Tume ya Vyuo vikuu Tanzania (TCU) imevifutia udahili vyuo 19 na kufuta
kozi 75 katika vyuo 22 kwa kukiuka Sheria taratibu na kanuni za utoaji wa
elimu ya juu hapa nchini.
Akitoa ufafanuzi kuhusu Taarifa hiyo Jijini Dar es Salaam Afisa habari wa Tume hiyo Bw. Edward Mkaku alisema
uamuzi wa kuvifutia udahili baadhi ya vyuo ni kutekeleza agizo la serikali
lililoitaka Tume hiyo kuvisimamia kwa karibu vyuo ili viweze kutoa elimu bora.
Bw.Makaku amesema kuwa kwa vyuo ambavyo wanafunzi wanaendelea na masomo
mabadiliko haya hayatawahusu wanatakiwa kuendelea na masomo kama kawaida, ila
vyuo hivyo haviruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwa mwaka huu wa masomo
2017/2018.
Alizitaja baadhi ya sababu zilizopelekea baadhi ya vyuo kufutiwa udahili
wa Shahada, Shahada za Uzamili pamoja na Shahada za Uzamivu kuwa ni kukosa
vitendeakazi na wataalam katika kufundisha elimu ya juu.
Aidha Mkaku amesema kuwa TCU imeandaa maonesho yatakayoanza Julai 26,
2017 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam,maalum kwaajili ya
kutoa elimu kwa wanafunzi wanaohitaji kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa
nchini, pia kuelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume hiyo.
Bw.Mkaku pia amesema baadhi ya vyuo vinavyotoa taaluma za afya kama
Kilimanjaro Chritiani medical College (KCMC) cha mkoani Kilimanjaro, Kampala
International University (KIU) cha Jijini Dar es Salaam pamoja na
Hubert Kairuki Memorial University (HKMU) pia cha Jijini Dar es
Salaam ambavyo vilikuwa vikitoa kozi za udaktari, ufamasia pamoja na shahada ya
uzamili katika Udaktari wa magonjwa ya kinamama iliyokuwa ikitolewa na Chuo cha
Hubert Kairuki imebainika kuwa hawakuwa na vifaa na wataalam wa kutosha
kufundisha kozi hizo.
Alivitaja vyuo vilivyofungiwa kutokana na kutokuwa na wataalam wa
kutosha kuendesha kozi zake kuwa ni, St. Joseph, St. John, Tumaini University
pamoja na vyuo vingine kadhaa ambavyo havina waalimu pamoja na vifaa kwa mujibu
wa maelekezo ya Tume hiyo.
Bw.Mkaku amebainisha kuwa katika vyuo 22 hapa nchni kuna zaidi ya kozi 75
ambazo hazitakiwi kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2017/2018 na
kuwashauri watahiniwa wanaotarajia kujiunga na mwaka huu wa masomo kuingia
katika tovuti rasmi za vyuo ili kujua kozi ambazo zinatakiwa na kozi ambazo
zimezuiliwa.
“Tulifanya uhakiki wa vyuo hapa nchni Septemba na oktoba 2016 na kubaini
baadhi ya vyuo kutokukidhi mahitaji ya watahiniwa katika baadhi ya kozi kwa
hiyo ni muhimu kutoa taarifa mapema kwa umma juu ya mchakato huu”
Alisema.
Katika kuondoa changamoto kwa watahiniwa wa miaka ijayo Mkaku amesema
kuwa maonesho ya vyuo yatakuwa yanafanyika kikanda ili kutoa elimu kwa umma
katika masuala mazima ya elimu ya juu.TCU ilikabidhi rasmi jukumu la udahili
kwa vyuo husika Julai 20,2017 ili waendeshe wenyewe na wao watabaki kuwa
wasimamizi wa Sheria na sera za vyuo vya elimu ya juu.
TCU wametoa onyo kwa vyuo vitakavyoendelea kudahili wanafunzi katika kozi
zilizofutwa kuwa ni kinyume cha Sheria na wakibainika watashitakiwa kwa mujibu
wa Sheria za nchi na zile za vyuo vikuu.
No comments:
Post a Comment