Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa akifungua Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Tamaduni Bagamoyo lililofanyika Usiku wa kuamkia Oktoba 28 hadi 30, 2021 katika viwanja vya Chuo cha Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo(TASUBA) mjini Bagamoyo.
.........................................
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema wizara yake imekusudia kukibadilisha chuo cha TaSUBa kilichopo Bagamoyo kuwa ni chuo cha Sanaa na Utamaduni cha kimataifa, ili kwenda sambamba na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza na kuendeleza Sanaa na Utamaduni hapa nchini.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo mjini Bagamoyo katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa) wakati wa kuzindua rasmi Tamasha la 40 la kimataifa la sanaa na utamaduni ambalo limeanza Tarehe 28 Oktoba 2021 litakalodumu kwa muda wa siku tatu hadi 30 Oktoba 2021.
Alisema kutakuwa na maboresho makubwa yatakayofanyika katika chuo cha TaSUBa ili kukidhi viwango na vigezo vya kimataifa katika maswala Sanaa na Utamaduni.
Aidha, alisema kuwa, maboresho hayo pia yatahusisha taasisi zinazowasaidia wasanii hapa nchini kama vile Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na Chama cha hakimiliki Tanzania (COSOTA) ambapo utendaji kazi wa taasisi hizo unapaswa kuwa wa kiwango cha juu ili wasanii waweze kunufaika kupitia kazi zao.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo itaendelea kushirikiana na wasanii hapa nchini ili kuhakikisha wasanii wanaboreshewa mazingira yao ya kazi pamoja na kulinda haki zao za msingi katika kazi zao.
Alifafanua kuwa, ushirikiano baina wizara na wasanii utasaidia kulinda ajira za wasanii na kazi zao ili waweze kufanya vizuri zaidi na hatimae wao iwe ni chachu ya kuenea ajira kwa vijana wengi walioingia kwenye tasnia ya sanaa.
Akizungumzia Tamasha hilo la 40 la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo, Bashungwa alisema ni Tamasha kubwa na la aina yake kuwahi kutokea na kwamba wizara itaendelea kuboresha mazingira ya maandalizi ili kila mwaka Tamasha liongezeke ubora katika macho ya kitaifa.
Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi mbalimbali ambao wamfanikisha maandalizi ya Tamasha hilo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallaah, Katibu Mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas pamoja Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUB) Dkt. Harbert Makoye.
Aidha, alisema kuwa kukamilika kwa Tamasha hilo la 40 ndio mwanzo wa maandalizi ya Tamasha ka 41 na kwamba amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abasi kuanza maandalizi ya Tamasha 41 hapo mwakani.
Aliwapongeza pia viongozi wa nchi mbalimbali waliohudhuria Tamasha hilo na kusema kuwa hiyo ndio maana ya kuita Tamasha la kimataifa kwa kukusanya kwake wageni kutoka nchi mbalimbali wakiwemo viongozi na vikundi vya sanaa kutoka katika nchi hizo.
Tamasha la 40 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni limezinduliwa rasmi Tarehe 28 Oktoba 2021 na linatarajiwa kufungwa tarehe 30 Oktoba 2021 katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa) ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni Sanaa ni Ajira.
No comments:
Post a Comment