Thursday, July 27, 2017

RPC. PWANI APANIA KUWASAKA WAHALIFU.

IMG_20170724_131141
 KAMANDA wa polisi mkoani Pwani ,kamishna msaidizi wa polisi (ACP ) Jonathan Shanna ,amesema amejipanga kupambana na wahalifu mbalimbali kwa kuwasaka uvungu kwa uvungu.

Aidha amewataka wakulima na wafugaji kuheshimiana kwa lengo la kuondoa migogoro baina yao .

Mbali na hayo amewaonya madereva wa vyombo vya moto ikiwemo mabasi yaendayo mikoani na magari madogo kutii sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali za barabarani zinazotokea mara kwa mara barabara kuu ya Dar as salaam -Morogoro .

Akizungumza na baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi Mkoani Pwani pamoja na waandishi wa habari Mkoani hapo,kamanda Shanna ,aliomba ushirikiano kwa askari polisi,waandishi hao pamoja na jamii .

Shanna alieleza kwamba ,atakwenda kitanda kwa kitanda ,pori kwa pori kuhakikisha wanapunguza matukio ya kiuhalifu .

Alisema yeye ni mgeni lakini ni mtu wa kazi alitaka ushirikiano kwa askari wa jeshi hilo mkoani hapa na wananchi baada ya kuchukua nafasi ya kamishna msaidizi mwandamizi, Onesmo Lyanga aliyehamishiwa mkoa wa kipolisi Rufiji ambao utakuwa na wilaya za Rufiji, Mkuranga, Kibiti na Mafia .

 “Baada ya kugawanyika kwenye utoaji wa huduma za Kipolisi na sisi Mkoa wa Pwani kubaki na Wilaya za Kipolisi Chalinze na Mlandizi, na Wilaya za Kiserikali Bagamoyo, Kisarawe, na Kibaha”alisema kamanda Shanna.

Katika hatua nyingine ,Shanna alisema Mariamu Omari (31) mkazi wa Muharakani Kwamatias, wilaya ya Kibaha amefariki dunia baada ya kuuwawa na watu wasiojulikana  .

Alisema mwili wa mwanamke huyo ulikutwa nje ya nyumba anayoishi mbele kidogo umbali wa mita 40 akiwa anavuja damu nyingi sehemu za usoni na jereha kichwani upande wa kushoto.

Kamanda Shanna alieleza kufuatia tukio hilo jeshi la polisi mkoani Pwani linafanya uchunguzi wa kina kuhakikisha wanaweza kuwabaini waliojihusisha na tukio hilo .

Aliwataka wananchi watoe ushirikiano kwa kuwafichua wahalifu hao ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
IMG_20170724_124326
 Baadhi ya maofisa wa Polisi wakiwa katika mkutano huo.

No comments:

Post a Comment