Waziri
wa afya ,jinsia,wazee na watoto Ummy Mwalimu ,akitembelea kituo cha afya
Mlandizi ,wa kwanza kushoto ni mganga mfawidhi wa kituo cha afya
Mlandizi,dk.Mpola Tamambele,ambae amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi
....................
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WAZIRI wa
afya, jinsia ,wazee na watoto ,Ummy Mwalimu ,amemsimamisha kazi mganga mfawidhi
wa kituo cha afya Mlandizi,dk.Mpola Tamambele,kutokana na kushindwa kusimamia
maelekezo ya serikali ya kuhakikisha mama mjamzito ,mtoto chini ya miaka mitano
na mzee wanapata huduma bure .
Kutokana na kutokuwa na mamlaka ya moja kwa moja amemuagiza kaimu
mkurugenzi wa halmashauri ya halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Beda Mmbaga
kumsimamisha kazi mganga mfawidhi huyo mara moja wakati uchunguzi wa tuhuma
zinazomkabili zikiendelea .
Amemuelekeza kaimu mkurugenzi huyo pia kuwafuatilia watumishi wa afya
kituoni hapo waliohusika kumuagiza mama aliyejifungua Salma Khalifan kwenda
kununua vifaa vya kujifungulia vya sh.180,000 ili apate huduma .
Aliyasema hayo wakati alipokwenda kutembelea kituo cha afya Mlandizi
,kabla ya kukabidhiwa kwa magari ya wagonjwa matatu kutoka kwa mbunge wa jimbo
hilo ,Hamoud Jumaa .
Waziri huyo alisema yeye hana mamlaka ya moja kwa moja kumsimamisha kazi
mganga mfawidhi huyo hivyo anaiachia mamlaka husika isimamie jukumu hilo.
Alisema hatokubali kuona watumishi wachache kwenye vituo vya afya
,zahanati na hospitali wanachezea maagizo ya serikali.
Alifikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mama
aliyejifungua ambae alisema amenunua vifaa vya kufanyiwa operesheni kwa gharama
ya sh .180,000 .
Ummy alisema haiwezekani kuona mama wajawazito ,wanalipishwa hadi gloves
na pamba ili kujifungua wakati serikali yao ilishasema watahudumiwa bure .
Alieleza kwamba ,kuanzia sasa waganga wakuu wa wilaya ,mikoa na watumishi
wa afya wote nchini wahakikishe wanatimiza maelekezo ya serikali kuhudumia
akinamama wajawazito na watoto ili kupunguza vifo vya uzazi .
Ummy alisema kuwa ,watumishi na wauguzi wengi wanajituma na kufanya kazi
zao kifanisi ila wapo wachache ambao wanakwamisha juhudi hizo .
“Sitokubali mtumishi anakwenda kinyume na serikali ,rais wetu John
Magufuli anasisimamia suala zima la kuboresha huduma za afya ,halafu akitokea
mtu mmoja mzembe anatuchanganya kwakweli sitoweza kumfumbia macho “
“Wananchi wamekuwa waoga hata kuingia katika suala la bima ya afya kwa
sababu ya mambo kama haya ,namsimamisha mganga mfawidhi huyo hadi hapo
uchunguzi utakapokamilika .” alisema Ummy .
Mbali ya hayo Ummy alibainisha,bajeti ya dawa katika halmashauri ya
wilaya ya Kibaha imeongezeka ndani ya miaka miwili mfululizo kwenye
uongozi wa serikali ya awamu ya tano .
Ummy alisema mwaka 2015/2016 bajeti ya madawa katika halmashauri hiyo
ilikuwa mil.24 na 2017 ilifikia mil.70 na bajeti ya sasa 2017/2018 imefikia sh.
mil.101 .
Kwa upande wake mama aliyejifungua kituoni hapo ,Salma Khalfani
,alimweleza Ummy kwamba aliandikiwa orodha ya dawa za kununua kwenye maduka ya
dawa ya nje .
Alieleza ,alitakiwa kufanyiwa upasuaji na hivyo kutakiwa kununua madawa
na vifaaa tiba ,pamba na gloves vya 180,000 akanunue ili aweze kujifungua .
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Mmbaga alisema maagizo aliyopewa na
waziri ameyapokea na atayafanyia kazi .
Nae mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaaa alisema kumekuwa na
malalamiko mengi juu ya wananchi hasa akinamama kulipishwa fedha za dawa na
vifaa tiba .
Alisema baadhi ya wazee wamekuwa wakishindwa kupewa huduma za afya bila
malipo .
Jumaa alimuomba Ummy kuendelea kushirikiana nae kuwadhibiti watumishi
wazembe wanaodidimiza haki za wananchi .
No comments:
Post a Comment