Thursday, October 21, 2021

SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMEJIKITA KATIKA MISINGI YA HAKI ILI KILA MTANZANIA APATE HUDUMA STAHIKI KATIKA TAASISI ZA UMMA

 No description available.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na waumini wa dini ya kiislam wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

...........................................

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan imejikita katika misingi ya utoaji haki ili kumuwezesha kila Mtanzania kupata huduma bora zinazotolewa na Taasisi za Umma nchini. 

Mhe. Mchengerwa amesema hayo jana usiku jijini Dar es Salaam, wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kwenye Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S. A. W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mchengerwa amesema, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan anasisitiza sana viongozi na watendaji katika taasisi zote za umma kutenda haki ili wananchi wapate huduma stahiki.

“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya kumsaidia Mhe. Rais kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora ninawahakikishia kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita itajikita katika misingi ya haki ili kila mmoja wetu apate haki,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambayo anaiongoza imeendelea na itaendelea kuwasisitiza viongozi na watumishi wote wa umma katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanatenda haki ili wananchi wafurahie huduma zitolewazo na Serikali kupitia taasisi zake.

Mhe. Mchengerwa amewaomba Watanzania wote kila mmoja kwa imani yake kumuombea Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuwa na afya njema itakayomuwezesha kutimiza ndoto yake ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewata Watanzania wote kuilinda amani kwani Mtume Muhammad S. A. W aliwaasa binadamu wote bila kujali itikadi zao kiimani, kulinda amani na ndio maana Mhe. Rais Samia Suluhu mara kwa mara amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza Watanzania wote kuilinda amani iliyopo.

“Amani ni lazima ianzie miongoni mwetu, ni lazima ianzie kwenye familia zetu, tulizungumze neno amani kwenye familia zetu na kwenye jamii yetu, na tukumbushane kuwa Tanzania ni yetu sote hivyo, tunao wajibu wa kuilinda amani tuliyonayo,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa amewahimiza Watanzania kuwa na mshikamano na kuthaminiana ili taifa liweze kupiga hatua haraka katika maendeleo. 

Waziri Mchengerwa amesema, kumthamini mwanadamu mwenzio ni agizo la Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad S. A. W, hivyo Watanzania hatuna budi kuthaminiana kwani ni agizo la Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Nchi.

Kuhusiana na janga la COVID 19, Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwasisitiza watanzania kupata chanjo ili kujikinga na janga hilo, hivyo amewaomba waumini wa dini zote kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kupata chajo ya UVIKO 19 ili taifa liendelee kuwa na wananchi wenye afya bora ambao watashiriki vema katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi kwa niaba ya waandaaji wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S. A. W, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara Mhe. Suleiman A. Saddiq amesema, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ana nia njema na taifa lake.

Ameongeza kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ana mipango madhubuti ya kuinua uchumi wa taifa letu ili wananchi wapate ajira, huduma nzuri za matibabu, shule na kujenga miundombinu itakayoliwezesha taifa kupiga hatua katika maendeleo na ndio maana anajenga mahusiano na wadau wa maendeleo duniani.

Sherehe hiyo ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika tarehe 19 Oktoba, 2021 iliandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi.

No description available.

Waumini wa dini ya kiislam wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

No description available.

 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara Mhe. Suleiman A. Saddiq akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Mchengerwa kwa niaba ya waandaaji wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

No description available.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishiriki dua ya kumuombea Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

No description available. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiongoza zoezi la kukata keki katika Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa kwa ajili ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.

No description available.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akilishwa keki na Mkurugenzi Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi, iliyoandaliwa kwa ajili ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.

No description available.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akimlisha keki Mkurugenzi Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi, iliyoandaliwa kwa ajili ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.

No description available.

Baadhi ya waumini wa dini ya kiislam wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment