Friday, September 22, 2017

RUKIA MASENGA MWENYEKITI MPYA UWT BAGAMOYO.

IMG_20170921_111716
Na Mwamvua Mwinyi ,Bagamoyo

ALIYECHAGULIWA kuwa mwenyekiti mpya wa umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi Ccm (UWT)wilayani Bagamoyo ,Rukia Masenga ,amewataka wanawake wanaounda umoja huo kuwa wamoja na kuacha makundi ili kuinua maendeleo yao.

Aidha amesema amepewa dhamana kubwa ,na kuwa na deni ambalo anapaswa kuwalipa wanawake wa UWT wilayani hapo hivyo anaomba ushirikiano kwani hakuna kiongozi anaesimama peke bila kushirikiana.

Akishukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT wilayani hapo ,mara baada ya kuchaguliwa kuongoza nafasi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo ,Rukia alieleza wakati wa uchaguzi umepita kilichobaki ni kutekeleza yaliyo mbele yao kimaendeleo.

Alisema ,kulikuwa na makundi na kila mjumbe alikuwa na mgombea wake lakini mshindi kishapatikana hivyo hakuna haja ya upambe wala makundi yasiyo na tija.

Rukia ,aliwashukuru wajumbe wote kijumla waliomchagua na wasiomchagua .
Mwenyekiti huyo ,alisema amejipanga kuinua maendeleo ya akinamama wa Chalinze na Bagamoyo na kuahidi kuwarejesha kwenye umoja .

“Tunatakiwa kuwa wamoja ,kipindi cha mpito kimekwisha ,tuungane pamoja na tusonge mbele.” alisisitiza Rukia.

Nae aliyekuwa mgombea katika nafasi hiyo ,ambae walikuwa kwenye mchuano mkali ,Sinasudi Onelo alisema ameridhika na matokeo yaliyotangazwa.
Alisema hana kinyongo ,na alimuomba mwenyekiti huyo kushirikiana nae pale atakapohitaji .

“Ukimsifia aliyeshinda ,mumsifie na aliyemkimbiza ,kura zangu hazikutosha ,nachoomba wapambe nuksi tuondoe upambe ,uchaguzi umepita tusonge mbele.” alisema Sinasudi.

Awali akitangaza matokeo ,msimamizi wa uchaguzi huo wilayani Bagamoyo ,uliofanyika Msata ,ambae pia ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT Mkoani Pwani ,Mary Luilo ,alimtangaza Rukia Masenga kuwa mwenyekiti mpya wa UWT Bagamoyo .

Mjumbe wa mkutano mkuu UWT Taifa ni Hafsa Kilingo ,mjumbe wa mkutano mkuu CCM wilaya Blandina Sembu ,mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM kutoka UWT Ummy Kisebengo .

Wengine ni mjumbe kuwakilisha vijana amechaguliwa Maua Jinga ,na wajumbe wa baraza la UWT wilaya ni Sijali Mpwimbwi,Mwanakesi Madega ,Rehema Mwene ,Mwanaisha Kikwete ,Mwanaharusi Jarufu ,na Nancy Mtalemwa.
Mary alisema ,uchaguzi ulikuwa ni wa uhuru ,uwazi ,haki na umefuata demokrasia na hakukuwa na viashiria vya rushwa .

No comments:

Post a Comment