Tuesday, September 19, 2017

DC BAGAMOYO AKIWA SHAMBANI KWAKE AHIMIZA KILIMO CHA UBUNIFU.



Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga, amewahimiza wananchi wa wilaya  hiyo, kulima kilimo cha ubunifu ili kujiongezea kipato.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Bagamoyo, aliyasema hayo hivi karibuni baada ya bagamoyokwanza blog kutembelea shambani kwake lililopo kata ya Kiromo wilayani humo.

Alisema, kilimo bora kitakachomuongezea kipato mtu ni kile kinachoendana na soko la zao husika.

Aliongeza kwa kusema kuwa, katika Wilaya ya Bagamoyo kuna viwanda kadhaa vya kusindika matunda, mbogamboga na viungo mbalimbali ambavyo vyote ni mazao yanayotokana na kilimo.

Majid alisema sio mwananchi ataweza kuajiriwa katika viwanda hivyo, bali kila mwananchi atafaidika kwa namna yake ikiwemo wale watakaoshughulika na kilimo cha mazao yanayohitajika kwenye viwanda hivyo.

Akitolea mfano wa Kiwanda cha viungo cha VEGETA kilichopo kata ya Kisutu wilayani Bagamoyo, mkuu huyo wa wilaya alisema kiwanda cha VEGETA kinatumia mazao ya kilimo ikiwemo, Pilipili, Nyanya NK. hivyo ni vyema wakulima wa Bagamoyo wakafanya utafiti kuhusu mazao yanayohitajika kwenye viwanda vilivypo ili walime mazao ambayo yakivunwa yanaenda sokoni moja kwa moja.

Mbali na kiwanda cha VEGETA Mkuu huyo wa wilaya amekitaja Kiwanda kingine cha Elvin kilichopo Kata ya Mapinga katika Halmashauri ya Bagamoyo, ambacho ni maalum kwa kukausha matunda ambayo yatasafirishwa nje ya nchi.

Alisema kuwa, kiwanda hicho cha Elvin ni kiwanda pia kitakachohitaji matunda ya aina mbalimbali kwa wingi ili kuweza kuzalisha bidhaa za matunda yaliyokaushwa na hivyo ni fursa kwa wakulima kutumia ubunifu wa kulima mazao ambayo tayari masoko yake yapo.

Aidha, alisema, mbali na hivyo kipo kiwanda cha Sayona Kata ya Msoga Halmashauri ya Chalinze ndani ya Wilaya ya Bagamoyo ambacho hicho ni kwaajili ya kutengeneza juisi za matunda na kwamba katika kiwanda hicho soko kubwa la matunda litapatikana hivyo ni vyema wananchi wa wilaya ya Bagamoyo wakachangamkia fursa hizo kilimo cha ubunifu kulingana na soko la zao husika ili kujiongezea kipato.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga, pamoja na majukumu yake aliyonayo ya kuingoza wilaya, hutmia muda wake wa ziada shambani, ikiwa ni sehemu ya kuonesha mfano wa kile anachokisema ambapo ameweza kupanda Migomba, Mipapai Pilipili, Ufugaji wa Samaki na Kuku wa Kienyeji.

Harakati hizi za shamba za mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, licha ya kuwa anaweza kujiongezea kipato kutokana na mazao yaliyopo shambani kwake, lakini pia ameweza kutoa ajira kwa vijana wanaofanya kazi za kuhudumia mazao hayo hapo shambani.

Ni Mfano wa Kuigwa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, majid Hemed Mwanga, mimi na wewe tufuate njia.

    Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, majid mwanga akionesha zao la pilipili ambazo amepanda shambani kwake eneo la Kiromo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, majid mwanga akiwa kwenye shamba lake la Migomba Kiromo wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, majid mwanga akionesha aina ya Mpapai ambao huzaa kwa muda mfupi katika shamba lake huko Kiromo ndani ya Wilaya yake.
Mkurugenzi wa bagamoyokwanza blog. Brother, Athumani Shomari (kulia) alipotembele shambani kwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, (kushoto) Alhaj Majid mwanga.

No comments:

Post a Comment