Tuesday, September 26, 2017

MWAKYEMBE ATAKA MKANDARASI MPYA WAKUTOA TIKETI UWANJA WA TAIFA.

PICHA 1
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama) akisalimiana na baadhi ya Viongozi wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda Mtwara wakati alipofanya ziara kujionea changamoto katika uwanja huo 25 Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.
PICHA 2
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama) akiongea na baadhi ya Viongozi wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda Mtwara wakati alipofanya ziara kujionea changamoto katika uwanja huo 25 Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.
 PICHA 3
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama) akiangalia eneo la uwanja wa mpira wa miguu akiwa na baadhi ya Viongozi wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda Mtwara wakati alipofanya ziara kujionea changamoto katika uwanja huo 25 Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.

 PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM
 .................................................

Na Benedict Liwenga-WHUSM.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kwamba pindi Uwanja wa Taifa Dar es Salaam utakapokamilia kufanyiwa ukarabati atahakikisha anapatikana Mkandarasi Mpya mwenye vigezo na ambaye ataleta mabadiliko hususani katika utoaji tiketi kulingana na namba za viti vilivyopo ndani ya Uwanja huo.

Kauli hiyo ameitoa jana Mkoani Mtwara wakati alipotembelea Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Nangwanda ili kujionea miundombinu ya uwanja huo ikiwemo baadhi ya changamoto zinazoikabili kiwanja hicho.

Dkt. Mwakyembe ameeleza kwamba, kumekuwa na changamoto ya kutofahamika idadi kamili ya watu wanaoingia ndani ya uwanja hali inayopelekea watu kukaa ovyo katika sehemu zisizo rasmi na wengine kulundikana nje ya uwanja wakati pesa za viingilio wamelipia ambapo ameweka wazi kuwa hali hiyo inasababishwa na urataibu mbovu wa utoaji tiketi.

Akiongea na Uongozi wa Uwanja huo wa Nangwanda Mkoani hapo alisema kwamba, kwakuwa sasa Uwanja wa Taifa uko katika ukarabati, pindi utakapokamilika Mkandarasi mpya lazima apatikane ili pindi mtu anunuapo tiketi yake iendane na kiti chake atakachokaa na sio vinginevyo kwakuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kuboresha sura za viwanja nchini.

“Napenda kusisitiza suala hili kuwa, ntahitaji apatikane Mkandarasi atakaetoa tiketi kulingana na siti atakayokaa mtazamaji wa mpira, kwasababu kumekuwa na kero kubwa katika utoaji tiketi hapo mwanzo jambo ambalo halileti sura nzuri kwa jamii”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Aliongeza kuwa Watanzania hawanabudi kuiga mifano ya nchi nyingine ambazo zimejidhatiti katika masuala ya utoaji tiketi wakati wa michezo.

Sambamba na hayo, Waziri Mwakyembe ameupongeza uongozi wa uwanja huo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuutunza uwanja wa Nangwanda huku akiaihidi kuzifikisha changamoto za uwanja huo katika Viongozi wa Juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ili waweze kushirikiana kwa pamoja kuona namna ya kuzitatua.

Uwanja wa Nagwanda ulianzishwa miaka ya 1980 ambapo awali ulikuwa ukiitwa jina la Uwanja wa Umoja Mtwara na baadaye kupewa jina la Uwanja wa Nagwanda lililotokana na jina la mtu maarufu wakati huo.

No comments:

Post a Comment