Monday, September 18, 2017

RC NDIKILO AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUKEMEA MADAWA YA KULEVYA.

Mkuu wa mkoa wa pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka viongozi wa dini mkoani humo kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kupambana na Madawa ya kulevya.

Mkuu huyo wa mkoa wa Pwani ameyasema hayo katika hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Ahaj, Majid Mwanga wakati wa Kongamano la mahusiano ya kibinadamu liliandaliwa na Kituo cha kiislamu cha Kimisri -Dar es salaam.

Amesema Madawa ya kulevya yanapoteza kuvu kazi ya Taifa na hivyo mmoja anapaswa kupiga vita biashara hiyo haramu ili mkoa uwe na watu wenye nguvu watakaoweza kusaidia uzalishaji kwenye viwanda vinavyoendelea kujengwa mkoani humo ili kufanikisha malengo ya Rais Magufuli ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wazazi kuwapeleka sekondari watoto waote watakaofaulu elimu ya msingi ili kila mtoto apate haki yake ya Elimu katika kipindi hiki ambapo Elimu inatolewa bure hapa nchini.

Akizungumzia swala usalama katika mkoa wa Pwani, mkuu huyo wa mkoa wa Pwani alisema Mkoa huo kwa sasa umekuwa tulivu baada ya vikosi vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi mkoani humo na kuwataka Viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani ili kuwavutia wawekezaji kufika katika Mkoa wa Pwani kuwekeza zaidi.

Alisema Kwa sasa mkoa wa Pwani una viwanda vingi na ni mkoa wa Mfano kwa Viwanda hapa nchini, hivyo ni vyema Amani ikaendelea kudumishwa ili wawekezaji hao waliojenga na wanaoendelea kujenga Viwanda waweze kufanya shughuli zao kwa utulivu na nchi ifaidike na kodi huku wananchi nao wafaidike kwa kupata ajira na bidhaa zinazozalishwa katika viwanda hivyo.

Nae Mkurugenzi wa kituo cha Kiislamu cha Kimisri ,Sheikh Muhsin Sayyed Majid alisema uislamu ni dini inayoendana na maumbile ya binadamu na hivyo mafundisho ya uislamu yanahimiza kuwa na mahusiano mema na watu wa dini zote bila ya kubaguana kwa rangi, kabila wala kwa lugha.

Alisema mafundisho ya mtume muhammadi Swalallaahu Alayhi wasalama yanafundisho mahusiano mema kwa watu wote na kwamba si vyema watu fulani wakajiona bora dhidi ya wengine ispokuwa mbora ni yule anae mcha mungu tu.

Kwa upande wake Sheikha mkuu wa mkoa wa pwani, Sheikh  Khamisi Abasi Mtupa amesema uislamu haumzuii mtu kushiriki katika shughuli mbalimbali ili mradi shughuli hizo hazimtoi kwenye uislamu kwa mujibu wa sheria.  


Washiriki wa kongamano hilo.
  Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Ahaj, Majid Mwanga akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi wa kituo cha Kiislamu cha kimisri,Dar es Salaam Sheikh Muhsin Sayyed Majid, kushoto ni Qadhi wa Mkoa wa Pwani, Sheikh Khamisi Abasi Mtupa

No comments:

Post a Comment