Baadhi
ya Wadadisi wakielekezwa namna ya kutumia ramani wakati wa kufanya mazoezi ya
kuorozesha kaya kwa vitendo na Mtalaam wa Ramani Jumanne Msuya wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (katikati) kwa ajili ya maandalizi ya Utafiti wa Mapato na
Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18. Zoezi hilo la
uorozeshaji kaya litafanyika kwa muda wa siku kumi na tano (15) kuanzia kesho
tarehe 11 Julai, 2017.
...........................
WADADISI wa Utafiti wa Mapato
na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 wameaswa kuzingatia
maadili ya kazi wakati wa zoezi la kuorodhesha kaya linalotarajia kuanza kesho
ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utafiti huo.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika jijini Dar es
Salaam kwa wadadisi hao, Meneja wa Takwimu za Jamii na Watu, Sylvia Meku kutoka
Ofisi ya Taifa ya Takwimu amesema ili kufanikisha zoezi la uorodheshaji wa
kaya, ni lazima wadadisi hao wakazingatia maadili ya kazi pamoja na kufuata
taratibu zote za Utumishi wa Umma.
“Ofisi ya Taifa ya Takwimu inawaagiza kwenda kwenye jamii kwa ajili ya
kuorodhesha kaya zitakazofanyiwa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi
Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18. Natumaini mtatii na kuheshimu maadili ya
Utumishi wa Umma ili muweze kufanikisha kazi hii kwa ufanisi,” amesema Slyvia
Meku.
Amesema Zoezi la Uorodheshaji wa Kaya litafanyika mikoa yote ya Tanzania
Bara kwa takribani siku 15 kuanzia kesho Julai 11, 2017 na baadae kufuatiwa na
utafiti wenyewe unaotarajia kuanza mwezi Desemba, 2017.
Sylvia Meku amesema utafiti huu unafanywa na Ofisi
ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na baadhi ya
Wadau wa Maendeleo kwa lengo la kuangalia kiwango cha umasikini nchini.
No comments:
Post a Comment