Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali akizungumza na waandoshi wa
habari kuhufu kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi leo Jijini Dar es Salaam.
Gazeti hilo limefungiwa kwa muda wa miezi 24 kutokana na kukiuka maadili ya
uandishi wa habari mara kwa mara bila kujirekebisha. Kushoto ni Mkurugenzi
Msaidizi Sehemu ya Usajili Bw. Patrick Kipangula.
Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali akizungumza na waandishi wa
habari kuhufu kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi leo Jijini Dar es Salaam.
Gazeti hilo limefungiwa kwa muda wa miezi 24 kutokana na kukiuka maadili ya
uandishi wa habari mara kwa mara bila kujirekebisha. Kulia ni Mkurugenzi
Msaidizi Sehemu ya Huduma za Habari na Picha Bw. Rodney Thadeus na Mkurugenzi
Msaidizi Sehemu ya Usajili Bw. Patrick Kipangula.
................................
Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa
gazeti la kila wiki la MWANAHALISI kwa kipindi cha miezi ishirini na
minne (24) kuanzia leo kufuatia mfululizo wa gazeti hilo kukiuka maadili,
misingi na sheria za taaluma ya uandishi wa habari, kuandika habari za uongo,
uchochezi na kuhatarisha usalama wa Taifa.
Zuio hili pia linahusu toleo la
mtandaoni la gazeti hili.
Uamuzi huo umechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 59
cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016 ikiwa ni baada ya jitihada za muda
mrefu za Serikali kupitia Idara ya Habari-MAELEZO kuwakumbusha wahariri wa
gazeti hili juu ya wajibu wa kufuata misingi ya taaluma bila mafanikio.
Miongoni mwa habari zilizokiuka maadili, uchochezi
na/au kusababisha hatari kwa usalama wa Taifa na hatua zilizochukuliwa
lakini uongozi wa gazeti hilo haukutaka kujirekebisha zinaanishwa hapa:
1.
Katika gazeti
la tarehe 30 Januari- 5 Februari, 2017 MWANAHALISI liliandika habari
iliyosomeka “Ufisadi ndani ya Ofisi ya JPM.” Habari hii ilisheheni nia ovu
dhidi ya Rais wakati suala husika lilihusu Shirika la Elimu Kibaha! Wahariri
walikiri udhaifu huo, wakaomba radhi, na kupewa ONYO KALI;
2.
Katika gazeti
la tarehe 17 -23 Aprili, 2017 toleo Na. 387 kulikuwa na habari iliyosomeka
“Mwakyembe: Maisha yangu yako hatarini” Habari hiyo ilikuwa ya kutunga. MWANAHALISI
lilipewa KARIPIO KALI na liliomba radhi katika gazeti toleo Na. 389 la tarehe
1-7 Mei, 2017. Waliahidi hata kumchukulia hatua za kiutawala mwandishi wao
aliyetunga uongo.
3.
Katika gazeti
la tarehe 4-10 Septemba, 2017 toleo Na 407 liliandika tena habari iliyosomeka
“Makinikia yakwama” ambayo haikuwa na ukweli wowote na ilikuwa na nia ovu ya kuuaminisha
umma kuwa mazungumzo hayo yamekwama na kubeza juhudi za Serikali katika
kupigania wananchi kufaidika na raslimali za madini. Licha ya kuelezwa sana
kuhusu udhaifu wa habari hiyo uongozi wa MWANAHALISI ULIKATAA KUOMBA RADHI;
4.
Aidha katika
gazeti Na. 407 la tarehe 4-10 Septemba, 2017 ilichapishwa makala iliyosomeka ‘Mkuu
wa Wilaya ya Karagwe anachafua kazi ya Magufuli’ na kumtuhumu kuwa kiongozi
huyo anavunja sheria za nchi bila kutimiza wajibu wa kumpa mtuhumiwa nafasi ya
kusikilizwa kabla ya kuichapisha habari hiyo. Juhudi za kuwataka wasahihishe
kasoro hiyo kubwa katika maadili ya uandishi kupitia toleo la Jumatatu Septemba
18, 2017 zilipuuzwa na wahariri wa MWANAHALISI;
5.
Pia katika
Gazeti la Na. 409 la tarehe 18-24 Septemba, 2017 wahariri waliruhusu
kuchapishwa makala iliyosomeka “Tumwombee Magufuli au Tundu Lissu” ikiokoteza
kejeli za mitandaoni na uchochezi wa aina mbalimbali dhidi ya Rais na Serikali.
Walipotakiwa kujitetea walisema tu eti habari hiyo ilichukuliwa kwa kuwa
ilishachapishwa mitandaoni. Serikali imeona utetezi huu ni dhaifu kwa kuwa
habari lazima izingatie maadili.
Ni kwa sababu hizi basi Serikali imeona kuwa
wahariri wa gazeti la MWANAHALISI na uongozi mzima wa gazeti hilo hawako
tayari kufuata maadili ya taaluma hii na wanastahili kwa mara nyingine tena
kupewa muda wakatafakari zaidi kama bado wanaona ipo haja kuendelea na kazi hii
au la.
Kufungiwa kwa gazeti hili ni juhudi ya mwisho ya Serikali kuwataka
wabadilike.
Natumia fursa hii kusisitiza tena, uandishi wa
habari ni taaluma kamili yenye haki (rights) na wajibu (responsibilities). Haki
muhimu za uandishi zimeainishwa katika kifungu cha 19(2) cha Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia, 1966 ambao Tanzania imeuridhia
tangu mwaka 1976 na kuingiza misingi hiyo katika sheria zake za nchi hasa
kifungu cha 7 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016.
Hata hivyo kifungu cha 19(3a-b) cha Mkataba huo
kinasisitiza kuwa pamoja na haki ya kusambaza na kuhariri habari, wanataaluma
ya habari wana wajibu adhimu unaosimama katika misingi minne (4): kutokashifu
watu wengine, kutoingilia faragha ya wengine, kutoathiri usalama wa Taifa na
ustawi wa jamii.
Wahariri wa MWANAHALISI walichagua kwa makusudi
kutotekeleza wajibu wao huu.
Serikali itaendelea kuisimamia vyema sekta ya habari
ili iendelee kutoa mchango wake kwa maendeleo ya Taifa na navipongeza vyombo
vya habari vinavyotimiza wajibu wao ipasavyo lakini ifahamike tena na
tena-hatutasita kuchukua hatua kali zaidi kwa wale wote wanaodhani uandishi wa
habari ni kuandika chochote na kuishia kukashifu watu na kufanya uchochezi.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu
wa Serikali.
No comments:
Post a Comment