Saturday, July 22, 2017

LUKUVI AWAONYA MAAFISA ARDHI.

1
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwaonya maafisa ardhi na maafisa mipango miji wasio waadilifu na kusababisha kero za migogoro ya ardhi nchini wakati wa uzinduzi Master Plan ya mji wa Iringa.
.........................................

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amewaonya maafisa ardhi na maafisa mipango miji wasio waadilifu na kusababisha kero za migogoro ya ardhi nchini.

Waziri  Lukuvi  aliyasema  hayo leo  katika ukumbi wa shule  ya sekondari  Lugalo mjini  Iringa  wakati  wa  Uzinduzi wa Master  Plan ya  Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa.

Amesema mchezo huo wa ufisadi ambao umekuwa ukitumiwa  miaka  yote na maofisa ardhi nchini ameubaini na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutokubaliana na ramani za maeneo mapya zinazoletwa na wataalam  hao bila ya wao kufika maeneo husika na kuoneshwa maeneo hayo ili kujiridhisha.

Waziri Lukuvi amefichua kuwa ufisadi unaofanywa na maafisa ardhi nchini kwa kupima viwanja  hewa kwa  ajili ya maslahi yao na kusema kuwa mbinu ambayo  wamekuwa  wakiitumia  kuiibia  serikali amekwisha  ibaini na  hata kubali  kuona mbinu  hiyo inapewa nafasi katika serikali  hii ya awamu ya  tano chini ya  Rais Dkt John Pombe Magufuli .

Maafisa ardhi wakishirikiana na maafisa mipango miji pamoja na wapima wamekuwa  wakitajirika  sana kwenye idara  zao na  wanatakata kwa  ujanjaujanja  na  ufisadi   wanaoufanya kwa kutengeneza ramani zinazoonesha maeneo mazuri na muhimu katika miji kwamba hayafai kutumika, kumbe wameyauza maeneo hayo kwa mlango wa nyuma na kwa bei za juu.

Unakuta kwenye ramani  inayonyesha  kuna bonde  kubwa  lisilofaa kujengwa  kumbe ukifuatilia  eneo hilo  ni  zuri  kuliko  yote na hapo  wametenga  viwanja  vya kuuza. Unakuta  ukipima  kuna  viwanja vingi na vizuri ambavyo ni vyao  wao   wanachofanya baada ya  kuuza  viwanja  halali za Halmashauri hurudi  kupima maeneo hayo walioonyesha ni mabonde na kugawana  wao kwa ajili ya kuuza kwa  faida  yao.

Lukuvi  amesema  kuwa wathamini  nao pi wamekuwa  wakiwapunja  wananchi  wasio elewa kwa  kuwafanyia  tathimini   kubwa  zaidi  ya uhalisia wake na  pindi pesa  inapotoka utakuta nyumba inathamani ya milioni 7 wakati wao wanasema inathamani ya milioni 20 ili cha juu wapate wao.

“wakati nilipokuwa Mkuu wa  Mkoa wa Dar es salaam niliweza  kubaini  ujanja wa wathamini baada ya  eneo ambalo nyumba  zake zina thamani kati ya  milioni 20 hadi 50  kwa maana  nyumba hizo ni za udongo  ila maofisa  hao  walimtafuta  mtu  na kutafuta nyumba  nzuri zaidi na kumshikisha  kibao  kisha kumpiga  picha na  kuandika kuwa  nyumba  hiyo inathamani ya  zaidi ya  milioni 200.

Niliamua kufanya uchunguzi wangu na kumtafuta mtu aliyekwenye picha na kumbana ndipo aliniambia ukweli kuwa mthamini huyo ni ndugu yake  hivyo walikubaliana pesa ikitoka atalipwa  milioni 70 na milioni 130 ni za afisa huyo”
Hata hivyo alisema kuwa ujenzi holela katika miji na halmashauri imesababishwa na ukilitimba wa utoaji wa vibali kwa wakati na ndio  sababu ya  wananchi  kuvamia maeneo yasiyo pimwa japo kuanzia sasa  wote  waliopo katika maeneo yasiyo pimwa  watapewa leseni ya makazi ya  miaka  mitano na watalipa  kodi ya ardhi na baada ya miaka mitano wahakikishe  wamepimiwa  ili  kupewa hati.

Hivyo  Lukuvi  aliwataka  maafisa ardhi na wathamini wa ardhi manispaa ya Iringa kutofanya kama maeneo mengine kwa kufuata mpango maeneo  yote ambayo yameelekezwa  kwenye Masta Plan hiyo na kwenda  kutenda haki.

Katika hatua  nyingine  waziri  Lukuvi  alitoa  agizo kwa  wale wote  waliopewa ardhi kwa ajili ya  ujenzi wa hoteli na  viwanda na wale waliouziwa viwanda  vya serikali, hotel na mashamba ya  serikali  kuviendeleza haraka kabla ya  ardhi hiyo haijapokonywa.

Nae Mkuu  wa  Mkoa  wa Iringa Bibi  Amina Masenza  akimkaribisha  waziri Lukuvi  amesema kuwa mkoa  wa Iringa  umeendelea  kuhamasisha  wananchi  kuzingatia  sheria  na taratibu za ujenzi na kuachana na ujenzi  holela na ndio  sababu ya  kuja na Masta Plan hiyo ambayo  imeanzishwa na aliyekuwa mstahiki meya wa halmashauri hiyo Amani Mwamwindi.

Akitoa taarifa ya uandaaji wa Masta Plan hiyo kwa ajili ya mwaka 2015-2035 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Dkt William Mafwere, alisema kuwa dhumuni la mpango huo ni kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili Manispaa na kuwa dhana kuu ya mpango huo ni dhana unganishi ikijumuisha dhana nyingine.

Alisema jumla ya miradi 31 itatekelezwa katika awamu ya kwanza 2015-2020 kuwa baadhi ya miradi hiyo ni kituo cha mabasi Igumbilo, kituo hicho kimeanza ujenzi na hatua ya utekelezaji imefikia asilimia 30.

Nae Mbunge wa jimbo la  Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa alisema  kuwa kazi inayofanywa na  Waziri  Lukuvi ni tofauti na mawaziri  wengine kwani amekuwa ni waziri wa mfano katika  kuchapa kazi.

“Kwa  mnaonifahamu  vizuri  mimi sio mbunge wa kusifia  sifia ni mbunge  mwenye msimamo ila nampongeza  sana Waziri Lukuvi ni  waziri  mchapakazi na kazi zake zinaonekana na ndio maana  hata  bungeni ni waziri pekee ambaye bajeti yake ilipitishwa kwa kishindo  hata na  sisi  wabunge wa kambi ya upinzani”
Mpango Kabambe ni chombo cha kuchochea utumiaji wa fursa zilizopo katika mji,  kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali  za kiuchumi na kijamii na kupunguza na kumaliza migogoro ya ardhi. kudhibiti ujenzi holela mijini na hutumika pia kuongoza, kusimamia na kudhibiti ukuaji na uendelezaji wa mji na kutoa uhakika kwa wawekezaji katika Halmashauri za Manispaa ya husika.


Hassan Mabuye Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ardhi

No comments:

Post a Comment