Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia
Evarest Ndikilo akimkabidhi kombe la ushindi nahodha wa timu ya Migomba Maulid
Mtupa baada ya kuibuka mabingwa wa kombe la IGP Sirro (Sirro Cup 2018 Kibiti)
kwa kuichapa Mjawa kwa penati 12 kwa 11 katika uwanja wa Samora Kibiti.
..........................
Na
Jeshi la Polisi.
Timu
ya Migomba kutoka Wilayani Rufiji mkoani Pwani wametawazwa kuwa mabingwa wa
kombe la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro (Sirro Cup 2018 Kibiti)
baada ya kuichapa timu ya Mjawa ya Wilayani Kibiti kwa mikwaju ya penati 12-11
katika fainali iliyopigwa katika uwanja wa Samora Kibiti.
Mchezo
huo ulikuwa mkali kwa dakika zote tisini ambapo kila timu ilijitahidi kutafuta
nafasi lakini mpaka dakika tisini zinakamilika hakuna timu iliyoweza kuona
nyavu za timu pinzani na hivyo kuamuriwa kupigwa kwa mikwaju hiyo iliyopelekea
Migomba kuibuka mabingwa.
Kutokana
na ushindi huo Migomba walikabidhiwa kombe, pesa taslimu shilingi milioni moja
na seti moja ya jezi huku Mjawa wakipata fedha taslimu laki tano na seti moja
ya jezi wakati mshindi wa tatu timu ya Mipeko alipata fedha taslimu laki tatu
na seti moja ya jezi.
Akizungumza
baada ya kuwakabidhi zawadi mabingwa hao, Mkuu wa Mkoa wa Pwani amemuomba IGP
Simon Sirro kuendelea kuandaa kombe hilo
kwa kuwa limesaidia kuinua vipaji vya vijana wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na
Rufiji na kuimarisha usalama kupitia michezo.
“Bila
usalama tusingekuwepo leo hii hapa, hivyo nawaasa kuendelea kutoa taarifa za
uhalifu ili zifanyiwe kazi kwa maana bila usalama hii burudani tusingeiona hapa
na namuomba IGP mwakani tena afanye hivi hivi” Alisema Ndikilo.
Kwa
Upande wake Mkuu wa Kitengo cha Michezo ndani ya Jeshi la Polisi Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP) Philip Kalangi alisema jumla ya timu 52 kutoka Wilaya
za Mkuranga, Kibiti na Rufiji zilishiriki michezo hiyo iliyobeba kauli mbiu ya
Kibiti Salama, Jamii Salama ikiwa na lengo la kuwakutanisha wakazi wa maeneo
hayo kupitia michezo na kupiga vita uhalifu.
Kalangi
alisema Programu hiyo ya michezo inafanywa pia katika mikoa mbalimbali kupitia
kwa Wakuu wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya na ni endelevu ili
kusaidia ushirikishwaji wa jamii katika mapambano dhidi ya uhalifu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Pwani Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Chatanda akimkabidhi seti jezi nahodha
wa timu ya Mjawa Bakari Tuga kutoka Kibiti baada ya kushika nafasi ya pili
katika kombe la IGP Sirro (Sirro Cup 2018 Kibiti) iliyoikutanisha timu hiyo na
Migomba kutoka Rufiji katika uwanja wa Samora Kibiti. Migomba walifanikiwa
kutwaa ubingwa baada ya kuichapa Mjawa penati 12 kwa 11.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia
Evarest Ndikilo akisalimiana na Wachezaji wa timu ya Migomba kutoka Rufiji
kabla ya kuanza kwa fainali ya kombe la IGP Sirro (Sirro Cup 2018 Kibiti)
iliyoikutanisha timu hiyo na Mjawa kutoka Kibiti katika uwanja wa Samora Kibiti.
Migomba walifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuichapa Mjawa penati 12 kwa 11.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia
Evarest Ndikilo akisalimiana na Wachezaji wa timu ya Mjawa kutoka Kibiti kabla
ya kuanza kwa fainali ya kombe la IGP Sirro (Sirro Cup 2018 Kibiti)
iliyoikutanisha timu hiyo na Migomba kutoka Rufiji katika uwanja wa Samora Kibiti.
Migomba walifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuichapa Mjawa penati 12 kwa 11.
Picha zote na Jeshi la Polisi
No comments:
Post a Comment