ya changamoto ambazo zinapelekea baadhi ya wanafunzi kujiingiza katika mambo ambayo hayana faida kwa jamii.
 
Baadhi ya wanafuniz kutoka katika baadhi ya shule za msingi zilizopo katika manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaa wakiwa wanafuatilia mdahalo huo ambao umeandaliwa na shirika la OCODE kwa lengo la kujadili namna ya kushirikiana katika suala la elimu jumuishi na elimu bora 
Walimu kutoka shule tofauti za msingi wakiwa wanafuatilia mwenendo mzima wa mhadalo huo ukiendelea katika maeneo ya Kiluvya madukani wenye lengo la kujadili mambo yanayohusina na sekta ya elimu jumuishi hasa kwa watoto wa shule za msingi.
(PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU)

No comments:

Post a Comment