Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A.
Mwalimu (Mb) amepokea kwa masikitiko makubwa kitendo cha mwalimu mmoja wa Shule
ya Msingi Samanzi, iliyoko kijiji cha Samanzi, Kata ya Kisumba, wilaya ya
Kalambo mkoani Rukwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba (jina
limehifadhiwa), na kushindwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi. Mhe.
Waziri amesema kitendo hicho ni ukatili na unyanyasaji dhidi ya mtoto wa kike
na ni ukiukwaji wa Haki za Msingi za Mtoto ikiwemo haki ya Kuendelezwa na
Kulindwa.
Waziri Ummy amewaasa walimu kuacha tabia ya kuwa na mahusiano ya kingono
na wanafunzi maana shule kama taasisi, ni chombo madhubuti cha kujenga uelewa
kwa jamii kuhusu ulinzi na usalama wa Mtoto katika jamii.
Aidha, amewataka
walimu, walezi na jamii kuhakikisha wajibu wa kuwalinda na kuwalea watoto
bila uwanyanyasaji na ukatili wa aina yoyote. Ameongeza kuwa, inapotokea mwalimu
amehusishwa na tuhuma ya kumpa mimba mtoto wa kike kitendo hicho kinatia doa
dhamana ya mwalimu na nafasi ya shule katika malezi ya mtoto.
Waziri Ummy, ameitaka jamii kuboresha ushirikiano wa wazazi, walezi na
walimu maana wanamchango mkubwa katika makuzi na maendeleo ya watoto.
Kadhalika, amesisitiza kutambua kuwa madhara ya mwalimu kumpa mimba mwanafunzi
anamfanya kuwa mwathirika wa vitendo vya ukatili katika maisha yake yote.
Aidha, Waziri Ummy ameelekeza vyombo vya dola mkoani Rukwa kuhakikisha
suala hili linachunguzwa kikamilifu na kumfikisha mtuhumiwa mbele ya vyombo vya
sheria ili haki iweze kutendeka.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
22/09/2017
No comments:
Post a Comment