Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kulia) akisikiliza taarifa kuhusu mradi wa ujenzi wa shule ya sekondarri ya wasichana Matai toka kwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Kalambo Shafii Mpenda (kushoto) alipokagua mradi huo ambapo hajaridhishwa na matumizi ya fedha. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera.
.........................................
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameonya watendaji wa serikali Mkoani humo kutotumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali.
Akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi wilayani Kalambo Tarehe 26 oktoba 2021, Mkirikiti hakuridhishwa na namna fedha kiasi cha shilingi milioni 60 zilivyotumika katika ujenzi wa madarasa matatu katika sekondari ya Wasichana Matai .
"Nataka kuona fedha za umma zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan zinatumika kwenye miradi mipya iliyopangwa na wala si kwa miradi viporo kwenye halmashauri yenu ya Kalambo. Sijafurahi kuona mradi huu wa majengo matatu ya darasa shule ya sekondari ya wasichana Matai kutokamilika licha fedha zote milioni 60 kuisha" alisema Mkirikiti
Mkirikiti alibainisha kuwa hataki kuona fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya UVIKO-19 zitumike kwenye miradi ya zamani bali halmashauri ikamilishe miradi viporo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani.
"Kuweka tiles (marumaru) kwenye darasa siyo mbadala wa kutoweka madawati na meza. Tafuteni fedha shule hii ikamilike" aliagiza Mkirikiti.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza viongozi wa wilaya hiyo kuongeza umakini kwenye usimamizi wa miradi pamoja na kuzingatia vigezo vilivyomo ndani ya (BOQ) ili miradi iwe bora na kuendana na thamani ya fedha.
Akizungumza kwenye eneo la mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Shafii Mpenda alisema shule hiyo ya wasichana Matai inatarajiwa kuanza mwezi Januari 2022 kutokana na kutokamilika kwa vigezo vilivyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Elimu Kanda.
Mpenda amemthibitishia Mkuu wa Mkoa kuwa amejipanga kushirikiana na watendaji wenzake kusimamia matumizi ya fedha kwenye miradi na kuepusha ubadhilifu unaoweza kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati.
Mkuu huyo wa Mkoa amenza ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani Kalambo ambapo atakagua miradi ya maendeleo, kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za kukuza uchumi na kuelimisha juu ya kujiandaa na zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika mwakani.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akisalimiana na wajumbe wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Kalambo leo alipoanza ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo. Nyuma yake ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera (aliyevaa shati jeupe).
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akikagua mlango uliotumika kwenye ujenzi wa madarasa mawili shule ya sekondari Matai wasichana ambapo amebaini kukiukwa kwa vigezo vilivyoaninishwa kwenye (BOQ) kutokana vifaa kuonekana kuwa na ubora hafifu.
Watumishi wa Halamshauri ya Wilaya ya Kalambo wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti leo wakati alipoanza ziara ya kikazi wilayani humo.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)
No comments:
Post a Comment