Wednesday, July 26, 2017

MBUNGE WA KIBAHA VIJIJINI ATOA MAGARI YA WAGNJWA JIMBONI KWAKE.

SAM_4784
MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa akikabidhi magari matatu ya wagonjwa (ambulance) ambayo yatasaidia kubeba wagonjwa katika jimbo la Kibaha Vijijini.
 ...............
MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa amekabidhi magari matatu ya wagonjwa (ambulance )ambayo yatasaidia kupunguza adha ya usafiri kwa wagonjwa hasa mahututi na warufaa.

Kati ya magari hayo ,mawili yametokana na nguvu zake na moja ni msaada kutoka kwa Rais John Magufuli ikiwa ni kati ya magari ya wagonjwa 67 yaliyogawanywa katika maeneo mbalimbali nchini .

Aidha mbunge huyo ,ameiomba wizara ya afya kukipandisha hadhi kituo cha afya cha Mlandizi kuwa hospitali ya wilaya ombi ambalo waziri wa afya,jinsia ,wazee na watoto Ummy Mwalimu amekubali ombi hilo .

Jumaa aliyasema hayo ,viwanja vya shule ya msingi Mtongani ,Mlandizi wakati Ummy Mwalimu alipokwenda kukabidhi magari hayo kwa niaba yake kwa halmashauri na mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha.

Alieleza ,ameamua kujikita kutatua kero zinazowakabili kwa kwenda sambamba na kauli mbiu yake ya  SISI KWANZA SERIKALI BAADAE .
“Ninamshukuru waziri Ummy kwa dhati ya moyo wangu kwa jitihada zake za kupigania gari moja kuletwa Kibaha Vijijini ,”
“Ni bahati kwetu kwani zilikuwa ambulance 67 ambapo 50 zilielekezwa mikoa ya kanda ya ziwa ambako idadi ya vifo vya mama wajawazito ni kubwa hivyo zilibaki 17 hivyo moja wapo ndio hiyo imekuja kwetu ” alisema Jumaa .

Alibainisha kuwa ,magari hayo ni sehemu ya kupunguza tatizo la usafiri linalokabili vituo na zahanati jimboni hapo .

Alisema ,serikali iangalie uwezekano wa kuwaongezea magari ya wagonjwa katika maeneo ya mbali kama Kwala na Magindu .

Hata hivyo Jumaa akizungumzia ombi la kituo cha afya Mlandizi kupandishwa hadhi ,alisema anaendelea kufanya jitihada za kutimiza vigezo vinavyotakiwa kupandishwa hadhi ikiwemo kujenga uzio .

Alimshukuru makamu wa rais kwa harakati zake za kuhakikisha juhudi hizo zinazaa matunda kwa kuwachangia mifuko ya saruji 500 ,waziri mkuu nae alichangia mifuko hiyo 150 .

Wadau wengine wamechangia kokoto tani 7 kwa sh. mil. 9.1, mchanga mil. 2.4 tofali sh. mil 8.4, nondo tani moja sh. mil. 3.6 na fedha zake mwenyewe na hadi sasa zimeshatumia sh .milioni 50 .

Jumaa aliwaomba wadau wa afya na serikali kuendelea kumuunga mkono ili tatizo hilo libakie historia.

Alichukua fursa hiyo pia ,kukabidhi vitanda 25 na mashuka 50 vilivyotolewa na Rais katika majimbo mbalimbali nchini .

Katika vitanda hivyo 20 ni vya kawaida na vitanda vitano ni kwa ajili ya kujifungulia .

Akikabidhi magari hayo ya wagonjwa ,waziri wa afya ,jinsia ,wazee na watototo Ummy alisema atachangia mifuko ya saruji 100 ili kuunga mkono ujenzi wa uzio.

“Nampongeza Jumaa na mmepata mbunge anaejua kujiongeza ,mtumieni ,mtieni nguvu kwa mambo anayowapigania ” alisema Ummy .

Alisema kutoka na ahadi walizowahi kutoa wakubwa wake kupandisha hadhi kituo hicho cha afya na kwa kuwa ni wakubwa wake amekubali ombi hilo .

Ummy alisema pia kuna fedha anaitegemea ambayo atawezesha kujenga wodi ya uzazi yenye sehemu mbili na maabara ya damu kwa lengo la kuboresha huduma za afya .

“Vigezo vikikamilika kwa namna hiii ,idadi ya watu wanaohudumiwa ,uzio ,idadi ya majengo na mengineyo naamini tutapata hospital ya wilaya iliyo nzuri na iliyokamilika ” alifafanua Ummy .

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Mansoor Kisebengo ,alisema watahakikisha wananchi hawagharamii mafuta kwa magari hayo .

Kisebengo alisema ,halmashauri hiyo itakuwa inachangia gharama za mahitaji ya mafuta ili kuondoa bugudha kwa wananchi .
SAM_4781

No comments:

Post a Comment