Wadau mbalimbali pamoja na wananchi wilayani
Bagamoyo wametakiwa kujitokeza kuchangia damu salama katika Hospitali ya Wilaya
ya Bagamoyo, ili kukabiliana na upungufu wa damu hospitalini hapo.
Wito huo umetolewa na Kamiu Muuguzi Mfawidhi
Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Saufa Khalifa, alipokuwa akizungumza mara
baada ya kamati ya Amanai wilayani Bagamoyo kutembelea Hospitalini hapo.
Saufa alisema kwa sasa Hospitali hiyo inakabiliwa
na upungufu wa damu, hivyo ni vyema wananchi wakajitokeza kuchangia damu ili
kuiwezesha Hospitali hiyo kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa wanaofika hospitali
hapo.
Alisema wanamshukuru Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo,
Alhaji, Majid mwanga kwa kutafuta wafadhili ambao ni Taasisi ya Kiislamu
ya Dhi Nureyn inayojenga jengo la wodi ya wazazi na jengo la
wagonjwa wa dharula na kuongeza kuwa, jengo la huduma ya dharula linahitaji
uwepo wa damu kwa wingi ili hata kama wanaletwa wagonjwa wa ajali ambao
wametokwa na damu nyingi waweze kuwekewa damu haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wao viongozi wa kamati ya Amani wilayani
Bagamoyo, ambao wamefika Hospitalini hapo wamesema watashirikiana na serikali
katika kuhamasisha wananchi kuchangia damu salama.
Walisema kazi ya kamati ya amani ambayo inaundwa
na dini zote ni kuwajenga waumini wao kiroho na kuweza kujitolea katika
shughuli za kijamii na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwaletea
maendeleo wananchi wake.
Kamati ya Amani wilayani Bagamoyo imefanya ziara
katika Hospitali ya Bagamoyo kwa lengo la kuangalia wagonjwa na kuwaombea duwa
pamoja na kukagua majengo yanayoendelea kujengwa Hospitali yanayojengwa na Taasisi
ya Kiislamu ya Dhi Nureyn ya Mjini Iringa.
Kamiu Muuguzi Mfawidhi
Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Saufa Khalifa,akitoa maelezo kwa kamati ya Amani ya wilaya ya Bagamoyo iliyofika Hospitalini hapo.
No comments:
Post a Comment